Kuangushwa Khilafah: Kuporomoka Elimu

Tukiwa mwishoni mwa mwezi wa Rajab, mwezi ilipoangamizwa kwa uadui dola ya mwisho ya Kiislamu ya Khilafah Uthmania, na kuuwacha Ummah wa Kiislamu na wanadamu kwa jumla katika misiba, mashaka na kiza kisichokuwa na mfano.

Miongoni mwa msiba kwa kuangushwa Khilafah ni katika upande wa kielimu. Vibaraka waliokabidhiwa kusimamia Waislamu baada ya ardhi za Waislamu kumegwa vipande vipande walipatiwa sera ya kikoloni ya kielimu isiyomuandaa mwanafunzi kuwa huru kifikra wala kumjengea ubunifu.

Sera hiyo inawafanya Muislamu na wanadamu kwa jumla kubakia kuwa watumwa, kuipupia dunia, kuitupa akhera na wasomi kujiona ni watu wa tabaka maalumu. Ni elimu ya kuwaandaa Waislamu na wanadamu kuwa watumishi na watetezi bila ya hoja mfumo wa kibepari.

Ni elimu isiyokuwa na meno ya kuwafanya wanafunzi kuwa wavumbuzi, kwa kuwa kiasili nchi zao haziko huru, ambayo ndio nyenzo ya kimsingi katika hilo. Matokeo yake wanafunzi hukaririshwa namna wengine walivyofikiri na sio kufanywa wao wafikiri.

Wakoloni katika masomo ya kithaqafa (arts) wanawahifadhisha wanafunzi shehena ya nadharia za wanafikra wao. Matokeo yake wanaoitwa wasomi wa masomo ya kithaqafa (arts) hawana zaidi ya kukariri kama kasuku nadharia za kimagharibi, na wanaosoma sayansi hubakia kusoma historia ya wavumbuzi badala ya wao kuvumbua.

Pamoja na ubovu wa elimu hiyo pia ikageuzwa kuwa biashara ya gharama kubwa. Ripoti ya 2014 ya Shirika la UNESCO imebainisha kuwa zaidi ya watu milioni 50 katika ulimwengu wa Kiislamu hawajui kusoma na kuandika.

Aidha, robo ya watu wote katika nchi zinazoendelea hawajui kusoma na kundika! Licha ya utajiri na rasilmali zilizomo ndani ya nchi za Kiislamu raia wametumbukizwa utumwani na kudhulumiwa waziwazi kwa kukosa elimu. Hiyo ni hasara kwa Waislamu na wanadamu kwa kuwa elimu leo ni biashara asiyoweza kumudu kamwe mtu mnyonge.

Dola ya Kiislamu ya Khilafah zama zote ilijifunga na mwenendo wa Mtume SAAW kwa kuipa elimu kipaumbele kwa kuwa ni uti wa mgongo, uhai na nyenzo muhimu kuilinda aqeedah ya Uislamu. Kama Mtume SAAW alivyowatuma maswahaba wawili kwenda kuchukua teknolojia ya utengezaji wa silaha kwa bingwa Jurash wa Yemen, Pia ni Khalifah Umar ibn khatwab ndiye aliyeanzisha teknolojia ya kutengeneza manowari. Aidha, makhalifa waliokuja waliwekeza katika elimu kiasi cha ulimwengu wa Kiislamu kumiliki miongoni mwa vyuo vikuu vya mwanzo vyenye hadhi kama Baitul-Hikma ndani ya Iraq na chuo kikuu cha Al-Qarawiyyin ambacho miongoni mwa wanafunzi wake ni Papa Sylvester II wa Kanisa Katoliki. Hali hii iliifanya Khilafah kuwa dola kuu sio tu kifikra na kijeshi bali katika nyanja zote za kielimu kwa zaidi ya karne kumi. Zama ambazo 95% ya watu wa Ulaya hawakujua kusoma wala kuandika! Leo mambo yamegeuka juu chini. Msiba na dhulma unaopaswa kufutiliwa mbali.

Enyi Waislamu na wanadamu,
Kama zilivyofanya Khilafah zilizotangulia katika elimu ndio itakavyofanya dola ya Khilafah itakaporudi na kuzidi mafanikio yaliyopita InshaAllah. Itazitumia rasilmali na utajiri mkubwa uliopo kufikia lengo hilo. Itawekeza katika kuifinyanga haiba ya mwanafunzi na kuzalisha wabunifu na fani mbali mbali ili kuhamasisha uvumbuzi. Utaijenga elimu juu ya utulivu wa nafsi na kuepuka shehena ya nadharia ambazo hazina uhalisia wowote. Kubwa elimu itasimamiwa na dola huru isiyoingiliwa katika mambo yake wala kupangiwa sera na madola ya kikoloni.

Risala ya Wiki No. 34
26 Rajab 1440 Hijri / 02 Aprili 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

#RajabuFarajaKwaWalimwengu

Maoni hayajaruhusiwa.