Kwanini Katika Nchi Changa Kunakuwa na Khofu na Vurugu Katika Uchaguzi?
بسم الله الرحمن الرحيم
Ni jambo maarufu katika nchi changa mara nyingi nyakati za chaguzi, badala ya kuwa siku za furaha na utulivu kwa kupitisha tu mchakato wa kubadilishana uongozi, kunakuwa na khofu kubwa ya vurugu, vitisho katika siku za uchaguzi kwa sababu zifuatazo:
- Watawala katika nchi changa huwa na khofu kubwa, na hii ni kutokana na kiwango kikubwa cha ufisadi na madudu mengi waliyofanya kwa rasilmali na kwa raia wao. Hivyo, watawala hupambana kufa kupona ili kurudi au walau kulazimisha mtu ambaye atawalinda ashike hatamu baada yao.
- Hakuna taasisi thabiti za kusimamia chaguzi ipasavyo kwa kujitegemea. Taasisi ‘majina’ katika nchi changa huwa ni maamuzi ya mtu mmoja au wawili juu ya kila kitu, licha ya kuwepo majina mengi yanayodhaniwa ni taasisi, lakini hazina sura ya udhati ya utaasisi unaojitegemea na kuwa huru na kujitosheleza kiutendaji. Hili unaweza kuona hata katika nchi kama Kenya ambapo taasisi zao za uchaguzi walau zimetangulia kiasi fulani kulinganisha na nchi kama Tanzania, hata hivyo, zimekuwa zikifanya kazi katika changamoto kubwa na mazingira ya vitisho na khofu kubwa.
- Licha ya kuwa wanasiasa wote chini ya mfumo wa ubepari, iwe nchi changa zinazoiga mfumo huo au nchi kubwa zilizobeba mfumo huo ipasavyo husukumwa na maslahi binafsi, katika nchi changa hili limeshtadi zaidi, kwa kuwa kuna ukosefu wa taasisi kuwadhibiti watawala, kinyume na madola makubwa ya kibepari ambapo utaasisi unaojitegemea kwa kiasi fulani katika vyombo vyao unawapa khofu fulani watawala na kuwafanya kula kimahesabu katika vitendo vyao vya ufisadi nk. Zaidi ya hayo nchi changa tofauti na nchi kubwa zenye mfumo, hazikujengwa juu ya maslahi mapana ya kinchi, na hii ni kimaumbile, kwa kuwa ni nchi ‘tawaliwa’ ndio maana hazina sera thabiti za ndani na nje kama kujitawanya na kujijenga, bali kila mtawala huja na ajenda ya maslahi ya tumbo lake, familia yake na wapambe wake. Hivyo kwa mtawala wa aina hiyo kwake uchaguzi huwa ni kufa na kupona kuhifadhi maslahi yake hata ikiwa ni kwa gharama ya kumaliza wengine.
- Vyama vya siasa katika nchi changa hususan vilivyopigania ‘uhuru wa bendera’ na kutawala kwa muda mrefu katika zama za mfumo wa chama kimoja zimerithi dhana ya kikoloni, ya wao kuona wana ‘haki miliki’ ya kutawala nchi peke yao. Urathi huu wa kikoloni waliupata kwa kuwa walitawala kwa muda mrefu katika mfumo wa chama kimoja na kujengwa nao na mabepari, kiasi cha watawala hao licha ya kujinadi kuwa walimfukuza mkoloni, lakini wakaingia katika tabia ile ile ya mkoloni kuona wao wana haki zaidi kutawala. Katika hali kama hiyo mfumo wa vyama vingi kwao umekuja kama kuwaondoshea haki yao ya msingi, na hivyo wanahisi wana haki ya kuilinda kwa gharama yoyote. Hivyo, sio ajabu kusikia wakisema ushindi upatikane kwa namna yoyote.
- Wananchi ambao ndio watawaliwa wamekosa imani na vyombo vya usimamizi wa uchaguzi ikiwemo pia vyombo vya ulinzi, kwa kuwa asili huwa havisimami juu ya mstari wa kati na kati. Katika hali kama hiyo ya kutoaminiana, likitokea jambo dogo tu huwa ni mripuko mkubwa wa vurugu katika nchi.
- Katika nchi changa mara zote vyama vya siasa, viwe vilivyomo madarakani au vya upinzani, huwa kimsingi sio milki ya wananchi, bali huwa ni milki ya madola makubwa, kwa leo vyama amma viko katika himaya au vinaungwa mkono na Marekani au Uingereza ambayo mara nyingi hujumuika na Jumuiya ya Ulaya. Katika hali kama hiyo mabwana hawa wa dunia kila mmoja hutaka chama chake kishinde ili kudhamini maslahi yake. Kwa hivyo, asili huwa ni uchaguzi wa wananchi kwa jina tu, lakini kiudhati huwa ni ushindani mkali wa mabeberu kwa mgongo wa raia. Hali hii ni tofauti na chaguzi zao nchini kwao, ambapo vyama huwa vyao wenyewe.
- Katika baadhi ya nchi kama Kenya kuna athari za urathi wa ukabila ulioshtadi katika siasa uliolelewa na kukuzwa tangu zama za wakoloni. Walifanya hivyo kwa kulipatia kabila moja au makabila fulani nafasi zaidi katika utawala kuliko makabila mengine. Ni wazi nyakati za uchaguzi huwa sio tu muhula wa kubadilisha kiongozi mtawala bali huwa ni vita vya watu kutetea na kuhami jamii yao na kabila lao au makabila fulani.
- Nchi kubwa za kibepari daima zimekuwa na uchu wa utajiri na rasilmali mbali mbali zilizomo katika nchi changa, na ndio maana wakazitawala kwa nguvu (ukoloni mkongwe) na hali ya kimataifa ilipobadilika ikabidi wabadilishe mbinu kwa kutoa’uhuru wa bendera’, lakini wakiweka vibaraka wa kudumu chini ya mfumo wa chama kimoja ili wadhamini na kulinda maslahi yao (ukoloni mambo leo). Na baada ya vibaraka hao kuchosha sana wananchi kwa dhulma zao na ukandamizaji wao na kujiri mabadiliko fulani kiulimwengu, nchi za kibepari wakaja na ujanja na mbinu ya kuasisi au kurejesha vyama vingi katika nchi changa. Hivyo, vyama vingi vimeletwa kuja kupoza joto la wananchi baada ya kubanwa na madikteta waliowekwa na wakoloni kulinda maslahi yao.
Kitu muhimu cha kuzingatia kwa makini hapa ni juu ya tabia ya mabepari wakoloni kuwa, wao huangalia kila kitu kwa maslahi yao, na sio maslahi ya wananchi. Na hiyo ndio asili ya mfumo wao wa kibepari. Kwa msingi huo, chaguzi katika nchi changa kwa mabepari ni aina tu ya ‘danganya toto’ kwa wananchi, bali mshindi wao tayari wanae katika mfuko, na ni yule ambaye atadhamini na kulinda maslahi yao, na sio atakayepata kura nyingi. Mawazo ya wingi wa kura wanayo wananchi lakini sio mabepari mabeberu.
Kwa hivyo, unaweza kuona mgombea akashinda kwa kura wazi wazi, lakini hatopewa utawala, na wao madola makubwa wakiwa ndio walioleta mfumo wa vyama vingi wakawa kimya, au wakajifanya kuchukua hatua nyepesi nyepesi za hapa na pale kughilibu ilhali mtawala aliyeshindwa kwa kura wazi wazi akiendelea kutawala kwa kujitanafasi kwa sababu tu anawalindia maslahi yao.
Chaguzi za namna hii ambazo ni maarufu katika nchi changa kimaumbile hutarajiwa kuzaa machungu, khofu na vurugu. Raia waliomchagua mgombea mshindi hutaka mgombea wao atawale, na mtawala aliyepora ushindi kwa baraka za madola ya kibepari na kuungwa mkono nao japo nyuma ya pazi hujizatiti kujilinda kwa hali yoyote.
Yafaa tukumbuke kuwa mabepari wana kanuni yao isemayo: ‘Hawana rafiki wa kudumu, bali wana maslahi yakudumu’. Leo maslahi ya madola makubwa hususan Marekani yametanuka zaidi, kando na rasilmali vitu kama maadini, mafuta, gesi asili nk. Baada ya kuanguka ukomunisti wamejitosa katika vita vya kimfumo dhidi ya mfumo wa Uislamu, na ndio maana wameasisi vita vikali ambavyo yanashirikishwa madola yote yakiwemo madola machanga. Kwa hivyo, kipimo cha maslahi kwao hakizingatii tu kuwalindia rasilmai vitu, lakini pia ni namna gani mtawala atatawala kwa ukali na kwa dhulma dhidi ya Uislamu / ugaidi.
Kinachodhihirika katika michakato ya chaguzi ni wananchi katika nchi changa kutapatapa kutaka mabadiliko ya kisiasa ili yaweze kuzaa matunda ya mabadiliko katika maisha yao, kitu ambacho kwa udhati ni ndoto. Chaguzi huwa hazileti mabadiliko ya kimsingi, kwa kuwa nchi hizi hazikubeba mfumo, bali zaidi ni ‘nchi tawaliwa; zisizokuwa na maamuzi yoyote katika mambo yao msingi. Kunahitajika mfumo mbadala utakaozikomboa nchi hizi kuwa huru na madola ya kibepari na pia kutoa dira thabiti itakayoleta ufanisi katika sekta zote za maisha ya.
20 Oktoba 2020
Maoni hayajaruhusiwa.