Maazimio Yetu Baada ya Ramadhani
بسم الله الرحمن الرحيم
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka huu 1440H umemalizika. Kilichobaki nikuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu SW Akubali funga na ibada zetu tulizozitekeleza na kuyapata manufaa ya mwezi huo. Manufaa ambayo ni kwa kuitazama na kuichukulia Ramadhani kama njia ya kufikia lengo na sio lengo lenyewe. Hivyo, baada kumalizika Ramadhani yapasa kuitafakari na kuweka maazimio ya kuondoka nayo kuishi nayo katika miezi mingine iliyobaki katika mwaka.
1. Kutafuta muandamo wa mwezi na kutegemea tangazo la kiongozi.
Kuelekea Ramadhani kila Muislamu alifahamu hakuna kufunga bila ya mwezi kuandama, yaani kila ibada ina mazingira yake ya kuitekeleza. Mfano, hakuna Hija ila mwezi maalum wa Dhul hija na mahali maalum ambapo ni Makka, hakuna swala bila ya udhu nk. Hivyo, kwa upande wa mwezi wa Ramadhani zilifanyika juhudi za kubaini muandamo (mazingira ya kutekeleza ibada). Hili ni kwa sababu Ummah wa Kiislamu unakiri kiasili juu uwajibu wa utekelezaji wa sharia za Kiislamu, na kwamba Uislamu una muongozo wake kwa kila jambo.
Pia tumeshuhudia ulazima wa uwepo wa kiongozi, hadi kufikia kuacha ufahamu na uhalisia kwa baadhi ya watu binafsi kushikamana na tamko la kiongozi juu ya muandamo. Kila mmoja kwa tafsiri yake kwamba kiongozi wa Jumuiya anayoikubali ndiye sahihi. Kukakosekana kiongozi mmoja wa Ummah mzima. Hatuna budi kuazimia kufanya juhudi na kuunganisha nguvu ili kupata Kiongozi mmoja wa Ummah wa Kiislamu kwa ulimwengu ili atuunganishe kwa mujibu wa ahkamu zote za kisheria.
2. Kukubali na kufuata maagizo ya Qur’an.
Kufunga Ramadhani ni utekelezaji wa Qur’an tukufu (2:283) iliyotuwajibisha ibada hiyo. Hata hivyo, zipo aya nyingi nyingine za Qur’an za maamrisho na makatazo lakini kwa bahati mbaya hazipewi uzito kama huu. Mfano kuna aya ya kisasi (2:178) inayowajibisha kulipa kisasi chini ya Qadhi aliyeteuliwa na Khalifah. Aidha, kuna aya iliyofaradhisha jihadi (2:216) nk. Haya yote ni katika mambo ya lazima ya kuazimia na kushikama nayo ili kujifunga na sharia za Allah SW na mwenendo wa Mtume SAW katika matendo yetu yote kwa kila sekunde. Anayeamrisha na kukataza ni Mmoja, Ndiye pia Anayehalalisha na kuharamisha, naye ni Allah SW, haitupasi kubagua wala kudogosha chochote katika amri na makatazo Yake.
3. Ukarimu na Utu.
Tumeshuhudia kuwepo kwa kiwango kikubwa tofauti na miezi mingine ya moyo wa kutoa kwa wenye nacho kuwapatia wahitaji, wasionacho. Dunia inashuhudia ongezo la ombaomba (wasionacho), wanaokufa njaa, kuongezeka huku baadhi ya watu (walionacho) wakisaza na kutupa vyakula. Haya ni matokeo ya fikra na ufahamu wa maisha uliyojengwa na ubepari katika mabongo ya watu na kuathiri hisia zao. Yatupasa kuazimia kubadili mfumo huu wa kibepari, na mahala pake tuweke fikra za mfumo wa Kiislamu ambao hulenga haswa kumjengea binadamu ufahamu unaojali utu na kuthamini ubinaadamu baada ya mtu kujitambua mwenyewe kwanza.
4. Kulingania dola ya Khilafah.
Tumeshuhudia uasi wa makusudi dhidi ya sharia za Mungu SW kuelekea Ramadhani kwa jina la ‘vunja jungu’. Baadhi ya Waislamu waliamua kuacha tabia na shughuli zao ambazo zipo kinyume na sharia za Allah SW, kuacha huku kulianzia na ‘kuyaaga maasi hayo’ kwa kujipinda kwa nguvu kubwa kutenda yaliyo mema. Wengi wao baada ya Ramadhani waliamua kulifinyanga tena ‘jungu’ kwa kuyarejea tena maisha ya kijahili kuanzia siku ya Eid, astaghafirullah !
Bila ya shaka baada ya msukumo binafsi kuelekea Ramadhani kumuwezesha Muislamu kuyaacha maovu, yahitajika apate msaada wa nguvu ya nje yake ya kuzuiya kulifinyanga ‘jungu’. Jukumu hilo ni la serikali, uwepo wa serikali ya Khilafah kutaondoa mazingira ya uwezekano wa watu kutenda mambo maovu wazi wazi. Na hili halipatikani kamwe katika serikali hizi zilizopo leo ulimwenguni ambazo huongozwa kwa usekula na matamanio ya binadamu, bali yanawezekana kwa serikali ya Kiislamu, Khilafah. Tuazimie kufuata njia ya Mtume SAAW kuitafuta Serikali ya Kiislamu. Serkali ambayo kila utendaji wake umejifunga na sharia za Allah SW, ndiyo pekee yenye kuweza kutatua kero zote za maisha haya.
Haya ni machache miongoni mwa mengi ya kujifunza na kuazimia kutokana na Ramadhani. Ni mambo ya msingi zaidi kuyazingatia na kuweka mikakati ya kuyadumisha kwa kina na upana ili athari zake zilete tafsiri halisi na sahihi ya Ramadhani, sio lengo bali ni njia ya kuliendea lengo la kuumbwa binadamu (kuabudu) na lengo la kuwepo Uislamu na Waislamu (kuongoza ulimwengu) katika nyanja zote za maisha.
Risala ya Wiki No. 45
21 Shawwal 1440 Hijri /24 Juni 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.