Eid Ul- Udh-Hiya na Jukumu Letu la Kujitolea Muhanga’ Kwa Ajili ya Uislamu

فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَابُنَيَّ إِنِّي أَرَى فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَى قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِنْ شَاءَ اللَّهُ مِنْ الصَّابِرِينَ
“Basi alipofika makamu ya kutembea naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja.Basi angalia wewe waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyoamrishwa, utanikuta mimi Insha’Allah katika wanaosubiri.” [TMQ 37:102]

Hivi ndivyo Qur’an Al-Kareem inavyotusimulia tukio kubwa, tukufu la aina yake na la kihistoria ambalo katika masiku ya Sikukuu ya ‘Eid ul udh-hiya’ huwa tunalikumbuka. Tukio ambalo mafunzo, mawaidha na msimamo wake ni changamoto inayotukabili Umma wetu wa Kiislamu leo.

Ni tendo kubwa la kujitolea muhanga wa aina yake lililotendwa na Baba wa Mitume Ibrahim (AS) la kumtoa dhabihu [kumchinja] mwanawe Nabii Ismail (AS), licha ya kuwa aliruzukiwa mtoto katika umri wa uzeeni. Na wakati alipopewa agizo la kumchinja tayari mtoto huyo alikwishaanza kutembeatembea nae huku na kule jambo linalopelekea moja kwa moja mzazi kuihisi ladha tamu na manufaa ya mtoto wake. Lakini pamoja na yote hayo baba na mwana walinyenyekea kikamilifu kwa agizo kutoka kwa Allah Ta’ala kwa unyenyekevu usio na mfano bila ya kuhoji kwa hoja za kiakili ili kutafuta nyudhuru za kishetani kukwepa amri ya Mola wao . Yote hayo ni kwa sababu hiyo ni amri kutoka kwa Mola wao Allah Ta’ala.

Kwa hakika, jambo hili litabakia kuwa ni mazingatio, fundisho na mawaidha ya milele yasiyokatika kwa Umma wetu na ndio maana likasimuliwa ndani ya Qur’an Al-Kareem ili liwe Muongozo na dira thabiti katika maisha yetu ya kila siku. Allah Taala nasema:

وَكُلاًّ نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنْبَاءِ الرُّسُلِ مَا نُثَبِّتُ بِهِ فُؤَادَكَ وَجَاءَكَ فِي هَذِهِ الْحَقُّ وَمَوْعِظَةٌ وَذِكْرَى لِلْمُؤْمِنِينَ
“Na yote Tunayokisimulia katika habari za Mitume ni kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa waumini” [TMQ 11:120]

Wakati tukiliangalia tukio hili na kufaidika nalo kwa funzo kubwa la msimamo wa kujitolea muhanga kwa ajili ya Allah Ta’ala, ni lazima pia kuifahamu fikra ya ‘kujitolea muhanga’ kwa kina kwa mujibu wa Uislamu.

Niwajibu kuelewa tunapojitolea muhanga amma wa mali, nafsi, wakati au hata uhai katika njia ya Allah iwe ni kwa ajili Yake Allah Ta’ala pekee. Na si kwa ajili ya kutaka sifa, umaarufu, kuonekana na watu au kupata maslahi fulani. Bali iwe kusudio letu lote na pekee kwa amali hiyo ya muhanga ni kutaka radhi Zake Allah Taala pekee na si zaidi ya hivyo. La sivyo, itakuwa amali ya kumshiriki Mola na itaambulia patupu kesho Akhera.

Aidha, ieleweke kujitolea muhanga kuwe ni katika mambo ambayo Sheria ya Kiislamu imeyaruhusu pekee. Huo ndio huwa ni muhanga kwa mujibu wa Uislamu. Kwa hivyo, kupoteza mali, nafsi na muda katika masuala ya haramu kama kuhamasisha na kuchangia katiba za kikafiri au mchakato wa chaguzi za demokrasia, mambo hayo na mithili yake kamwe si muhanga, na si tu kuwa ni kupoteza rasilmali bila ya malipo yoyote. Laa bali mambo hayo hilo ni maangamizi mbele ya Allah Ta’ala kwa kuwa ni kuchangia mambo ya haramu. Enyi Waislamu, zingatieni vizuri jambo hili!

Kujitolea muhanga pia hulazimu mtu asijifunge tu katika baadhi ya majukumu fulani ya kiSheria na kuyaepuka mengine, kana kwamba baadhi ya majukumu hayatuhusu na yanawahusu watu fulani. Kwa mfano, baadhi ya Waislamu huyafungamanisha maisha yao ya Kiislamu na baadhi tu ya amali kama ndio dini yote kwa kujihusisha nayo na kujitolea muhanga majukumu hayo fulani fulani ya kibinafsi pekee kama swala, saumu, hijja nk. huku wakiwacha majukumu mengine. Ilhali Uislamu ni dini kamili na pana unaobeba majukumu mengi ya kibinafsi pamoja na majukumu ya Umma mzima ambayo kamwe mtu binafsi hawezi kuyatekeleza peke yake. Moja wapo ya jukumu kubwa la Umma mzima ni suala nyeti la kurejesha tena maisha ya Kiislamu katika ulimwengu kwa kupitia kurejesha tena Dola ya Kiislamu ya Khilafah kwa kumpa ba’ya (ahadi ya kumtawaza au kumtii Amiri wa Waislamu wote). Jambo ambalo ni suala la kufa na kupona. Amesema Mtukufu wa darja Mtume (SAAW) katika hadithi iliopokewa na Imamu Muslim:
“Yoyote anayekufa bila ba’ya juu ya shingo yake amekufa kifo cha kijahiliha!”

Changa moto hii ni nzito inayotukabili Waislamu sote na inayohitaji tujitolee muhanga kwa gharama yoyote ikiwa ni nafsi, mali na hata uhai wetu ikibidi bila ya kuogopa vitisho, propaganda chafu, lawama ya mwenye kulaumu au vikwazo mbalimbali vinavyowekwa na makafiri na wakala wao katika kuzorotesha amali ambayo ndiyo ukombozi kwa Umma wa Kiislamu na wanaadamu wote.

Ikumbukwe kwamba muhanga katika suala la ulinganizi lazima uwe ndani ya kikundi/chama. Kwa sababu hata Mtume (SAAW) licha ya kuwa ni kiumbe mtukufu aliyeruzukiwa kila aina ya kipawa lakini katika ulinganizi wa Uislamu alijumuika kwa kushirikiana na maswahaba zake kama kundi la pamoja na sio kama amali ya kibinafsi binafsi.

Mwisho, ni muhimu kutupia macho Uislamu namna ilivyosheheni watu wema namna walivyojitolea muhanga katika kila chao ili kufanikisha amma katika kuusimamisha ,kuilinda dola mara baada ya kusimamishwa kwake, kufanya fathi ulimwengu mzima nk. Mifano ni mingi kama walivyojitolea masahaba Ammar bin Yasir, Ali bin Abi Twalib, Bi Khadija, Bi Sumayya, Suhaib Ar-Rumi, Abubakar As-Siddiq, Mus’ab bin Umayr, Umar bin Al-Khatwaab (Radhi za Allah ziwafinike wote) na wengi wengineo. Pia kuna waliokuja baada yao kama Tariq bin Ziyad, Salahuddin Al-Ayyubi nk. Pia kuna ndugu zetu wa leo sehemu mbalimbali duniani kuanzia Somali, Iraq, Afghanistan, Burma, Philipines nk. bila ya kuwasahau mashujaa wa Syria wanaopambana usiku na mchana kwa mwaka wa nne sasa ili kulinda dini yao na heshima yao dhidi ya mikono ya muuwaji, katili, kafiri Bashar Assad anayepewa kila aina ya msaada na makafiri ili kuzuiya kurudi tena dola tukufu ya Kiislamu ya Khilafah ndani ya Biladu Sham. Kwa hakika muhanga wa ndugu zetu hao ni wa aina yake lau tutauelezea hapa kwa maandishi ya dhahabu kamwe haitofidia thamani yake.

Amesema kweli Allah ‘Azza wa Jalla kwa kusema:

رِجَالٌ لاَ تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلاَ بَيْعٌ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ وَإِقَامِ الصَّلاَةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ يَخَافُونَ يَوْمًا تَتَقَلَّبُ فِيهِ الْقُلُوبُ وَالأَبْصَارُ
“Watu ambao biashara wala kuuza kwao hakuwashughulishi na kumdhukuru Allah, kusimamisha swala na kutoa zakaa. Wanakhofu siku ambayo nyoyo na macho yatakapogeuka!” [TMQ 24:37]

Tunamuomba Allah Taala katika masiku haya matukufu Aunusuru Umma wetu mashariki na Magharibi na Atupe nusra yake kama alivyoabashiri Kipenzi chake SAAW kwa kurudi tena dola ya Khilafah kwa manahaj ya Utume – Amiin

Na Masoud Msellem

 

Maoni hayajaruhusiwa.