Maafa Ya Vita Ya Kongo: Chanzo Chake Wakoloni
بسم الله الرحمن الرحيم
Jumapili tarehe 26/01/2025 waasi wa M23 waliingia mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na siku moja baadaye yaani Jumatatu 27/01/2025 walitangaza kuuchukua na kuudhibiti mji huo. Katika mapigano hayo zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha na zaidi ya watu 1000 wamejeruhiwa
Huu ni muendelezo wa vita ya muda mrefu ya Kongo, vita ambayo vimekuwepo mara tu baada ya Kongo kupata uhuru wake wa bendera mwaka 1960 kutoka kwa Ubelgiji, ikawa chini ya ukoloni wa Uingereza tangu kipindi cha Raisi wa kwanza wa nchi hiyo Joseph Kasa-Vubu, na Marekani ikawa na shauku kubwa ya taifa hilo kupitia Kibaraka wake Patrice Lumumba.
Uingereza mara baada ya kuona ushawishi wa Lumumba unakuwa kwa kasi, ikamuua kuzuiya ushawishi wa Marekani. Kisha ikawa Uingereza inabadili marais wa Kongo kila mara pale inapoona raisi fulani kukosa nguvu na ushawishi kupitia mapinduzi mpaka kufikia kwa Felix Tshsekedi ambaye alipatikana kwa makubaliano na uchaguzi na mtangulizi wake Joseph Kabila. Muda wote huu Marekani imekuwa ikijaribu kuichukua Kongo mikononi mwa Uingereza bila mafanikio
Kwahiyo, Marekani imekuwa ikitumia karata ya ukabila kupitia watawala wenye asili ya kitutsi katika baadhi ya nchi za maziwa makuu hususan Rwanda, Uganda ili kuunga mkono waasi wa Kongo kama vile M23 ili kuitaabisha serikali ya Kinshasa inayoungwa mkono na Uingereza, Ubelgiji na Ufaransa (Ulaya) ili kumakinisha na kuhakikisha maslahi yake ndani ya Kongo yanatamalaki. Pia Marekani katika mpango huutumia Umoja wa Mataifa(UN).
Uingereza kwa upande wake imekuwa ikitumia jumuiya yake ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na watawala wenye ushawishi wa kisiasa katika kanda yaani Tanzania, Afrika Kusini na Zimbabwe katika kudhibiti hatua za Marekani na kumakinisha serikali ya Kinshasa.
Kuhusu watawala wa Rwanda,Uganda kuunga mkono waasi wa Kongo, hii inatokana na ukweli kuwa waasi wale wengi wao ni watutsi, na viongozi wa (Rwanda na Uganda) ni watutsi. Kwahiyo, Marekani anadandia dhana ya ‘ututsi’ kuwatumia katika vita vya Kongo.
Kauli za viongozi hao (wa Rwanda na Uganda) za kuunga mkono waasi hao wa M23 zipo wazi. Kwa mfano, Raisi wa Rwanda Paul Kagame anasema wazi kuwa M23 si waasi kutoka Rwanda, bali ni wakongo wenye asili ya Rwanda ambao wana haki ya kuishi Kongo kama wakongo wengine, na kuwa walinda amani wa SADC wanasaidia serikali ya Kongo kuua raia wake yenyewe.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Kijamii wa x, 30/01/2025 alisema Kagame kuituhumu SADC: “SAMIDRC si kikosi cha kulinda amani, na haina nafasi katika hali hii. Iliidhinishwa na SADC kama kikosi cha kijeshi kinachojihusisha na operesheni za kivita ili kusaidia Serikali ya DRC kupambana na watu wake yenyewe”
Clémentine de Montjoye, mtafiti mwandamizi wa masuala ya Afrika kutoka Shirika la Haki za Binadamu (Human Rights Watch) aliiambia BBC kwamba picha za kijiografia zilionesha wanajeshi wa Rwanda wakiwa huko Sake, mji ulio nje kidogo ya Goma wiki iliyopita. (BBC 29/01/2025)
Katika mwezi Disemba 2024, M23 ilikusanya kiasi cha $800,000 (£643,000) kwa mwezi kutokana na ushuru Coltan huko Rubaya na kuhakikisha kwamba karibu tani 120 za madini hayo yanayotamaniwa yanatumwa moja kwa moja nchini Rwanda kila baada ya wiki nne (BBC 29/01/2025).
Hii inaonesha wazi kuwa Rwanda inaunga mkono mkono waasi wa M23 na kamwe haiungi mkono juhudi za SADC.
Amma kuhusu Rwanda kuungwa mkono na Marekani ni jambo la kihistoria, kwani Kagame amepata mafunzo yake ya kijeshi nchini Marekani katika kambi ya kijeshi ya Fort Leavenworth, Kansas kabla ya kurudi na kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya Kihutu iliyokuwa ikiungwa mkono na Ufaransa mwaka 1994. Kisha Kagame akawa makamo wa raisi chini ya raisi Pasteur Bizimungu (mhutu) aliyekuwa rais wa Rwanda mwaka 1994 kupitia chama cha Rwanda Patriotic Front kilichoanzishwa na Kagame na watutsi waliokuwa Uganda. Ni jambo maarufu kuwa watutsi waliokuwa Uganda pia walikuwa wakimuunga mkono (mtutsi mwenzao) Yoweri Museveni, kibaraka mwingine wa Marekani dhidi ya Milton Obote (kibaraka wa Uingereza). Hatimae Kagame akadiriki kuwa raisi wa Rwanda tangu mwaka 2000, kwani chama cha RPF, japo kilikuwa na baadhi ya wahutu, bado kilikuwa na watustsi wengi, kiasi cha kumzidi nguvu raisi Bizimungu na kupelekea kujiuzulu kwake.
Jamii ya Watutsi ndani ya Kongo imekuwepo kwa makarne ndani ya mashariki ya Kongo, japo upo uwezekano wa kuongezwa jamii hiyo kwa makusudi na Rwanda. Mnamo mwaka 2006 jamii hiyo chini ya viongozi wao wa Kitutsi ilijiunda kama chama cha CNDP (National Congress for the Defence of the People) kutokana na madai yao ya kuongezeka kwa mvutano wa kikabila kati yao, wahutu na makundi mengine, hasa baada ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda na kutaka watambuliwe rasmi haki zao ndani ya Kongo. Mwito mkuu wa CNDP chini ya Laurent Nkunda ulikuwa ni kulinda jamii za Watutsi ndani ya Kongo.
Mnamo Machi 2009, makubaliano ya amani yalifikiwa ya kuunganisha vikosi vya CNDP katika jeshi la Kongo, lakini mvutano uliendelea, na kwa mujibu wa CNDP mawafikiano hayakutekelezwa, hali iliyosababisha kuundwa kwa M23 mnamo 2012. Jina la M23 linatokana na muda walipofanya makubaliano ya amani ya Machi 23, 2009.
Kwa hivyo, jamii hizo tatu za Watutsi, wa Rawanda, Uganda na Kongo Mashariki zimekuwa turufu adhimu kwa Marekani katika kufanikisha unyonyaji wa rasilmali ndani ya Kongo na kuondoa athari ya mabwana wakongwe, yaani Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji au tuseme ushawishi wa Ulaya kwa jumla.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika taarifa yake 28/01/2025 alizungumza na Rais wa Rwanda Paul Kagame. Katika taarifa hiyo Rubio alisisitiza kuwa: “Marekani inasikitishwa sana na kuongezeka kwa mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC, hasa kuanguka kwa Goma chini ya kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda… alihimiza kusitishwa kwa mapigano mara moja”
Kisha, kufuatia maelekezo haya ya kusitisha mapigano akaongea Kagame kesho yake 29/01/2025. “Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema alikubaliana na serikali ya Marekani kuhusu hitaji la kusitishwa kwa mapigano mashariki mwa Kongo, lakini hakutoa dalili ya kusalimisha wito wa kuwataka wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 wanaounga mkono kuondoka Goma” (Reuters 29/01/2025)
Taarifa hizi mbili zinaonesha kuwa: kwanza ni kweli kuwa Rwanda inaunga mkono M23 kwa mujibu wa taarifa ya Marekani, pili ni kuwa Rwanda inapokea maagizo kutoka Marekani, kwani mara baada ya kuambiwa kusitisha vita amesitisha mara moja.
Kuhusu Uingereza kuiunga mkono Kongo (DRC) inajionesha kupitia kauli zake. Taarifa rasmi ya Ofisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya Uingereza iliyotolewa 30/01/2025 inasema: “Uingereza inalaani uvamizi wa Goma na maeneo mengine mashariki mwa DRC na M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) kama ukiukaji usiokubalika wa mamlaka ya DRC… Uingereza inatoa wito wa kuondolewa mara moja kwa jeshi la RDF yote kutoka eneo la Kongo….Uingereza inazingatia kikamilifu hatua zinazofuata, pamoja na washirika wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa mapitio ya msaada wote wa Uingereza kwa Rwanda”
Hii inaonesha wazi kuwa serikali ya Uingereza inaunga mkono serikali ya Kinshasa ya Rais Felix Tshsekedi kama ilivyofanya kwa watangulizi wake, huku Marekani akijaribu kunyakua tonge hiyo bila mafanikio yaliyotamalaki mpaka sasa
Kuhusu SADC kuunga mkono Kongo, hili nalo linatokana na uhalisia kuwa mataifa yaliyounda jumuiya hiyo ni vibaraka wa Uingereza ambao kwa miaka mingi wanatetea maslahi ya Uingereza na kuhakikisha wanabakiza maslahi ya ukoloni mamboleo wa Uingereza dhidi ya Marekani.
Harakati za kupigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika hazikuwa ila kubakiza ukoloni wa Uingereza na kuzuiya ujio wa Marekani katika makoloni ya Uingereza. Kwahiyo, SADC inatumiwa na Uingereza na inaunga mkono serikali ya Kongo.
Taarifa rasmi ya Sekretarieti ya SADC iliyotolewa 25/01/2025 inasema kuwa:” SADC inasisitiza dhamira yake isiyoyumba ya kuendelea kuunga mkono DRC katika harakati zake za kulinda uhuru wake, mamlaka yake na uadilifu wa eneo lake, pamoja na amani endelevu, usalama na maendeleo”. Hii inamaanisha kuwa SADC wanaunga mkono serikali ya DRC
Kuhusu hatua za Marekani za hivi karibuni za kuzuiya kuenea kwa vita nchini Kongo kwa sasa na kumuamrisha Kagame kuhakikisha amani na usitishaji wa mapigano inaweza kuwa ni kwa sababu ya uwekezaji wake katika mradi wa ukanda wa Lobito (Lobito Corridor) ambapo amewekaza Dola milioni 560 kati ya jumla ya Dola 800 zinazohitakika katika ujenzi wa reli ya kisasa kutoka bandari ya Lobito nchini Angola mpaka Kolwezi nchini Kongo. Hali ya kukosekana utulivu kunaweza kuthiri maendeleo ya mradi huu.
Huu ndiyo uhalisia wa vita ya Kongo, ni vita ya kimaslahi kati ya wakoloni wa Ulaya hasa Uingereza dhidi ya Marekani. Katika vita yao hii wakoloni hawa wanatumia watawala vibaraka katika Afrika na jumuiya za vibaraka hao katika kufikia malengo yao.
Hii inafanya Kongo na Afrika kiujumla kuendelea kuwa vibaraka na wafanyakazi wa wakoloni huku wakiuwa watu wao kwa ahadi za utawala na ulinzi kutoka kwa wakoloni wa kimagharibi na Marekani.
Licha ya kuwa na rasilimali nyingi lakini Afrika tangu ilipovamiwa na ukoloni haijanufaika na rasilimali zake zinazoendelea kuporwa kila siku kwa gharama ya damu na maisha yao yenyewe kwa vita visivyoisha.
Afrika na ulimwengu kwa jumla unahitaji mfumo wa uadilifu ambao ni Uislamu. Chini ya dola yake ya Khilafah itadhamini matumizi bora ya rasilmali zake, huku ikizingatia amani na usalama wa raia, kinyume na mashaka na madhila ya ubepari leo ambapo umeugeuza utajiri wa Kongo na pengine kama laana kwa watu wake kwa vita vya kutengenewza visivyokwisha.
Risala ya Wiki No. 199
6 Shaaban 1446 Hijri | 5 Februari 2025 Miladi
Afisi Ya Habari – Hizb Ut Tahrir Tanzania
Imeandikwa na Said Bitomwa
Maoni hayajaruhusiwa.