Elimu Zanzibar: Filamu ya Vichekesho Endelevu
Zanzibar ikiwa ndio iliyotoa shule nne katika shule kumi za mwisho katika matokeo ya kidato cha sita (A level) yaliyotangazwa karibuni, jinamizi hili la kutisha linaendea ‘kuicharura’ Zanzibar kwa miaka kadhaa sasa mutawaliya (mfululizo).
Matarajio ya wengi ni kuona mikakati thabiti na mipango ya SMZ katika kujikwamua na ‘ndwele’ hii, lakini wapii! tunachokishuhudia ni filamu ya vichekesho hususan kwa watendaji wake wakuu wa Wizara ya Elimu kana kwamba hakuna lililojiri au kama vile wanafurahia na kuridhia fedheha hiyo.
Itakumbukwa mara baada ya kutangazwa matokeo hayo mabaya ya aibu kwa Zanzibar tuliona tunadiriki kusema ni kichekesho cha aina yake ! tulimshuhudia Waziri wa Elimu Mhe. Riziki Pembe Juma akiwa katika hafla ya kumpongeza na kumpa zawadi mwanafunzi mmoja wa Zanzibar, nasisitiza mwanafunzi mmoja, wa shule ya Feza (shule binafsi) aliyeshika nafasi ya saba kitaifa (sayansi), hafla hiyo ikitendwa kwa mbwembwe, madaha na kujifakhiri. Kana kwamba matokeo ya mwanafunzi huyo mmoja, tena wa shule binafsi, ndio fidia ya ‘maziroo’ na matokeo ya shule nne ‘matiroo’ katika kumi, tena skuli za mjini Zanzibar.
Hatujakaa vizuri, filamu ya viroja hiyoo! bado inaendelea, si ya kucheka, ila inabidi tucheke ! karibuni Waziri huyo huyo wa Elimu akiwa katika jimbo la Kikwajuni alitoa matamshi yanayoashiria hali ya mkanganyiko, mpaka tunaandika makala hii bado hatujaelewa, Waziri Pembe alikusudia kuunga mkono kitu gani, na anapinga kitu gani.
Waziri huyu wa Elimu katika mkutano wa jimbo la Kikwajuni alisema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi ‘kuhangaika’ kwenda kujisomea masomo ya ziada “tuition” hali ya kuwa walimu wanaowasomesha ‘wanatosha’ katika ufundishaji wao.
Katika kauli hiyo ya Waziri, maneno mawili, ‘kuhangaika’ na ‘wanatosha’ ni vidokezi (indications / qarina) kwamba wanafunzi waachane na masomo ya ziada (tution).
Tahamaki ! mara Waziri huyo huyo, tena hapo hapo, walau ingekuwa siku nyengine, anatuambia kuwa, kuna baadhi ya walimu wamekuwa wakikwepa vipindi vyao, hali ambayo imewafanya baadhi ya wanafunzi kuamua kusoma masomo ya ziada (tution). Bila ya Waziri Pembe kutaja sababu za walimu kukwepa vipindi hivyo, lakini sasa waziri anaonekana kana kwamba anaunga mkono suala la wanafunzi kuwa na masomo ya ziada (tution) ambalo awali alilipinga, kwa sababu walimu wanakwepa vipindi vyao.
Nae Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni Mhe. Hamad Yussuf Masauni, mwenyeji wa mkutano huo akaja na suluhisho la masomo ya ziada (tution) kwa jimbo lake, Mbunge huyo akawataka wanajimbo wake wawatumie walimu waliomaliza muda wao kazini kuandaa masomo ya ziada (tution) kwa ajili ya wanafunzi. Sasa sijui tuseme hili ni suluhisho alilolikataa Waziri au kuliunga mkono. Viwe viwavyo kwa mfumo wa kidemokrasia mkanganyiko kama huu ni kawaida na maarufu.
Mfumo wa kidemokrasia umejengwa na kuishi juu ya mhimili wa usanii , vioja na maslahi, na wanasiasa wake ndio kielelezo chake, hawajawahi kuwa na tembe ya shauku ya kubadilisha hali, wala kutatua matatizo kwa udhati wake, wanachojali ni maslahi yao katika hali yoyote, wakihesabu usiku na mchana kwa khofu siku za kumaliza muda wa ‘uluwa’ wao.
Uislamu kinyume na siasa hizi za kimaslahi, kwanza unawataka watu wote wasimame kidete kuunyoosha uongozi (Khilafah) ili usimamie majukumu yake ipasavyo. Lakini kubwa zaidi Uislamu unalifungamanisha suala la uongozi wa Umma na maisha yajayo ya akhera, likiwa ni dhima kubwa mbele ya Muumba.
Viongozi watakaotekeleza majukumu yao ipasavyo Kiislamu na kwa uadilifu watalipwa ujira mkubwa mbele ya Mola wao. Na viongozi watakaopuuza katika kubeba majukumu hayo ipasavyo, wakawa hawana insafu, uadilifu na wakaufanyia khiyana Umma. Hao ni mfano wa viongozi waovu wanaowadhulumu raia na kuwapeleka katika maangamizi, basi wajiandae kwa adhabu kali ya moto.
وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَدْعُونَ إِلَى النَّارِ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ لاَ يُنصَرُونَ (القصص: 41
“Na tuliwafanya wao (walioshika mwendo huo) kuwa viongozi wanaongoza kwenye Moto. Na Siku ya Kiyama hawatonusuriwa” (AL-QAS’AS: 41)
Risala ya Wiki No. 51
05 Dhu al-Hijjah 11440 Hijri / 06 Agosti 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.