Maana ya Shahada Laa ilaha ila Llah

Tamko la ( لا إله إلا الله ) (Laa ilaha illa Allah) linalojulikana kama Shahada hutamkwa na Waislamu. Tamko linalojulikana pia kama tamko la Tawhid (upwekeshaji) ndio taklif ya kwanza kwa mtu yoyote yule atakaye kuingia kwa Uislamu. Kwenye Makala haya tutaliangalia  tamko hili kwa kina zaidi ili tufahamu uzito wake na maana halisi yake. Pia ni muhimu kufahamu kuwa tamko hili la shahada ndiyo msingi wa Uislamu na msingi wa sheria zake yaani hukumu.

Tamko la shahada limeanza kwa herufi ya lam-alif ( (لا ambapo hapa imebeba maana ya kukanusha jinsi zote ( لا النافية للجنس ) zile hivyo maana yake ni kusema hakuna/ hapana. Laa sampuli hii huingia kwenye sentensi inayoanzishwa kwa jina. Kilugha ya Kiarabu sentensi hugawika mara mbili: Inayoanza kwa jina nayo huitwa (Jumla Ismiyyah) na nyengine ni inayoanza kwa kitendo (Jumla fiiliyyah). Kwa kuwa hapa imeingia kwenye sentensi ya kijina basi hubeba maana ya kutilia mkazo na kuthibitisha. Kwa hivyo hapa kuna msisitizo wa ukanushaji wa habari zinazofuata. Kwa maana hii inaposemwa ‘laa ilaha’ لا اله ) (maana yake ni kukanusha kabisa kuwa hakuna yeyote au chochote chenye kustahiki kuabudiwa. Kwa sehemu hii itakuwa ina maana watu wanapaswa kukanusha ibada kwa chochote kile na wala haimaanishi hakuna kuabudu kwa sababu ibada ni sehemu ya maumbile ya wanadamu. Ni maumbile ya kibinadamu kumtukuza Mungu hali inayomsukuma mwanadamu yeyote yule kuabudu chochote. Fauka ya haya kitarekh ya Mwanadamu hakukosekaniwa mahala pa kuabudu na cha kuabudiwa. Hiyyo ibada ni sifa/ishara ya kuweko na umbile kwa mwanadamu la kutukuza dini.

Kwa maana haya ndiyo mwanadamu anapofanya ibada huwa ni mwenye kuhisi raha kwani katika huko kuabudu kwake atakuwa ameshibisha ile ghariza yake ya Kidini. Kuabudu kwa hali ya umaumbile hakufai kuachiwe kihamasa tu bali lazima kutumike akili pamoja na hisia ili kutambua nani apaswaye kupewa haki hii ya kumwabudu. Na hii ndiyo maana watu waliabudu viumbe kama vile majini, mawe, miti, watu na kadhalika.

Tukija kwa neno la اله (ilaha’) ni jina la chochote/yeyote anayeabudiwa yaani waarabu huita chochote au yeyote mwenye kuabudiwa kwa jina hilo. Jina hili hapa lipo katika sifa ya umoja na pia maana yake ya kisheria na ya kilugha humaanisha maana moja tu nayo ni chochote / yeyote anayeabudiwa. Kwa muktadha huu, maana ya neno hili limefungika tu kwa maana moja ya kilugha na kisheria kwa tamko la Ilaha ni katika dalili kubwa na rehema ya Mwenyezi Mungu katika kusimamisha hoja kwa watu wote wasiamini mungu mwengine ila Mwenyezi Mungu pekee. Fauka ya haya Ilaha hapa sio lenya kuashiria jinsi maalum, aina hii ya jina huitwa nakira نكرة *) (jina ambalo halikufungika) nalo likitanguliwa na herufi ya ‘laa’ humaanisha hakuna ruhusa ya kuabudu chochote/yeyote. Hekima ya hilo ni kutaka kusiweko na mwenye kuabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu pekee. Na hapa ndiyo yaja uzito wa tamko hili la Tawhid.

Ama kuhusu ibara ya ila llah ( الا الله ); nayo ni kuwa hii ni ibara ya pili inayofuata na kutoa jibu la yule anayestahiki kuabudiwa. Kwenye lugha ya kiarabu herufi ya ILLA hutumika katika kuvua jambo au kitu huku ikithibitisha baada ya kukanusha. Kwa maana itakua Hakuna apasaye kuabudiwa isipokuwa aliye na haki ya
kuabudiwa ni Mwenyezi Mungu pekee. Na haya ndiyo maelezo ya pili kwenye shahada yana mkalifisha
mwenye kuitamka kutoabudu yeyote kinyume na Mwenyezi Mungu. Kushuhudia kuwa Mwenyezi Mungu
(swt) ndiye anayestahiki kuabudiwa kama inavyoelezwa kwenye shahada ni amri kwa Mwanadamu awe na Imani ya kihakika ya kumuamini Mwenyezi Mungu. Na kuwa yeyote asiyeamini hivyo anakuwa kafiri. Kama vilevile kutamka shahada kuna maanisha kuwa hakuna yeyote anayestahiki kuabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu nako pia ni amri ya kukanusha miungu. Kupambika kwa Mwenyezi Mungu kuwa peke yake ndiye astahikiye kuabudiwa kwa haki kama ilivyo katika tamko hili la Tawhid ni kuelezwa kwa njia ya kukalifishwa na kutakikana watu wakubali na kusadikisha jambo hili tena pasina na shaka yoyote. Maelezo haya ni kutakikana kuitakidi msimamo huu ambao anayeitakidi kinyume chake au kupinga msimamo huu basi anakuwa kafiri. Aidha kuelezwa kuwa hakuna mungu mwengine ila Mwenyezi Mungu kama yalivyo maelezo ya shahada ni kutakikana kuamini mungu mmoja tu naye si mwengine ila Allah. Na yeyote atakayeamini uwepo wa mungu mwengine kinyume ya Allah basi ni kafiri vilevile.

Aidha shahada inamaanisha yeyote anayeabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu ni urongo na batili:
فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِالَّلِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَ انفِصَامَ لَهَا وَاللَُّ سَمِيعٌ عَلِيمٌ
Basi anaye mkataa shetani (Kila chenye kuabudiwa kinyume na MwenyeziMungu) na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka yeye amekamata kishikio madhubuti kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. [Al-Baqara: 256]

Kufikia hapa ni kuwa kumwamini MwenyeziMungu sio kuwa ni kuamini tu kwamba yeye ni Muumbaji bali yeye ni mwenye kustahiki kufanyiwa ibada. Kwa maana haya shahada ya Laa ilaha illa LLah humaanisha
hakuna yeyote anayestahiki kuabudiwa ila Allah. Hii ni kusema kwamba kalima hii inamwamrisha Muislamu kufungamanisha Imani yake moja kwa moja katika kumuabudu Mwenyezi Mungu (swt). Muislamu anaamrishwa kwa kutamka kalima hii kumtukuza Mwenyezi Mungu (swt) kwani Yeye ni muumbaji wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.

Katika ulimwengu wa kileo hasa ulimwengu wa Kimagharibi suala la kumwamini Mwenyezi Mungu (swt) huchukuliwa kuwa ni nadharia tu ambayo ukweli wake sio sana. Wanashikilia kwamba kuamini kuwepo
kwa mungu ni fikra nzuri na husaidia mwanadamu kuepuka mabaya. Mtizamo huu ni hatari na kosa kubwa
sana kwani masuala ya kumwamini Mwenyezi Mungu (swt) sio nadharia bali ni ukweli usokuwa na shaka.

Uislamu ukabainisha vizuri njia maalumu ya kumwamini Mwenyezi Mungu (swt) nayo ni kuwa Imani ya kuweko kwake ni ile inayotokamana na kukinai kwa akili na kutafakari utendakazi wake na Quran imebainisha wazi Imani ya kuweko kwa Allah (swt) Anayestahiki kuabudia.
Asema Mwenyezi Mungu (swt):

وَإِلَٰهُكُمْ إِلَٰهٌ وَاحِدٌ لَّ إِلَٰهَ إِلَّ هُوَ الرَّحْمَٰنُ الرَّحِيمُ
“Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.”
[Al-Baqara: 163]

Kuelewa maana ya shahada ni jambo muhimu sana kwa Waislamu kwani haitakikani kwa mtu kushuhudia kitu asichokijua. Kwa bahati mbaya leo kutojua maana ya shahada ni moja wapo ya ujinga mkubwa sana licha ya wengi kuitamka shahada. Maisha yetu leo yako mbali mno na maana halisi ya shahada. Kwa hali hii Viongozi makhaini katika biladi za Kiislamu wanatawala maisha ya watu kwa kutegemea misingi ya Kisekula. Shahada leo imefungwa ndani ya Misikiti na kila anayejaribu kutanua maana yake hadi iongoze kwa maisha jumla basi hupachikwa jina kwa yeye ni mwenye misimamo mikali. Hivyo ni muhimu sana kufahamu maana halisi ya shahada yetu.
Shabani Mwalimu
Mwakilishi Kwa Vyombo Vya Habari Hizb ut Tahrir Kenya

Inatoka Jarida la Uqab: 23.    https://hizb.or.tz/2018/12/01/uqab-23/

Maoni hayajaruhusiwa.