Kufutwa Mashtaka ya Uamsho : Fedheha na Uwongo wa Mashtaka Dhidi ya Ugaidi

بسم الله الرحمن الرحيم

Mashtaka ya tuhuma za ugaidi kwa Uamsho na wengine kwa jumla katika kufichwa uonevu, dhulma na uwongo wake yamezingirwa kwa makusudi ukuta mrefu wa khofu, kisingizio cha kutokamilika ushahidi na vitisho katika kuzifuatilia kesi zake, kiasi kwamba mpaka sasa katika baadhi ya magereza kama la Lilunga, Mtwara ni hatia mahabusu kutembelewa na ndugu, kuwapelekea huduma ya chakula mahabusu nk.
Wako wengi waliotishwa kwa kusaidia familia za watuhumiwa, wapo waliokamatwa, kuteswa na kujumuishwa na watuhumiwa kwa sababu tu ya kufuatilia ndugu na jamaa zao.
Khofu kubwa imesambazwa na kukuzwa, wanatishwa watu wa kawaida, wanaharakati, mawakili, vyombo vya habari hadi kuzuiliwa kuripoti rasmi.
Baadhi ya masheikh, maustadh na taasisi za Kiislamu ambao wana jukumu la kidini kusimama kidete kuliko mwengine yoyote kupinga dhulma hizo kama Waislamu na kama wahanga nao wakagubikwa na khofu ya karne isiyomithilika.
Ulinganizi wa Uislamu umezorota na kudorora kwa usafi wake kwa khofu na vitisho, fikra kadhaa za Kiislamu zikapindwapindwa kuridhisha mrengo wa kupambana na ugaidi, wakati mwengine ukitaja qadhia za mahabusu wa ugaidi iwe misikitini au pengine, maimamu na maamuma wanatetemeka na wengine kukuzuiya kwa khofu wasije kuingizwa katika ugaidi au kuambiwa wanasaidia magaidi. Japo kwamba jambo hilo pia wengine halikuwasaidia na hawakusalimika wakasombwa na kuingizwa katika tuhuma hizo.
Katika Waislamu, ukiachilia kando kundi dogo la Waislamu, masheikh, maustadh na wanaharakati linalosimama imara na thabiti, kundi moja liko kimya cha mfu, kundi jengine mada zao ni kupaka mafuta na kujihamihami (apologists) kwamba sio magaidi, na kundi jingine linakwenda mbali zaidi hata kuwa tayari kuwatosa Waislamu wengine waonekane magaidi, ilimradi lijitakase na kuonekana wao safi na wema.
Katika hali kama hiyo ya Waislamu wakiwemo masheikh, kushikwa na khofu, wale waliopewa jukumu la kukamata, kuuwa, kutesa na kudhulumu kwa mgongo wa kupambana na ugaidi wanapata uhalali na nguvu na kuzidi kiburi cha kuuwa, kutesa, kuteka, kunyakuwa na kufanya wanavyotaka kwa sababu wahanga ambao ni Waislamu wamekubali kuvishwa guo la unyonge na udhaifu, basi waliopewa jukumu hilo wanatenda ya kuyatenda kwa mapana na marefu bila ya kujali wala kubali chochote, hata sheria walizotunga wenyewe ambazo huapa kuzilinda wakaweka pembeni.
Baadhi ya wanasiasa wenye kiburi na chuki za wazi nao wakawa ndio mahakama, waendesha mashtaka na majaji, wakadiriki kuwatia hatiani watuhumiwa wa ugaidi, hawakufanya hayo mahakamani, bali kwenye majukwaa ya kisiasa.
Kwa kufutwa mashtaka ya Uamsho, leo Allah Taala mbele ya macho ya kila mtu Kafedhehi suala la mapambano ya ugaidi na mashtaka yake, Kaondosha guo na giza la uwongo lililotanda, kwa kuleta mwangaza wa ukweli, Katuonesha wazi wazi kuwa mashtaka ya tuhuma za ugaidi kwa kiasi kikubwa yamejengwa juu ya msingi wa uwongo na udanganyifu, tena uwongo wa mchana kweupe, kwa lengo la uonevu, dhulma, chuki nk.
Aidha, imetudhihirikia kumbe vishindo vyote vya kutia watu khofu, mateso, kuteka, kisingizio cha ushahidi usiokamilika kwa miaka ni katika ujanja wa kuficha uwongo wa mapambano na mashtaka yake, uwongo ambao baadhi yetu tunaufahamu na kuunadi mara nyingi, lakini kwa sasa uwongo huo uko hadharani uwanjani unaonekana na kila mtu.
Kwa jambo hili sisi Waislamu hakuna haja ya kunyoosheana vidole juu ya misimamo yetu ya nyuma na kulaumiana, bali kilichopo sasa ni kuangalia mbele, kwa sote kusimama kidete kutetea mahabusu na watuhumiwa wa ugaidi wengine wengi waliobakia kwa mamia kama sio maelfu ili watendewe haki, kwa ama kuachiwa huru, wapatiwe dhamana au kesi zao zisikilizwe mara moja.
Qadhia hii kwa Waislamu na wapenda haki kwa jumla itupe ibra, mazingatio na mafunzo makubwa ya kuendelea kutetea haki, kukataa dhulma na kudumu na msimamo huo kwa kujiamini bila ya kutetereka, kwa kuwa ghilba, uwongo na udanganyifu hata uchukuwe muda mrefu, upambwe vipi mbele ya macho kwa vitisho na ujanja ili kuumiza, kuonea na kukandamiza, kwa kuonesha kwamba ati ni ukweli, mwisho wake huporomoka na hudamirika, tena mporomoko wa hadharani uliojaa aibu, idhilali na fedheha.
Allah Taala anatuonesha namna wachawi wa Firaun walivyoghilibu na kuzuga macho ya hadhira na kujaza khofu watu kwa uchawi wao ili kumshinda Nabii Musa As. ili kumpa uhalali na nguvu Firaun aendelee kutesa na kukandamiza.
فَلَمَّا أَلْقَوْا سَحَرُوا أَعْيُنَ النَّاسِ وَاسْتَرْهَبُوهُمْ وَجَاءُوا بِسِحْرٍ عَظِيمٍ (الأعراف: 116 ).
‘Basi (wachawi) walipotupa (kamba zao) waliyazuga macho ya watu, na wakawatia khofu, na wakaleta uchawi mkubwa mno. (Al-Aaraf:116)
Lakini mwisho wake ilikuwa idhilali na fedheha, kwa kuwa uchawi kama ulivyo uwongo wowote mwengine hauwezi kufanikiwa popote, viwe viwavyo.
فَغُلِبُوا هُنَالِكَ وَانقَلَبُوا صَاغِرِينَ (الأعراف: 119).
‘Kwa hivyo, walishindwa hapo (wachawi) na wakawa ni wenye kudhalilika”
(TMQ Al-Aaraf:119)
إِنَّمَا صَنَعُوا كَيْدُ سَاحِرٍ وَلاَ يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَى (طه:
‘Hakika walichotengeneza ni vitimbwi vya mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote afikapo’ (TMQ Twaha: 69)
Risala ya Wiki No. 102
11 Dhu al-Qi’dah 1442 Hijri / 20 June 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.