Huku Ndio Kuwanusuru Ndugu Zetu Wa Turkistani Mashariki
Kutokana na mateso yanayowasibu ndugu zetu wa Turkistan Mashariki chini ya serikali ya China, ya kuteswa, kubakwa, kuritadishwa, kulazimishwa kunywa ulevi na kuuza, kuhasiwa na mengineyo, Waislamu takriban wote pia na kundi la wapenda haki wamesimama kupaza sauti na kuionesha dunia madhila hayo ili ndugu zetu hao watokane na dhulma hiyo.
Hata hivyo, kuepusha shari hizi na nyenginezo mfano wake hulazimu kuwepo hatua ziada za kivitendo na sio kauli pekee. Licha ya kuwa kulaani na kupaza sauti ni matendo yanayosaidia. Lakini kubakisha kauli zetu katika kupaza sauti pekee bila ya hatua za kupelekea hatua za kivitendo, ni khiyana kubwa kwa ndugu zetu na pia ni kuonesha kuwa tuna ufahamu mdogo wa dini yetu.
Waislamu marejeo yetu ni Kitabu na Sunnah za Mtume saw, na viwili hivyo vinatufundisha kuwa sio sahihi mahali pa matendo kuweka maneno matupu, ikiwa pana uwezo, au kinyume chake.
Kwani hatusomi visa mbalimbali ndani ya Qur-an namna vinavyotuonesha uwekaji wa kila kitu mahala pake? Kwa mfano, Nabii wa Allah SW Yaaqub As. alivyotenda. Kwa kuwa alikuwa na yakini kuwa mwanawe Yusuf As. yuko hai hakuacha kufuatilia habari zake kwa watu mbalimbali pamoja na kuwa aliitakidi kuwa subra ni jambo jema.
فَصَبْرٌ جَمِيلٌ عَسَى اللَّهُ أَنْ يَأْتِيَنِي بِهِمْ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ (يوسف:
“…Basi subra ni jambo zuri ! (nami nasubiri). Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ni Mjuzi na Mwenye hikma” (Yusuf : 83)
Aidha, Nabii Yaaqub hakukaa tu bali alichukuwa hatua za kivitendo mpaka mwisho akawaagiza wanawe waende wakawatafute Yuusuf na nduguye:
يَا بَنِيَّ اذْهَبُوا فَتَحَسَّسُوا مِنْ يُوسُفَ وَأَخِيهِ وَلاَ تَيْئَسُوا مِنْ رَوْحِ اللَّهِ (يوسف: 87
” Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye wala msikate tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu….” (Yusuf: 87)
Aidha, tunaona katika sira ya Mtume SAW namna alivyohama Makkah kwenda Madina. Kamwe Mtume SAW hakuhama mpaka kapewa ruhusa na Allah SW, lakini hakuondoka tu kimafamba bali alipanga mpango wa uhamaji wake kwa umakini wa hali ya juu.
Miongoni mwa aliyoyatenda:
a-kumlaza kitandani kwake Sayyidna Ally ra. ili kuwaghilibu makureishi
b-kumkodi mtambuzi wa njia za majabalini ili awaongoze njia.
c-kutafuta mtu wa kuwaletea chakula, kinywaji na habari za maquraish
d-kutoka usiku, ilhali watu wamelala nk.
Kwa hivyo, ni lazima na sisi tufanye hatua za kivitendo kuwanusuru ndugu zetu wa Uyghur, ila jambo hilo limefungwa kwa amri na hukmu za kisheria, na mwenye mamlaka hayo ni dola pekee. Tusighilibike na unafiki wa baadhi ya nchi za Waislamu hususan Uturuki kujidai kuilaumu na kuitaka China kuwatoa Waislamu katika kambi za mateso kwa maneno matupu, ilhali ina uwezo wa kupeleka jeshi kuwanusuru na kuwakomboa Waislamu hao.
Uislamu kupitia Mtume SAW umetuonesha kuwa katika dhulma kama hizi ni lazima serikali iende kuzinusuru heshima, mali na damu za Waislamu. Kama pale Mtume SAW alipopeleka jeshi kwenda kuwatia adabu wayahudi wa Bani Qaynukai walipovunja heshima ya mwanamke mmoja tu wa Kiislamu.
Vilevile Khalifah Muutasim ametuonesha mwenendo kama huo wa Mtume SAAW, pale askari wa Kiroma alipomkashifu mwanamke wa Kiislamu, na mwanamke huyo kunadi “wayaaa Muutasim” (Ewe Muutasim). Waroma wakamcheka kwa kejeli na kumwambia huko aliko Iraq atakusikia. Jambo hili likamfanya Muislamu mmoja avunje yake aende kwa Khalifa Muutasim na kumpasha taarifa ya mkasa wote na kilio cha Yule mwanamke. Khalifah Muutasim kwa haraka aliitikia wito huo muda huo huo kwa kupeleka jeshi lililowatia adabu Waroma na kumkamata askari huyo khabithi na kufanywa mtumwa kwa mama huyo, ingawa mama huyo alikataa, ila adabu hiyo iliwakomesha waroma kuuchezea Uislamu na Ummah wa Kiislamu kwa jumla.
Kwa ufafanuzi huo ni wazi inakuwa faradhi kwetu kuacha kila tulichonacho kufanya kazi ya kumtawaza Khalifah katika nchi kubwa ya Kiislamu, ili achukue hatua za kivitendo dhidi ya dhulma kama hizo za China, za Mabudha ndani Burma, Afrika ya Kati nk.
Ni muhimu pia tupaze sauti zetu kwa ulimwengu ili watawala wakhaini ndani ya Ummah huu wadhihirike uovu na uongo wao mbele ya Ummah, pia kwa wale wenye hatamu za mamlaka waweze kuzitumia nguvu hizo kuukomboa Ummah wetu mtukufu.
Ali Amour
Mjumbe wa Afisi ya Habari
Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.