Kisa Cha Mkufu Wa Thamani Kilichojaa Mafunzo ya Thamani

Wakati tukiwa ndani ya mwezi huu wa Dhul Hijja, mwezi ulionza muhula wa utawala wa Khilafah ya Imam Ali bin Abi Talib ra. Khalifa wa nne, mchaMungu, alim mkubwa, jasiri na muadilifu asiye na mfano, ni muhimu tujikumbushe baadhi ya mafunzo adhimu aliyotuachia.

Siku moja Ibn Abi Rafi, mtunza hazina za Baitul Maal ya Waislamu katika zama za Khilafah ya Imam Ali bin Abi Talib ra. alipokea mkufu na vito vya thamani na mali nyengine kutoka Basra kwa ajili ya kuzihifadhi katika Baitul maal.
Binti wa Imamu Ali ra. akamtumia Ibn Abi Rafi ujumbe wa kuomba kuazima mkufu ule ili auvae katika sikukuu ya Eid kubwa. Bwana Ibn Abi Rafi akakubali ombi hilo kwa sharti kwamba mkufu huo utunzwe, usipotee, wala kuharibika na urejeshwe ndani ya siku ya tatu.

Imam Ali ra. alitokea kuuona na kuutambua mkufu huo na kupata maelezo jinsi binti yake alivyoupata. Imam Ali ra. akamkabili mtunza hazina Abi Rafi akamuuliza.
‘Jee unadhani ni halali kwako kuvunja dhamana ya Waislamu’?
Abi Rafi akajibu: ‘Allah Aniepushe na uovu huo’.
Imam Ali akasema: ‘Kwa nini hukupata idhini yangu wala idhini ya Waislamu kumuazima binti yangu mkufu kutoka Baitul Maal? Abi Rafi akajibu: ‘Ewe Imamu wa Waumini huyo ni binti yako, aliazima ili kujipamba na kisha aurejeshe”. Imamu Ali ra. alimkaripia sana Abi Rafi na kumueleza: ‘Rejesha huo mkufu leo hii na ukifanya kosa hili siku nyengine nitakuadhibu’.

Binti wa Imam Ali ra. alipopata taarifa zile akamkabili baba yake na kumueleza. ‘Ewe baba yangu mimi ni binti yako kipenzi, ni nani mwengine anastahiki mkufu huo zaidi yangu’? Imamu akajibu: ‘Ewe mtoto wa Abu Talib usiache njia ya haki. Unaweza kunieleza ni wanawake wangapi wa Answari na Muhajiruun wanaojipamba kwa mikufu kama hiyo’?
Hiyo ndio hali ya makhalifa namna walivyofika daraja ya juu ya uadilifu wao katika zama za dhahabu chini ya dola ya Kiislamu ya Khilafah. Uadilifu ambao leo ni adimu kiasi kwamba hata katika masimulizi, baadhi huona visa kama hivi kama ni visa vya ngano.

Ulimwengu una kiu kubwa kuupata uadilifu kama huu, na hautorudi kamwe ila kwa kurejesha tena dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa manhaj ya Utume (Khilafah ala minhaj Nubuwat).
Chini ya dola ya Khilafah kinyume na nidhamu ya kidemokrasia, ambapo watawala huanza kwa kujitajirisha wao binafsi, familia zao, marafiki, wapambe wao kisha kujiwekea kinga ya kisheria wasishitakiwe mahkamani, huvuruga na kuponda mali za Umma kwa ubadhirifu bila ya kujali kwamba ni mali za Umma ambao unahangaika kwa dhiki na mashaka.

Aidha, kisa hiki kuna funzo kubwa, kuwa Uislamu katika zama zote ulikuwa na utawala wake na idara mbalimbali za usimamizi wa mambo yake ikiwemo usimamizi rasmi wa mali zake. Na hii ni hoja tosha kwamba Uislamu ni mfumo kamili wa maisha, na kamwe mambo yake chini ya dola hayakuwa yakienda shaghala baghala.

Pia kisa hiki kInadhihirisha waziwazi namna Uislamu unavyokubaliana na maumbile ya mwanaadamu. Na kattu Uislamu haumfungi mwanaadamu katika jela ya dhiki na mashaka ya kupingana na maumbile yake.
Ndio maana ukatoa ruhusu na kupendekeza sana wanawake kujipamba kwa mapambo mbali mbali ili wazidi kuvutia kwa waume zao, na kuwa hilo suala la kujipamba ni sehemu ya maumbile yao. Lakini ukaliweka jambo hilo kwa mipaka maalum na maeneo maalum ya kisheria ili kuuhifadhi mujtamaa/jamii usiangamie.

Kwa msingi huu, wanaume wenye uwezo wawagharamie kwa kadri ya uwezo wao wake na mabinti zao kwa aina tofauti za mapambo na vitu vya thamani. Na kwa upande mwengine, mama na dada zetu nao wasiwatenze nguvu waume zao kwa kuwatia shemere kwa yalio nje ya uwezo wao.

لِيُنفِقْ ذُو سَعَةٍ مِنْ سَعَتِهِ وَمَنْ قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ فَلْيُنفِقْ مِمَّا آتَاهُ اللَّهُ لاَ يُكَلِّفُ اللَّهُ نَفْسًا إِلاَّ مَا آتَاهَا سَيَجْعَلُ اللَّهُ بَعْدَ عُسْرٍ يُسْرًا

“Atoe mwenye wasaa kwa kadiri ya wasaa wake, na mwenye dhiki atumie katika kile alichompa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa kadiri ya alichompa. Karibuni hivi , Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraja”

(TMQ 65:7)

#UislamNiHadharaMbadala

Maoni hayajaruhusiwa.