Ikiwa Taasisi Za Umma Zinabambikia Kesi Wananchi Wao Wasio Na Hatia, Je Haki Itapatikana Wapi?

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:

Siku ya Jumanne tarehe 18 Mei 2021, Raisi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakati akizindua Karakana ya kushonea sare za Polisi alisema kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) tayari imeshafuta kesi 147 za kubambikiza, na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya hivyo pia.

Maoni:

Hatua hii ya kufutwa kesi hizo za kubambikiza imekuja kama utekelezaji wa maagizo ya Raisi aliyoyatoa wakati alipokuwa akipokea taarifa ya TAKUKURU iliyowasilishwa kwake tarehe 28 Machi, 2021.

Taarifa hiyo ilionesha wazi kuwa serikali ilishinda kesi 271 pekee kati 381 zilizofunguliwa katika mahakama tofauti katika mwaka uliopita 2019/2020. Hata hivyo nyingi ya hizi kesi zilikuwa ni za kubambikiza zinazohusiana na ukwepaji wa kodi, uvunjaji sharia katika matumizi mabaya ya ofisi, nk

Taasisi kama TAKUKURU kujihusisha na kubambikiza kesi watu wasiokuwa na hatia ni zaidi ya aibu, matumizi mabaya ya ofisi ya umma, kunajisi haki, kukebehi mchakato wa kusimamia haki na hivyo taasisi hiyo kupoteza uhalali wa kimaadili katika kupambana na kuthibiti rushwa.

Juu ya hayo, maswali mengi yanaibuka kuhusu TAKUKURU, kama vile: ni nani aliyewatuma kubambikizia watu kesi, kubambikizia huku watu kesi kulikuwa na lengo gani, ni adhabu gani watapewa wakosaji hao waliobambikia watu kesi, nini watalipwa kama fidia wahanga wa kesi hizi za kubambikiza, nk

Kuhusiana na kesi za kubuni na kubambikia watu, Waislamu wa Tanzania wamekuwa wahanga wakubwa wa suala hili na kwa muda mrefu wamekuwa wakiteseka katika mkono wa sheria ya kibaguzi na ya dhulma, yaani Sheria ya kuzuiya Ugaidi. Sheria hii ya kikoloni imeasisiwa na wakoloni wamagharibi ili kuwarahisishia ajenda yao ya unyonyaji wa rasilimali na kupambana na Uislamu kama inavyoshuhudiwa sehemu mbalimbali ulimwenguni, wakiingilia kati mifumo ya ulinzi na usalama na taasisi za kusimamia haki kama Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na kulazimisha taasisi hizo kutengeneza mashtaka ya  uwongo  na kesi za kubambikiza  za ugaidi  dhidi ya wasio na hatia.

Katika hali hii, serikali za nchi zinazoendelea, kwa kuwa hazijali watu wao wanatumika na mataifa ya kikoloni hususan Marekani katika kupambana na Uislamu kwa jina la kupambana na ugaidi. Na matokeo yake nchi changa kama Tanzania zimeshikilia mahabusu mamia kama siyo maelfu ya Waislamu wasio na hatia kwa kesi zisizo na mashiko za ugaidi na za  kuhatarisha usalama wa nchi,  ili tu kuwaridhisha mabwana zao wakoloni Wamagharibi na  kwa kupewa hongo kwa jina la fedha za kupambana na ugaidi.

Wanaharakati wengi wa Kiislamu, masheikh, maustadh na Waislamu wa kawaida wamewekwa mahabusu kwa miaka mingi sasa kwa kisingizio cha “uchunguzi unaendelea”. Kwa mfano mwaka 2011 viongozi na wanachama wa jumiuya ya “Uamsho” waliwekwa ndani na kubambikiwa kesi ya ugaidi. Pia mwaka 2017 wanachama watatu wa Hizb ut Tahrir Tanzania: Ustadh Ramadhan Moshi Kakoso, Pamoja na Omar Salum Bumbo na Waziri Suleiman Mkaliaganda walitekwa, kuzuiliwa na kisha kubambikiwa kesi ya ugaidi, na wengine wengi katika mikoa mbalimbali kama vile Tanga, Mwanza, Arusha, Lindi, Pwani, nk, wote hawa wapo vizuizini kwa miaka mingi bila ya ushahidi wowote kuletwa dhidi yao.

Ni wakati sasa kwa vyombo vya usimamizi wa haki ndani ya Tanzania kurejesha imani kwa watu kwa kushikamana na taratibu sahihi za kisheria, kwa kuwasilisha ushahidi mahakamani dhidi ya watuhumiwa kama wanao, au wawape watuhumiwa dhamana, au wawaachie watuhumiwa huru mara moja.

Imeandikwa na Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.