Fiqhi Ya Kiislamu Juu ‘Hati Miliki’

بسم الله الرحمن الرحيم

Kila tarehe 26 Aprili ya kila mwaka ni siku ya Kimataifa ya Milki za Kifikra (World Intellectual Property Day).
Maana ya milki za kifikra ni kama ubunifu, uvumbuzi, wazo, fikra, maarifa anayoyatoa mtu binafsi, kikundi au taasisi nk.
Miongoni mwa dhana inayotumika kuhifadhi milki za kifikra ni dhana inayoitwa “hati miliki (copy right)
Hii ni dhana inayokusudiwa kuhifadhi umiliki wa fikra, wazo au uvumbuzi wa kimaandishi wa mtu kwa kumzuiya mtu mwingine asiyekuwa mtoa wazo hilo kuiga, kutawanya au kutumia wazo hilo bila ya idhini ya mzaa wazo hilo au mbunifu wa fikra hiyo wa asili.
Hatimiliki wameweka wamagharibi katika kuendeleza ukoloni, uchoyo, ukiritimba na roho mbaya katika kuenea maendeleo duniani kwa usahali na kwa haraka.
Lau kama si dhana hii katili ya hatimiliki huenda dunia ingekuwa katika hali ya ajabu ya sayansi na teknolojia.
Kabla ya kufafanua mtazamo wa Kiislamu juu ya hatimiliki ni muhimu kufahamu namna mtazamo wa kibepari unavyolifafanua na unavyoonesha sura ya jambo hili :
a. Hati miliki ya mtu ni milki yake kama milki nyingine za mwanadamu kama vitu vya kushikika kama nyumba, gari, nk.
b. Hatimiliki ni miongoni mwa mambo yanayosimamiwa kimataifa chini ya shirika maalumu la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na uhifadhi wa milki za kifikra linaloitwa World Interlectual Property Organization (WIPO) lililoundwa mwaka 1967, lenye wanachama 193 ikiwemo Tanzania. Lengo la shirika hilo ni kuhamasisha ulinzi wa milki za kifikra duniani ikiwemo suala la hati miliki.
c. Haki miliki ya mtu inalindwa kisheria ulimwenguni kote, na kuna sheria nyingi zimetungwa kuhifadhi milki hiyo. Kwa mfano, Tanzania ina sheria maalumu inayoitwa Copyright and Neighbouring Rights Act.5. Na taasisi inayoitwaThe Copyright Society of Tanzania (COSOTA) ndio taasisi yenye dhamana ya usimamizi wa masuala ya hati miliki.
d. Haruhusiwi mtu mwengine kutumia au kunufaika na milki hiyo ya kifikra, kielimu au kiubunifu bila ya idhini ya mmiliki asili.
Uislamu na Hatimiliki
Uislamu haukubali wala hautambui dhana ya hatimiliki kwa sababu zifuatazo:
1. Inadumaza akili za watu na ni kipingamizi cha ubunifu au kuzidisha ubora juu ya kitu kilichobuniwa na mwingine.
2. Dhana hii inapingana na uhalisia wa maisha ya wanadamu. Kwa sababu wanadamu katika dunia wamekuwa wakitegemeana katika ubunifu na uvumbuzi. Kinachodhihirika ni kuwa wakati wote wanadamu hufanya ubunifu na uvumbuzi, na wanadamu wengine huja kuzidisha au kuboresha elimu au ubunifu wa waliomtangulia tokea zama za binadamu wa mwanzo. Mfano hai, nchi za magharibi waliiba vitabu vingi vya wabunifu na wavumbuzi wa Kiislamu ambavyo vimewaongoza katika ubunifu wa mambo mbali mbali. Kwanini wavumbuzi wapya nao wasilipe kwa wavumbuzi na wabunifu waliotangulia ?
3. Dhana hii ina dhulma, kwa sababu inampokonya umiliki wa dhati kwa mtu. Mathalan, vipi mtu aliyenunua kitabu, lakini kwa mujibu wa fikra ya hatimiliki hana haki ya kukichapisha nakala zaidi, kupiga kopi, kuuza nk.? Hii maana yake yeye si mmiliki wa kitabu hicho. Lakini pia hata kama amegaiwa bure tayari ameshamiliki, kwani hata mtu akipewa kitu bure huwa amemilikishwa. Hivyo, lazima awe na umiliki kamili wa kitu hicho.
Jambo hili lazima liwe bayana kwamba ikiwa mtu ana mawazo, maarifa au uvumbuzi akauza au kuutoa kwa mwengine kazi yake hiyo ya kifikra, iwe kwa sura ya maandishi kama kitabu, makala au kwa namna nyengine kama sauti kama kutoa muhadhara nk. Basi mzaa mawazo au ubunifu huo hana umiliki tena juu ya kitabu alichouza, au muhadhara alioutoa au chochote alichotawanya bure chenye wazo, ubunifu au fikra alizoandika. Na wale walionunua, kupokea, kusikiliza watakuwa na umiliki kamili wa kitabu, makala au fikra zilizomo.
Kwa hivyo, kwa mujibu wa Uislamu walionunua kitabu huwa wamemiliki na wanaruhusiwa kutoa nakala zozote watakazo, au kama ni wazo au ubunifu kutokana na maandishi hayo au sauti wanaweza kuutumia na kuutanua kwa kuuboresha bila ya idhini ya mtoaji wa asili. Kwa kuwa, kitendo cha kununua kitabu, kupewa bure au kuwa katika muhadhara wa wazi maana yake amemiliki.
Uislamu unachokataza unapotawanya kitabu, makala au muhadhara wa mtu fulani lazima umnasibishe mtoaji wa asili. Na inapotokea umeongeza au kupunguza katika kazi hiyo ni haramu kumnasibisha mtoaji wa asili, kwani atakuwa yeye sio tena mwenye kazi hiyo.
Kwa hivyo, yule ambaye anataka wazo, ubunifu, fikra zake zibakie kuwa zake peke yake na sio za mwengine, abakize katika akili yake au katika makabrasha yake kibinafsi anayohifadhi bila ya kutawanywa hadharani kama kitabu au muhadhara. Katika hali kama hiyo endapo mtu atamuubia makabrasha yake aliyohifadhi kibinafsi kama katika laptop yake, mwenye kufanya hivyo atakuwa ametenda haramu. Lakini makabrasha yakiwekwa hadharani kwa muundo wa kitabu, makala au muhadhara maana yake yapo huru kumilikiwa na wengine na kuyatumia au kuyatawanya kwa namna watakavyo.
4. Dhana ya hatimiliki ni sehemu ya kuibana na kuificha elimu isisambae. Na hilo ni haramu katika Uislamu. Mtume SAAW anasema:
من كتم علماً ألجمه الله يوم القيامة بلجام من نار
‘Atakaye ficha elimu Mwenyezimungu atamvisha hatamu za motoni’
Katika jambo la aibu ni kuona vitabu vya dini ya Kiislamu ati navyo vinashikilia dhana hii batil ya kimagharibi ya hatimiliki vikiandikwa :
“Haki miliki imehifadhiwa hairusiwi kufanya chochote ila kwa idihini ya mtunzi”
Risala ya Wiki No. 204
25 Shawwal 1446 Hijri | 23 Aprili 2025 Miladi
Afisi Ya Habari – Hizb Ut Tahrir Tanzania
(Kutoka Jarida la Khilafah No. 61- Shawwal 1446 Hijiria —Aprili 2025 Miladia)

Maoni hayajaruhusiwa.