Hijja Yathibitisha Umoja Wa Kimaumbile Kwa Ummah Wetu

Waislamu kwa mamilioni kutoka maeneo mbali mbali ulimwenguni tayari wanaendelea kutekeleza ibada ya Hijjah katika mji mtukufu wa Makkah. Ibada hii inatukumbusha wito alioutoa Nabii Ibrahim AS pale alipoamrishwa na Allah SWT kuwatangazia watu kwenda kuhiji katika nyumba tukufu ya Al- Kaaba. Allah Taala anasema:

وَأَذِّنْ فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالاً وَعَلَى كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِنْ كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ 
“Na watangazie watu habari za Hijjah, watakujia kwa miguu na (wengine) juu ya kila mnyama aliyekonda(kwa machofu ya safari) wakija kutoka maeneo ya mbali”(TMQ Hajj:2)

Nabii Ibrahim AS alikuwa katika mji wa Makkah kwa wakati huo uliokuwa jangwa bila ya wakaazi, wala hakumiliki vyombo vya kileo kama vipaza sauti, simu au televisheni ya kupeperushia wito wake. Lakini alitekeleza kwa utiifu mkubwa amri ya Allah Taala bila ya kuhoji. Leo hii tunashuhudia misururu na misafara ya watu kutoka kila pembe ya dunia kuitikia wito huo. Waislamu kutoka makabila, mataifa, mabara tofauti wanakusanyika katika kuitekeleza ibada hii, wote wakiwa kitu kimoja, na kuweka mbali kabisa ikhtilafu zao za kimadhehebu na mitizamo yao katika masuala mbali mbali. Huu ni mfano mzuri na dhihirisho la wazi kwamba umoja wa Waislamu ni jambo linalowezekana. Aidha, inatuonyesha bayana kwamba ni ufahamu wa kimakosa kwamba Waislamu hawawezi kuwa kitu kimoja kwa dalili ya kwamba kuna madhehebu na ikhtilafu nyingi miongoni mwa Waislamu. Huu ni ufahamu batili na haufai kubebwa na Muislamu kwani Allah Taala Amefaradhisha Waislamu wawe kitu kimoja pale aliposema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلاَ تَفَرَّقُوا
“Shikamananeni na kamba ya Allah (Uislamu) Wala Musifarikiane” (TMQ Imran: 102)

Hivyo maadamu umoja ni faradhi kwa Waislamu basi bila shaka unawezekana kwani Allah Taala hawezi kufaradhisha jambo ambalo haiwezekani kulifikia mwanadamu. Pili, Waislamu huwa lazima kuwa kitu kimoja katika mambo ya kimsingi (Usuulu-ddin) na huruhusiwa kutafautiana katika mambo ya furu’u (matawi). Mambo ya kimsingi ni kama aqeeda, mfano kuamini Mungu Mmoja, Mitume wake, malaika, siku ya malipo, moto, pepo nk. Pia huingia mambo ya faradhi kama mfano sala, hijjah, funga ambayo hutakuta tofauti kati ya Waislamu wote ulimwenguni juu ufaradhi wa swala, idadi ya rakaa nk. Aidha, mambo ya furu’u ni kama namna ya utiaji wa udhu, kufunga mikono kwenye swala, kuweka ndevu nk. Haya ni mambo ambayo yana ufahamu zaidi ya mmoja na ndio maana wakapatikana maulamaa waliotangulia mfano Imam Shaafi, Imam Malik, Imam Ahmad bin Hambal nk. ambao walikuja na ijtihadi zao katika mambo haya kwa kutegemea dalili fafanuzi kutoka kwa Mtume wetu SAAW.

Kilicho katazwa kwa Waislamu ni kufarikiana (Firka) kama ilivyokuja katika Ayah وَلاَ تَفَرَّقُوا na maana yake ni kutafautiana katika mambo ya msingi wa dini mfano kupatikane watu wanaodai kwamba Qur’an haijakamilika, hiyo si ikhtilafu bali ni firka. Aidha, ikhtilafu/kuikhtalifiana ni jambo ambalo linakubalika kisheria na walikhtalifiana maswahaba wakati wa uhai wa Mtume SAAW na baada ya kufa kwake katika mambo mbali mbali ya dini na hili halikuwa chanzo cha mizozo wala migogoro (Rejea kitabu cha Nidham-ul Islam kilichoandikwa na Taqiuddin Annabhani). Lakini zilipokuja zama za mporomoko na kushuka kwa kiwango cha elimu kama ilivyo leo katika jamii ya Kiislamu watu wengi wakiwemo baadhi ya walinganizi wakakosa ufahamu huu na badala yake wakawa ni wenye kulazimisha rai walizozibeba na kudhoofisha rai za wengine japo zina dalili za kisheria. Jambo hili ikawa ndio chanzo cha mitafaruku na mizozo miongoni mwa jamii ya Kiislamu.

Enyi Waislamu, wakati tukiadhimisha masiku kumi matukufu katika mwezi huu mtukufu ni muhimu kufahamu kwamba Waislamu sote ni kitu kimoja na umoja wetu kikweli utadhihirika chini ya dola la Kiislamu ya Khilafah na dola itapambana na kila fikra ya kiubaguzi imma uzalendo, ukabila, urangi, utabaka, utaifa nk. ambayo itavunja umoja wetu.

Maoni hayajaruhusiwa.