Kutokomeza Umasikini Hakuwezekani Chini ya Ubepari

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:
Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia aliyemaliza muda wake nchini Tanzania Bella Bird aliishauri serikali ya Tanzania kuendelea na kuekeza zaidi katika miradi ya kutokomeza umaskini inayogusa maisha ya makundi makubwa ya walalahoi nchini ili kuweza kuyafikia malengo kadhaa ya kimaendeleo. (IPP Media 15 Januari, 2020)

Maoni:
Kampeni ya kupambana na umasikini ni mwito ulilosambaa duniani kote, iwe kitaifa au kimataifa hususan katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Kampeni hiyo inahusisha njia na mbinu mbalimbali zinazochukuliwa kuwa ni suluhisho katika kutokomeza umaskini unaoathiri mamilioni ulimwenguni.

Kuna taasisi nyingi kieneo, kitaifa na kimataifa zinazojihusisha na kinachoitwa mapambano dhidi ya umasikini kwa dhamira ya kuhafifisha dhiki na taabu za jamii ya masikini.
Sera kadhaa zimetungwa ili kuongoza miradi ya kitaifa ya kupambana na umaskini. Tanzania kama zilivyo nchi nyengine zinazoendelea inajihusisha kikamilifu na suala hilo la kupambana na umaskini ikiwa ni utekelezaji wa msimamo wa Mkutano wa Masuala ya Kijamii uliofanyika mjini Copenhagen ndani ya mwaka 1995.

Mkakati wa Tanzania wa Kitaifa wa kupambana na umasikini uliasisiwa mnamo mwaka 1998, na suala la kupambana na umaskini likaunganishwa katika dira ya malengo ya muda mrefu, inayoitwa Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025, (mkakati huo) pia ukihusishwa katika sera za malengo ya muda wa kati, na ndani ya Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (NSGRP).

Na kwa upande wa Zanzibar, suala la sera za kutokomeza umaskini pia nalo likaunganishwa katika Mpango maalum wa Zanzibar wa Kupunguza Umaskini, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020, pia katika Mkakati wa Zanzibar wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (ZSGRP).

Mikakati na miradi yote imedhamiriwa kujihusisha katika suala la kupunguza umaskini wa kipato kwa kutilia nguvu katika uzalishaji, kutengeneza ajira endelevu, kuunda miundo mbinu ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji, usalama wa chakula na upatikanaji wa nishati kwa wengi katika wakaazi wake.
Pia chini ya Sera ya Ukulima na Mifugo kulenga kuleta mabadiliko ya sekta ya kilimo kwa kuifanya sekta hiyo iwe ya kibiashara, kuinua hali za maisha ya watu na kuongeza fursa za upatikanaji wa ardhi na elimu kwa makundi dhaifu na masikini.

Suala nyeti na la msingi la kujiuliza katika qadhia ya kutokomeza umaskini, ni kwanini watu wa mataifa ya nchi zinazoendelea wanaishi katika umaskini wa kutupwa ilhali mataifa yao yana rasilmali zote muhimu na kila aina ya nyenzo za kuufanya umasikini kuwa suala la kihistoria?
Kwa mfano, Tanzania wakati ikiwa na mikakati na miradi mingi tu ya kupambana na umaskini kama tulivyotangulia kutaja, katika hali ya kushangaza imezunguukwa na Bahari ya Hindi yenye shehena kubwa mali bahari kwa chakula na biashara, ina hazina kubwa ya gesi asilia, pia ina aina nyingi za madini ikiwa na kiasi kikubwa cha dhahabu, kiasi cha kushika nafasi ya tatu barani Afrika katika kutoa maadini ya dhahabu baada ya Ghana na Afrika ya Kusini.

Kuhusiana na ukulima, Tanzania ina ardhi kubwa mno ya kilimo, rasilmali kubwa ya watu, karibu milioni 60, pamoja na vyanzo vikubwa vya maji kama Ziwa Victoria , likiwa miongoni mwa maziwa makubwa ulimwenguni likichukuwa eneo mraba wa 65,583 sq m, ambapo Tanzania pekee ina sehemu ya 49% ya 33,700 square kilometers, sehemu kubwa zaidi ulikilinganisha na majirani zake (Uganda na Kenya). Bila ya kusahau Ziwa Tanganyika, ziwa la pili kuchukuwa ujazo mkubwa duniani na kuwa na kina kikubwa katika Afrika, likiwa na ujazo mkubwa zaidi wa maji mwanana na baridi.

Ukweli mweupe na usio na shaka kwa kila mtu, ni kuwa chanzo cha umaskini wa Tanzania , Afrika na nchi zinazoendelea kwa jumla ni kutokana na kukosa uhuru wa kujiamulia mambo yao na kukosa dira thabiti, na hili ni kutokana na kukosa nguzo ya kimfumo ya kuwaongoza ipasavyo katika mambo yao. Kuiga kwao kibubusa mfumo wa kibepari wa kimagharibi hakukuwapeleka popote, zaidi ya kuwadumaza na kuyasalimisha kikamilifu mataifa yao kwa mataifa maroho ya kibepari ya kimagharibi, China, makampuni ya kibepari ya kimataifa, na taasisi za kifedha za mrengo wa kibepari na kinyonyaji kama Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la kilimwengu nk. Matokeo yake, rasilmali zote za nchi zinazoendelea zinanyonywa na mabepari wa kimagharibi kupitia wanasiasa mafisadi, ambapo wananchi wa kawaida wanaendelea kuhangaika kwa umasikini usiokwisha.

Kwa hivyo, kauli ya Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake Tanzania kuhusu kupambana na umaskini, sio chochote sio lolote zaidi ya dharau na dhihaka kwa serikali na kwa watu wa Tanzania, kwa kuwa anatambua fika kwamba chanzo kikubwa cha umaskini katika nchi zinazoendelea ni ubepari.

Tanzania na nchi zote zinazoendelea kamwe haziwezi kutokomeza umaskini chini ya miradi ya mfumo wa kibepari ambayo husimamiwa kwa sera za kibepari na ala zao za kinyonyaji, bali kinachohitajika kwa nchi zote changa ulimwenguni ni ukombozi wa kweli kupitia mabadiliko ya kimfumo, kutoka mfumo wa ubepari kuelekea katika mfumo wa Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah.

[إِنَّ اللهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّى يُغَيِّرُوا مَا بِأَنْفُسِهِمْ]
“Hakika Allah habadili yaliyoko kwa watu, mpaka wabadilishe wao yaliyomo nafsini mwao.”
[Surat Ar-Ra’d: 11]

Imeandikwa na Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

#ConquestofIstanbul

Maoni hayajaruhusiwa.