Kuanguka Khilafah Chanzo Cha Kuporomoka Elimu

Tukiwa ndani ya mwezi wa Rajab, mmoja katika ya miezi minne mitukufu kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu. Ukiachia utukufu wa mwezi huu pia kuna matukio mengi ya kitarekhe yaliyojiri ndani yake. Miongoni mwa hayo ni: tukio la Israa na Miiraj, kukombolewa kwa Al-Quds chini ya Jemedari mahiri na shujaa Salahuddin Al-Ayyubi, kufariki kwa Abi Taalib, Ami yake Mtume SAAW nk.

Pamoja na matukio hayo pia kuna tukio ambalo limeacha msiba mkubwa kwa Ummah wetu wa Kiislamu na wanadamu kwa jumla hadi leo, nalo ni tukio la kuangushwa kwa serikali ya Kiislamu/Khilafah (mwezi 28 Rajab 1342 Hijri ).
Tukio hilo limeacha athari kubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu katika fani mbalimbali . Hivi sasa ubepari ndio mfumo pekee wenye kuitawala dunia katika mikakati yake ya kujitanua, kujilinda na kujihifadhi unatumia mbinu ya ukoloni mambo leo katika kila sekta kama siasa, uchumi pia elimu ili kufikisha malengo yake nchi changa na bara la Afrika ndiyo muathirika mkubwa.
Sekta ya elimu nayo imelengwa na wakoloni ili kuhakikisha inakuwa duni na ya kuwatumikia wakoloni na fikra zao. Wawe wahitimu wa elimu ya kisekula na hata wa madrassa wametengenezwa kubeba mtazamo wa maisha wa kimagharibi, na wala hawana athari yoyote kwa Umma na mazingira wanayoishi.
Katika elimu kuna changamoto kadhaa kama uhaba wa skuli, vitendea kazi pia walimu nao hubezwa zaidi na watawala ambao ni vibaraka wa nchi za magharibi kwa kuwalipa vipato duni sana. Bahati mbaya hata zile nchi zinazoitwa ati ‘zimeendelea’ walimu wapo katika hali mbaya ya kudharauliwa na kunyanyaswa hasa na wanafunzi ambao wamepewa mamlaka chini ya kinachoitwa ‘Haki za kibinaadamu’.

Yanayojiri katika taasisi za kielimu, iwe skuli au vyuo hayasemeki katika upande wa kimaadili! Skuli zinakabiliwa na tatizo la mimba za zinaa, ukosefu wa maadili, mahusiano ya kimapenzi ndani ya umri mdogo nk.
Na kwa upande wa vyuo vya elimu ya juu hali ni mbaya zaidi kiasi cha baadhi ya wanafunzi kushiriki katika vitendo vya ukahaba wa kujiuza miili yao nk. (rejea makala: Reported risky sexual practices amongst female undergraduate students – African journal of primary health care).
Tatizo la ‘elimu gamba’, yaani wanafunzi kufanya chochote ili kupata shahada pia nalo limekuwa likiiandama sekta ya elimu kila mahala. Leo kumesheheni wataalamu wa vyuo vikuu wakiwa chini ya viwango na hawana uwezo wa kitaalamu wa kuvumbua mambo mapya.

Enyi Walimu, Wasomi, Wanafunzi na Wadau wote wa elimu :
Ulimwengu ikiwemo Afrika unahitaji mfumo wa Uislamu chini ya serikali yake/Khilafah Rashidah kuja kuleta ukombozi wa kweli katika elimu na sekta nyengine zote ambazo leo zimeoza chini ya mfumo wa kibepari na nidhamu yake batil ya kidemokrasia.
Tuna wajibu wa kila mmoja wetu kuitumia fursa na elimu aliyonayo katika kuuendeleza na kusogeza mbele gurudumu la kurudisha tena maisha ya Kiislamu, jambo litakalowezekana tu chini ya serikali ya Kiislamu ya Khilafah ambayo haina budi kuanzishwa katika nchi kubwa ya Waislamu na kuenea dunia nzima.
Basi tuuchukulieni mwezi huu wa Rajab kuwa ni faraja kwa ulimwengu kwa kujizatiti zaidi katika wajibu huo wa kurejesha Khilafah huku tukiwa na uhakika wa ushindi, kama Mtume SAAW aliposema :
“…kisha itarudi Khilafah kwa manhaj ya Utume”  (Ahmad).
Kwa dola hiyo tutapata izza/nguvu kama walivyopata waliotangulia katika imani na kufuzu duniani na akhera.
Iliandikwa na ZAMSA (Imehaririwa)
#RajabFarajaKwaWalimwengu

Maoni hayajaruhusiwa.