Elimu Bora ni Chini Ya Khilafah Pekee.

Sera ya elimu Tanzania na katika nchi za dunia ya tatu ambazo takriban zote haziko huru kisiasa, kiitikadi, kiuchumi, kiutamaduni nk. ni kauli mbiu tupu zisizo na muelekeo thabiti wala dira iliyonyooka.

Tunashuhudia mporomoko mkubwa wa kiwango cha elimu kila kukicha licha ya kunadiwa sera ya elimu ‘bure’ kama ilivyotangazwa Zanzibar mara baada ya mapinduzi ya mwaka 1964, na kama inavyonadiwa sasa Tanzania Bara.

Utoaji wa elimu na sera zake katika nchi changa kwa bahati mbaya haulengi kutoa wavumbuzi, wanasayansi, wanafikra thabiti (thinkers) na wanasiasa mahiri wa kuweza kuelewa na kuchukuwa hatua za kimfumo dhidi ya njama, mikakati na mipango ya mataifa ya kibepari katika kuzinyonya na kuzitawala nchi changa. Bali sera hizo huzalisha wasomi wanaomakinisha ukoloni mamboleo, watetezi wake na wanaoulinda mfumo wa kibepari kwa gharama zote.

Matokeo yake elimu ya sayansi hufundishwa kinadharia pekee ili kujaza madaftari. Bila ya kutaja ukosefu wa walimu wenye sifa hususan katika masomo ya sayansi, ukosefu wa madawati, umbali wa kijografia wa wanafunzi, bila ya kutaja ukosefu mkubwa wa vifaa vya kutosha vya maabara au kukosekana kabisa.

Hapa Tanzania tunashuhudia wanafunzi kufundishwa masomo kwa kiswahili lakini mada ‘notes’ huandikiwa kwa kiingereza. Tunashuhudia pia mrundikano mkubwa wa wanafunzi madarasani, si ajabu darasa kukusanya zaidi ya wanafunzi hamsini tena wanaogaragara chini kwenye vumbi bila ya vitabu!

Katika mazingira kama haya ni ndoto kuweza kuzalisha wanafunzi wenye viwango, wabunifu wa kweli na wavumbuzi wa kuweza kuzikomboa nchi hizi na madhila ya ukoloni mambo leo. Licha ya kupazwa juu sauti ya uwepo wa elimu bure.

Uislamu chini ya dola yake ya Khilafah huzalisha wasomi wa uhakika wanaoikomboa jamii katika hali zote iwe kijamii, kiuchumi, siasa ya nje na ndani na ufanisi wa juu kabisa wa kuitoa jamii katika makucha ya madhalimu wa aina zote ulimwenguni.

Elimu chini ya Dola ya Khilafah katika hatua ya msingi na kati itatolewa bure, kwa maana ya bure, ikiwa na kiwango cha ubora wa hali ya juu. Na katika hatua ya juu itatolewa kwa kadiri ya mahitaji na kulingana na uwezo. Lakini pia dola itatoa fursa hata kwa walio nje ya shule na vyuoni kwa kuwawezesha kufanya tafiti na uvumbuzi. Kitabu cha Nidhamu ya Uislamu (Sheikh Taqiudin Nabahan) kikifafanua kuhusu Sera ya Elimu kinasema:

‘Kusoma yanaomlazimu mtu katika nyanja tofauti za kimaisha ni faradhi juu ya kila mtu, mwanamume au mwanamke. Kwa hivyo, kusoma ni lazima juu ya wote katika marhala ya kwanza na ya pili; na ni juu ya Dola kuwasomesha wote bure. Kadhalika ni juu ya Dola kufungua nafasi za elimu ya juu ya bure kwa kadri ya uwezo wake”.

Na kwa upande wa vifaa na mbinu kinaendelea kitabu hicho kutaja haya:

“Dola hutayarisha maktaba ya vitabu, maabara za utafiti na mbinu zote za kuzidisha maarifa nje ya shule na vyuo vikuu ili kuwawezesha wenye nia ya kuendeleza utafiti katika maarifa tofauti kama fiqhi, usul-ul-fiqh, hadith, tafsiri na pia fikra, utabibu, uhandisi, elimu ya kemia, uvumbuzi, maendeleo mapya nk. ili kuzalisha idadi kubwa ya mujtahidina, watunzi na wenye kuvumbua vitu vipya.”

Aidha, sera ya elimu katika Dola ya Khilafah ni kuhakikisha elimu inayotolewa inawajenga wanafunzi kuwa viumbe bora katika ardhi watakaoungoza ulimwengu katika muelekeo wake unaostahiki. Maadili mema na uwajibu wa kubeba majukumu kwa Umma ni katika vipaumbele katika sera yake, kwa kuwajenga kuwa na shakhsia bora ya Kiislamu.

Sera ya namna hiyo ndio iliyotoa wasomi wa kupigiwa mfano katika ulimwengu mzima chini walioandaliwa na dola ya Khilafah kabla haijaangushwa mwaka 1924. Dola hiyo ilikuwa mbele katika elimu za fani mbali mbali na kuwa kivutio kikubwa kwa watu wa Ulaya na maeneo mengine. Na kwa udhati ndiyo sera itayotumika leo chini ya dola ya Khilafah Rashida ya Pili, tunayoitarajia kurudi tena karibuni Inshaallah.

Risala ya Wiki No. 16

25 Muharram 1440 Hijri | 05-10- 2018 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.