Innallilahi Wainna Ilayhi Rajiuun

Sheikh Hussein Hassan (Nyundo) ametangulia, nasi tunafuatia.

Tumepokea kwa majonzi na huzuni kubwa taarifa za msiba wa kutangulia mbele ya haki Sheikh maarufu Hussein Hassan (Sheikh Nyundo).

Kifo kilimkuta usiku wa kuamkia leo huko Zanzibar na maziko InshaAllah yatafanyika leo Jumatatu 16 Machi (saa saba – adhuhuri, maiti itaswaliwa na kuondokea Msikiti wa Mohammed Ali, Kidongo Chekundu na kuzikwa Muyuni, mkoa wa Kusini Zanzibar.

Sheikh Hussein Hassan (Sheikh Nyundo) ametoa mchango usio na mithali katika Uislamu hususan katika upande wa kutoa nasaha za Kiislamu katika masuala ya ndoa na mahusiano ya kijamii kwa jumla. Jambo hilo linadhihirika wazi kutokana na mihadhara yake mingi huku nakala za sauti na video za nasaha zake kuenea kwa kiwango kikubwa sio tu katika Afrika ya Mashariki bali na sehemu nyengine.

Aidha, Sheikh Hussein atakumbukwa kwa kuwa na mlahaka mwema, mafungamano na mahusiano mema na masheikh, maustadh na walinganizi wa Uislamu wakiwemo wanaharakati wa Hizb ut Tahrir Tanzania ambapo ndani ya kati yamwaka 2016 Miladia/ Dhulhijah, 1437 Hijiria alikutana rasmi na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Hizb Ut-Tahrir Tanzania- Sheikh Musa Kileo kwa mazungumzo maalum ikiwemo kukumbushana juu ya qadhia nyeti ya ulinganizi wa kurejesha maisha ya Kiislamu kupitia kurejesha tena Serikali ya Kiislam (Khilafah) Ulimwenguni kuanzia katika nchi kubwa za Waislamu.

Kufuatia msiba huu mkubwa mkubwa, kwa niaba ya Hizb ut Tahrir Tanzania natoa mkono wa taazia kwa familia ya Sheikh Hussein, Waislamu wote, masheikh, maustadh, ndugu jamaa na marafiki.

Tunamuomba Allah SW awamakinishe wafiwa wote kwa subra, istiqama katika kipindi hiki kigumu na kuwalipa ujira mkubwa.

Pia, tunamuomba Allah Taala kwa unyenyekevu mkubwa Amsamehe, Amrehemu Sheikh Hussein, Amjazie penye mapungufu na kumuingiza katika Jannat ul- Firdaus, kwa rehma zake zilizokienea kila kitu.

Amiin

16 Machi 2020

Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari Hizb ut Tahrir Tanzania

(Pichani marehemu (mwenye koti) akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Hizb Ut-Tahrir Tanzania- Sheikh Musa Kileo walipokutana Masjid Rahma, Buguruni kwa Madenge, Dar es Salaam)

Maoni hayajaruhusiwa.