Kubadilishwa Qibla na Mafunzo Yake

( Sha’aban 2 AH)

Ndani ya mwezi wa Shaaban kuna matukio mbalimbali yaliyotokea katika tareekh ya Kiislamu. Moja katika matukio makubwa ndani ya mwezi huo ni kubadilishwa qibla kutoka Masjid-ul Aqswa (Sham) kuelekea qibla cha Masjid-ul Haram ndani ya Makka. Waislamu walitumia qibla cha Al-Quds (Biladu Shaam) kwa muda wa miezi 16 au 17 kabla ya kubadilishwa. Tukio hili lilitokea mwezi wa Sha’ban mwaka wa 2 Hjiria. Ndani ya tukio hili kuna mafunzo mengi katika utekelezaji wa dini yetu.

Awali, Allah Taala kutuonesha uwepo wa mgongano wa kimaumbile baina ya haki na batil. Aidha, tunadhihirishiwa ukali wa Allah Taala kwa makafiri hususan makafiri (harbii/wapiga vita) kiasi cha Allah Taala kuwafedhehi Ahlul kitaab wazi wazi kwa kuwaita ‘wapumbavu’ kufuatia msimamo wao wa kiuadui dhidi ya qibla kipya cha Mtume SAAW, Uislamu na kuficha haki kuhusu qibla, wanayoijua kinagaubaga kama watoto wao.

سَيَقُولُ السُّفَهَاءُ مِنْ النَّاسِ مَا وَلاَّهُمْ عَنْ قِبْلَتِهِمْ الَّتِي كَانُوا عَلَيْهَا قُلْ لِلَّهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ
“Wapumbavu miongoni mwa watu watasema: Nini kilichowageuza kutoka qibla chao walichokuwa wakikielekea? Sema Mashariki na Magharibi ya Mwenyezi Mungu ……..” (TMQ 2: 142)

الَّذِينَ آتَيْنَاهُمْ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ وَإِنَّ فَرِيقًا مِنْهُمْ لَيَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ
“Wale tuliowapa Kitabu wanayajua haya kama wanavyowajua watoto wao, na kundi miongoni mwao huificha haki na hali wanaijua “ (TMQ 2: 146)

Pili, tunajifunza subra ya Mtume SAAW, licha ya kuwa alikuwa na hamu na shauku kubwa ya kubadilishiwa qibla kutoka Sham kuja mji mtukufu wa Makka, lakini alichokifanya Mtume SAAW ni kusubiria maamuzi ya Allah Taala, Mleta sheria afanye maamuzi yake. Kwa kwa kuwa Yeye pekee, Allah Taala ndie mwenye haki ya kuleta sharia, ziwe sharia za ibadaat, siasa, uchumi, jamii nk.

Katika Hadithi ya Bukhari iliyopokewa kutoka kwa Barra amesema:

«لَمَّا قَدِمَ رَسُولُ اللهِ r الْمَدِينَـةَ صَلَّى نَحْوَ بَيْتِ الْمَقْدِسِ سِتَّةَ عَشَرَ أَوْ سَبْعَةَ عَشَرَ شَهْرًا وَكَانَ يُحِبُّ أَنْ يُوَجَّهَ إِلَى الْكَعْبَةِ فَأَنْزَلَ اللهُ تَعَالَى قَدْ نَرَى تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْـلَةً تَرْضَاهَا فَوُجِّهَ نَحْوَ الْكَعْبَةِ
“Alipokuja Mtume (SAAW) Madina aliswali kuelekea Baitul-Maqdis kwa miezi kumi na sita au kumi na saba, na alikuwa anapenda aelekee kibla cha Al-Kaabah, basi Allah Ta’ala akateremsha aya isemayo :

قَدْ نَرَى تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْـلَةً تَرْضَاهَا
‘’Kwa yakini tumekuona unavyogeuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza wewe kwenye qibla ukipendacho’’ (TMQ 2 : 144)
Na akamuelekeza upande wa Ka’abah…….” (Bukhari)

Tatu, tukio hili linatufunza namna Mtume SAAW na Waislamu waliotangulia walivyozipokea hukmu za kisheria kwa moyo mkunjufu, ikhlasi na unyenyekevu. Na hukmu hizo walizibeba na kuzitekeleza ipasavyo. Tena utekelezaji wa moja kwa moja kimsingi/radical bila ya kusubiri, kusitasita au kuzitekeleza kwa hatua kidogo kidogo yaani kufanya tadarujj.

Kuna wanaodai kwa ufahamu wa kimakosa kwa kufungamanisha uteremshwaji wa hukmu na utekelezaji, na kudai jambo hilo linatupa uhalali wa kutekeleza hukmu za kisharia hatua baada ya hatua ili kwenda sambamba na namna zilivyoteremshwa kidogo kidogo.

Katika suala hili kuna mambo mawili yenye sura mbili tofauti: Kwanza, uteremshwaji wa hukmu. Pili, utekelezaji wake. Suala la uteremshwaji wa hukmu lina uhusiano na Muumba na Mleta sharia peke yake na kamwe haingiliwi katika elimu yake. Na suala la utekelezaji lina uhusiano na wanadamu na tutaulizwa na Muumba juu ya utekelezaji huo.

Suala la uteremshwaji wa sheria, kama vile muda, munasaba, namna Allah Taala alivyoziteremsha nk. kamwe halihusiani na wanadamu wala halipaswi kuwa hujja au dalili kwa namna yoyote kulifungamanisha na namna ya utekezaji. Hii ina maana kuwa, mara hukmu ikishushwa na Allah Taala kwetu, huwa ni wajibu kuitekeleza kimsingi/radical bila ya kutoa kisingizio kwamba twaweza kuitekeleza kidogo kidogo. Suala la uteremshaji ni kando na utekelezaji, na hilo ni elimu ya Mteremshaji na sio zaidi.

Pamoja na mifano mingi ya jambo hilo namna masahaba walivyozitekeleza hukmu kimsingi mara zilivyoteremshwa. Tukio hili la qibla ni mfano hai na wa wazi zaidi.
Mtume SAAW alibadilisha qibla akiwa ndani ya swala, hata hakusubiri kumaliza swala hiyo, baada ya Allah Taala kumtaka abadilishe. Ndio maana hadi leo kuna Msikiti unaoitwa Masjid Qiblatain huko Madina, kwa kuwa Mtume SAAW aliwaswalisha Waislamu swala moja kwa kutumia vibla viwili.

Nne, katika tukio hili kuna mazingatio ya kuzifikisha hukmu za kisharia kwa wengine bila ya kutafuna maneno. Tunaona wale walioswalishwa na Mtume SAAW katika swala kilipobadiliswa kibla ndani yake, waliporudi tu katika maeneo yao kando kidogo na kuwakuta baadhi ya Waislamu bado wanaswali, haraka nao waliwaeleza Waislamu hao wakiwa bado ndani ya swala kuwataka wabadilishe qibla mara moja. Hayo ni kwa sababu masahaba walielewa fika uwajibu wa jukumu la kuifikisha hukmu hiyo kwa wengine ili itekelezwe kivitendo, kwa kuwa haikuletwa kuwa ni nadharia.
Imesimuliwa katika Hadithi ya Barr Ra. katika Sahih Bukhar aliposema:

وَصَلَّى مَعَهُ رَجُلٌ الْعَصْرَ ثُمَّ خَرَجَ فَمَرَّ عَلَى قَوْمٍ مِـنْ الأَنصـارِ فَقَـالَ هُوَ يَشْهَدُ أَنَّهُ صَلَّى مَعَ النَّبِيِّ
فَانْحَرَفُوا وَهُمْ رُكُوعٌ فِي صَلاةِ الْعَصْرِ»
“(Siku kilipobadilishwa kibla)……Na aliswali asri (Mtume SAAW) pamoja na watu, kisha akatoka mtu na akapitia watu wa Ansar na akasema, kwamba yeye anashuhudia kuwa aliswali pamoja na Mtume (SAAW) na kuwa ameelekea al-kaaba. Basi waliokuwa wakiswali wakageuka wakiwa katika rukuu katika swala ya asri”.

Kwa kumalizia, katika hali yetu ya leo ambapo tayari hukmu zote zimeshateremshwa huwa ni wajibu Waislamu kuzitekeleza zote. Amma zile zinazohusiana na nguvu ya kidola, ni wajibu dola ya Kiislamu ya Khilafah kuzitekeleza mara moja inaposimamishwa dola hiyo InshaAllah. Na kimsingi hili ni sharti la msingi kwa dola ya Khilafah, yaani kutekeleza hukmu zote bila ya kuacha hata moja.

Aidha, hii pia ni dalili kuwa madola kama Saudia, Iran, Sudan na mfano wake si madola ya Kiislamu. Kwa kuwa si tu yanaendelea kuwadhuru Waislamu wazi wazi, bali pia hayatekelezi hukmu zote za Kiislamu ipasavyo. Hivyo, ni wajibu kwa Ummah wa Kiislamu kufanya kazi usiku na mchana kumtawalisha mtawala atakayetawala kwa sharia zote kwa ujumla wake. Kwa kuwa hivyo ndivyo unavyowajibisha Uislamu.

Masoud Msellem
03 Sha’aban 1440 Hijri / 09/04/2019

Maoni hayajaruhusiwa.