‘Krismasi’ Hoja ya Kuwalingania Wakristo Katika Uislamu
بسم الله الرحمن الرحيم
Krismasi iko mlangoni, sikukuu iliyoibuka muda mrefu baada ya Nabii Issa As. Sikukuu hii iliasisiwa karne ya 313 AD. na Mtawala Constantine wa Roma alipoukubali ukiristo. Akaunda sikukuu ya krismasi kwa mchanganyiko wa sherehe za kipagani za waroma kutoka sikukuu yao ya Saturnalia pamoja na ibada ya mafursi kwa mungu wao Mithra. www.history of christmass.net. Kwa hakika hakuna uhakika wowote wa tarehe 25 disemba kuwa ndio siku aliyozaliwa Issa As. Na ndio maana Kanisa la Mashariki (Eastern Church) wao husheherekea Krismasi Januari 6 ya kila mwaka badala ya tarehe 25 disemba.
Kwa Waislamu ni haramu moja kwa moja kusherehekea sikukuu ya krismasi kwa namna yoyote. Iwe ama kumpa mkiristo kadi ya krismasi (christmass card), mkono wa pongezi, kumtakia sikukuu njema (‘merry christ mass’), kuipamba nyumba, gari au mahala pa kazi kwa alama za krismasi (sha’air) kama vile kuweka mti wa krismasi (Christmass tree) kuigiza kwa kuvaa au kuwavalisha watoto mavazi ya Father Christmass nk.
Ni muhimu tukumbuke kwamba kumpa zawadi kafiri au kupokea kutoka kwake zawadi halali kiasili ni kitu cha halali, lakini kwa munasaba na dini jambo hilo huwa ni haramu. Kwa sababu, zawadi hiyo umepewa kwa mkabala wa sikukuu ya kikafiri. Japo kwamba zawadi hii ni kitu cha ‘mada’ (kushikika) lakini kina mahusiano na fungamano la moja kwa moja katika upande wa kiimani na ‘hadhara’. Na maana ya ‘hadhara’ ni kule kupatikana fungamano fulani la kifikra au la kiitikadi. Kwa hivyo, hata kama zawadi utakayotoa au kupokea kutoka kwa mkiristo asili ni ya kitu cha ‘mada’ na halali, lakini kwa kuwa imefungamana na sherehe ya itikadi ya kikafiri huwa haramu.
Ubepari/udemokrasia ambao ni mfumo wa kikafiri na mfumo wa kimaslahi umeipigia debe mno na kuitumia vyema kimaslahi Krismasi:
Kwanza, kuiunga mkono kikamilifu na kuonesha kwamba mfumo wao hauna ugomvi na dini. Lakini kiudhati hauna mgongano na dini za kiroho ambazo hazina nidhamu za masuluhisho kama ukiristo, ubudha, uhindu nk.
Pili, kuwalaza na kuwapoza raia wao wapunguze joto la mfumo unaowabana, kwa raia hao kujinyenyekeza ‘kiurongo’ kwa ibada katika baadhi ya wakati ukiwemo wakati wa Krismasi.
Tatu, ubepari unaidandia Krismasi kwa malengo na maslahi ya kibiashara na masoko ya bidhaa zao. Kwa kuuza kwa gharama ya juu bidhaa mbalimbali kwa jina la ‘siku tukufu’ ya Krismasi. Na kwa kuwa ubepari umepandikiza fikra ya hatari ya ‘pupa na uroho’ wa kila kitu (consumerism) kwa raia wengi hususan wa nchi za Magharibi hufanikiwa kukusanya mabilioni katika kipindi hiki. Kiasi cha raia wa nchi hizo na nchi zetu changa kujitumbukiza katika madeni yasiyomithilika na yanayochukuwa muda mrefu kuyalipa kwa ajili ya kununua zawadi za Krismasi, mapambo yake, zawadi nk. Kwa mfano katika Krismasi ya mwaka wa jana (2019) kwa mujibu wa mtandao wa World Economic Forum, nchini Marekani walitumia zaidi ya dolari trillioni moja kwa ajili ya Krismas.
Nne, mfumo wa kidemokrasia huitumia Krismasi na sherehe nyengine za kidini za kikafiri kama ‘Pasaka’ kama mbinu ya kuleta ‘ukuruba wa kidini baina ya Uislamu na Ukiristo’, pamoja na jamii za wafuasi wa dini mbili hizi, kwa kusisitiza kauli za ‘kuishi pamoja’, ‘maelewano’ na ‘mashirikiano ya kidugu’ kwa kudai ati dini zote zinatoka kwa Mungu, na zaidi hudai dini zote hizi mbili zinatokana na chimbuko la Ibrahim As.
Fikra hii ni fikra ya kikafiri, hatari na haramu na kimsingi inawadhuru Waislamu kwa kuwa dini yao ndio ya haqi. Tunasema hakuna ukuruba baina ya haqi na batil, wala baina ya Uislamu na ukafiri kwa namna yoyote. Na Waislamu ni wajibu kujiepusha mbali na fikra na mtazamo huu na kuupiga vita kwa nguvu zote za kifikra. Ukuruba uliopo baina ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu ni katika mambo yasiyo ya kidini, kama miamala ya kibiashara, mikataba nk. Lakini sio katika suala la kiimani. Kwa kuwa kila dini ina misingi na Imani yake.
Ni muhimu kwetu Waislamu badala ya kubeba fikra za dini mseto au ukuruba wa kidini kwa kuwa ni Umma bora wenye mfumo wa haqi unaokubaliana na maumbile na wa kilimwengu tunapaswa kuijadili Krismasi kwa kuchemsha mjadala wa kistaarabu na hekma kwa ukiristo na wakiristo kwa kuwalingania na kuwavuta kuja katika Uislamu kwa kutumia hoja za kiakili. Tunasema kwa hoja za kiakili, kwa kuwa wao wakiristo hawakikubali kitabu chetu kitukufu cha Quran. Na sisi Waislamu hatukikubali kitabu chao cha biblia. Japo kwamba kuna baadhi ya Waislamu waliochanganyikiwa huipachika jina biblia kwamba ni kitabu cha ‘Injili’ na Waislamu wana wajibu wa kukisoma. Lakini kwa hakika hatuna wajibu wa kuisoma biblia na wala biblia sio Injili, kwa kuwa sifa msingi ya kitabu cha Mungu hupaswa kubakia katika uhalisia wake kama kilivyoteremshwa. Lakini tunakiri na kuamini kwamba kilikuweko kitabu cha injil alicholetewa Nabii Issa As.
Mtume SAAW kamwe hakuiwacha fursa ya kuwalingania wakiristo kadiri ilivyowezekana hata katika mazingira magumu, kama alivyomlingania Addas, mtumishi wa kikiristo katika shamba la mizabibu la Rabia, alipokuwa Mtume SAAW akirejea Makka kutoka Taif akiwa na majeraha baada ya kupigwa mawe. Aidha, alizidisha kuwalingania makafiri wa kikristo baada ya kusimamisha dola ya Kiislamu ndani ya Madina, kama alivyosimamisha hoja nzito dhidi ya ujumbe mkubwa wa wakiristo 60 wa Najran uliokuja Madina mwaka wa 9 Hijria chini ya kiongozi wao Abu-Masih. Na wakiristo hao walipojikanganya na kuzikataa hoja zake, Allah Ta’ala akamtaka Mtume SAAW afanye maapizano nao kwa kiapo maalum (mubahala) cha kuomba laana kwa muongo. Quran Tukufu inatukumbusha:
فَمَنْ حَاجَّكَ فِيهِ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنْ الْعِلْمِ فَقُلْ تَعَالَوْا نَدْعُ أَبْنَاءَنَا وَأَبْنَاءَكُمْ وَنِسَاءَنَا وَنِسَاءَكُمْ وَأَنْفُسَنَا وَأَنْفُسَكُمْ ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَلْ لَعْنَةَ اللَّهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ (آل عمران: 61).
“Watakaokuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii waambie: Njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zenu na wake zetu, na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mungu iwashukie waongo.” (Tmq 3:61)
Jambo hilo pia wakiristo wa Najran walilikataa. Kiongozi wao akawaeleza wenzake:
“Enyi manasara! Mimi naona nyuso ambazo, lau zitaomba jabali liondoke lilipo basi linaweza kuondoka. Kwa hivyo msiapizane nao msije mkaangamia”.
Kisha wakiristo hao wakamueleza Mtume SAAW kwa kusema:
‘Ewe Abul-Qasim tumeonelea tusiapizane na wewe’. Mtume akawambia: ‘Basi silimuni’ wakakataa kusilimu kisha wakakubali kulipa jizya.
Leo hii hususan kuelekea katika Krismas tuna fursa mwanana kuwaonesha wakiristo juu ya udhaifu wa fungamano lao duni kwa Muumba. Kwa kuwa unyenyekevu wao hudhihirika siku ya Krismasi, Jumapili au baadhi yao Jumamosi, tena katika baadhi ya ibada chache za kiroho. Na kipindi chote kilichobakia katika maisha yao hawana suluhisho lolote kutoka katika dini yao linalotatua matatizo yanayomkabili mwanaadamu kila siku. Amma yawe ya matatizo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na mengineyo.
Aidha, kuwaonesha wakiristo kwa hoja kwamba Issa as. hakuwa Mungu, kwa kuwa Mungu hazaliwi, na yeye alizaliwa na mwanaadamu. Kwa kuwa kinachozaliwa ni kiumbe, na kiumbe hakina budi kufa, na Mungu kwa kuwa ni Muumba kamwe hafi na akifa huwa si Mungu.
مَا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلاَّ رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ كَانَا يَأْكُلاَنِ الطَّعَامَ انظُرْ كَيْفَ نُبَيِّنُ لَهُمْ الآياتِ ثُمَّ انظُرْ أَنَّى يُؤْفَكُونَ (المائدة:
“Hakuwa Masihi mwana wa Mariamu ila ni Mtume. (na sio Mungu) Wamekwishapita Mitume (wengi) kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. (mchamungu na sio Mungu). Wote wawili walikuwa wakila chakula (kwa kuwa ni wanaadamu). Angalia tunavyowabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyogeuzwa.’
(TMQ 5:75)
Masoud Msellem
23 Disemba 2020
Maoni hayajaruhusiwa.