Ijue Kampeni ya ‘Ramadhani na Muongozo wa Quran’

(Ramadhan 1440 Hijri)

1. Kwanini kampeni hii muda huu?
Licha ya kuwa kampeni hii inapaswa iwe ya wakati wote, lakini kutokana na mwezi mtukufu wa Ramadhani
kufungamanishwa na kuteremshwa Quran, ni wazi mwezi huu unastahiki zaidi kwa kampeni hii. Allah Taala
anasema:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنْ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ

“Ni mwezi wa Ramadhani ndio ambao imeteremshwa humo Qur’an kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi”

2. Lipi lengo la kampeni ?
Kuwarudisha wanadamu kwenye muongozo sahihi wa Quran kwa kufungamanisha Quran na Ramadhani. Kwanza, kwa Waislamu kwa kuwa wao ndio wabebaji na Waumini wa Quran, kuwakumbusha na kuwafafanulia kwa kina nafasi ya kitabu hicho katika maisha ya kila siku kikiwa ni muongozo kamili kwa wanadamu wote. Pili, kuwapa changamoto wasiokuwa Waislamu waanze kuitafiti Quran na Uislamu kwa jumla, kwa kuwa Quran ni muongozo kwa wanadamu wote, pamoja na ukweli kwamba wasiokuwa Waislamu hawalazimishwi kuingia ndani ya Uislamu, lakini bado hupaswa kusimamiwa na muongozo wa Quran.

3. Jee kampeni hii inaanza lini na itachukua muda gani?
Kampeni hii itazinduliwa rasmi siku ya Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Shaaban 27 Shaaban 1440 / 03 Mei 2019 sehemu mbali mbali mara baada ya Swala ya Ijumaa na itaendelea katika kipindi chote cha Ramadhani.

4. Jee kampeni itafanyika maeneo gani ?
Kampeni hii itafanyika takriban katika miji yote mikubwa kama Dar es Salaam, Zanzibar, Tanga, Pemba, Mtwara, Mwanza nk.

5. Jee kampeni itatumia mbinu gani?
Kampeni hii itahusisha mbinu mbalimbali ili kuwafikia watu wa aina tofauti. Miongoni mwa mbinu hizo ni mihadhara, khutba za Ijumaa, darsa za misikitini na penginepo, risala za wiki, uandishi wa makala magazetini, vipeperushi, mitandao ya kijamii kama facebook, twitter, whatsapp, tovuti, kuandaa futari za pamoja, warsha na semina ndogo ndogo, itikafu, utoaji wa kalima katika maeneo ya wazi, vipindi vya redio na Tv nk.

6. Kampeni itajikita kufafanua mambo gani?
Kampeni hii itatia nguvu kuweka ufahamu na ufafanuzi kwa hadhira katika nukta zifuatazo :
a. Haja ya mwanadamu kuhitaji muongozo kutoka kwa Muumba pekee na sio wa kibinadamu.
b. Muujiza wa Quran na dalili ya kuwa kwake kitabu kutoka kwa Muumba
c. Namna watu walivyokuwa zama za jahilia kabla ya Quran
d. Mapinduzi makubwa ya Quran kwa waarabu wa zama zile
e. Quran ni muongozo wa zama zote mpaka leo
f. Quran ni muongozo, na ili isibakie kuwa nadharia hulazimu awepo kiongozi na dola ya Khilafah kuutabikisha.

7. Jee Waislamu wana jukumu gani kwa kampeni hii ?

Pamoja na kuwa sisi ndugu zenu wa Hizb ut Tahrir Tanzania tumejitolea kuwa mbele zaidi katika kampeni hii, haina maana kwamba kampeni hii ni milki yetu, bali kiasili kampeni hii inamuhusu kila Muislamu, kwa kuwa Waislamu wote ndio Waumini wa Quran na wabeba risala yake. Hivyo, tunawaomba Waislamu wote wawe tayari kushirikiana nasi katika kuifanikisha kampeni hii kabambe. Aidha, wawe tayari kujumuika nasi kwa namna moja au nyengine ikiwemo kutupatia fursa kila inapowezekana iwe katika misikiti, vyuo, madrassa, kushiriki na kuchangia katika mitandao ya kijamii, na kuutunganisha na taasisi mbalimbali ili kufanikisha kampeni hii adhimu ya uwajibu wa kuirejesha nafasi ya Quran katika maisha ya wanadamu.

Kwa kumalizia, tunakumbusha kauli mbiu ya kampeni ni ‘Ramadhani na Muongozo wa Quran” na hashtag ni: #RamadhanNaMuongozoWaQuran.

Tunawaomba wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kama facebook na twitter wasisahau kuweka hashtag hiyo katika maandishi yao.

Tunamuomba Allah Sw. Atupe tawfiq tufunge Ramadhani kwa imani na kutaraji malipo Yake (imaan wa Ihtisaban). Pia Aifanikishe kampeni hii iwe chanzo cha nusra ya Waislamu mashariki na magharibi – Amiin

26 Sha’aban 1440 Hijri / 02 Mei 2019 Miladi

https://hizb.or.tz/

https://twitter.com/Hizb_tanzania

https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

#RamadhanNaMuongozoWaQuran

Maoni hayajaruhusiwa.