Dhulma Ya Kamari Za Utabiri Wa Matokeo Ya Soka (Kubeti) Na Ukimya Wa Serikali

Moja katika masuala yaliyotajwa kuwa ni kero kubwa katika mkutano wa ikulu karibuni baina ya Raisi na viongozi wa dini, lilikuwa ni suala la kusheheni kwa vitendo vya uchezaji kamari. Makala hii chini iliandikwa na mwandishi wetu miaka miwili iliyopita kuliangazia suala la kamari kwa kina. Kwa faida ya wasomaji tunaichapisha tena hapa:

Mpira wa miguu (soka) ni moja kati ya michezo inayopendwa na watu wengi hususan vijana hapa Tanzania na duniani kwa ujumla. Mchezo huu kama ilivyo michezo mengine hujumuisha pande mbili za mashabiki ambao huonesha ushabiki ndani na nje ya uwanja. Wapo ambao hufikia hatua ya kuwa maadui na mahasimu kwa sababu ya upinzani. Wengine kwa ushabiki wao hufikia hata kuzimia na kupoteza fahamu katika kushabikia timu zao. Kwa mfano, shabiki mmoja mwanamke Saudia aliamua kuingia upande wa mashabiki kiume katika kuonesha ushabiki wake uliopitiliza mipaka.

Ushabiki wa timu katika soka unachangiwa na mambo kadhaa, ikiwemo kuwapenda wachezaji nyota, vipawa vyao, asili zao, tabia zao, aina ya ushangiliaji wao, rangi wanazotumia, maisha yao nk.
Kwa miaka ya karibuni Tanzania pamezuka wimbi kubwa la ongezeko la makampuni yanayoendesha shughuli za kamari (kubeti). Wananchi hususan vijana wamejikuta wakipoteza fedha nyingi na muda kwa kuweka dau pindi timu zinapocheza. Iwe ligi za ndani au ligi za Ulaya kama Uingereza, Hispania, Ujerumani na Ufaransa.

Miaka mitano iliyopita makampuni haya ya kamari ya utabiri wa soka yalianzishwa na wafanyabiashara wa ndani kama majaribio. Kuonesha matokeo chanya na kuteka vijana wengi kumepelekea kumiminika msururu wa makampuni haya ambayo yamekuwa ni mwiba mkali nawa hatari kwa vijana wengi, ustawi wa kijamii na taifa kwa ujumla.

Tangu mwaka 2010 mpaka sasa kuna makampuni 12 ya kamari ya soka. Kuna vituo rasmi 2,684, nchini, nusu yake vikiwa Dar es Salaam pekee. Kamari hii mara nyingi huchezeshwa kupitia mawakala, ambapo ili kushiriki mchezaji lazima achukue ratiba ya timu zote na vifupisho vyao, yaani “code” zao. Kisha huangalia alama za timu na kuzijumlisha alama hizo kwa mujibu wa kiasi cha pesa anachoweka. Baada ya hapo wakala ambapo humchapishia na kumpatia orodha ya timu na kiasi cha pesa anachotarajiwa kupata lau atashinda, maarufu kama “mkeka” Na baada ya kupata mkeka husubir timu kucheza, na zikishinda ndipo eti hujipatia pesa ambazo ni jumla ya kiasi cha fedha na idadi ya alama za timu alizochagua.

Kimsingi, yapo madhara meng yanayosababishwa na kamari hii ya “kubeti” kama zilivyo kamari nyengine. Kubwa zaidi ni kumuasi Allah Taala kwa kujihusisha na kitendo ambacho kimekatazwa kwa dalili za kukata (qatw-ii) yaani moja kwa moja. Kamari hii kama ilivyo yoyote hupelekea kuongezeka umaskini kutokana na dhulma inayofanywa na makampuni haya kwa raia ambao hupambiwa na kuvutika na uraibu wake.

Vijana wengi wamepoteza pesa zao nyingi katika “kubeti”. Wengine wamepoteza mali zao za kuhamishika kama nyumba, magari nk. kwani kamari ni kamari ni nadra sana kushinda. Kijana mmoja amecheza miaka 5 na kupoteza zaidi ya Tsh milioni 5, mwingine amecheza miaka 3 amepoteza dola 18,000 sawa na Tsh milioni 38 (Jamii forum November 17, 2010)

Kamari hii imezalisha uzembe wa matarajio hewa kwa baadhi ya watu. Vijana wengi wamekuwa hawafanyi kazi za kuingiza kipato kwa bidii na ipasavyo. Kwa kuwa wamo ndani ya matarajio ya hadaa wakiamini kwamba ipo siku watashinda katika kamari hii kuwa matajiri na kukomboka na umaskini. Jambo ambalo ni ndoto ya mchana.

Katika hali hii wamejikuta wakipoteza muda mwingi katika kamari hii bila mafanikio. Mchezo huu mchafu wa hadaa na wizi umepelekea kuvunjika kwa familia na kuzuwa tafrani katika jamii. Vijana wanapuuza majukumu yao ya kifamilia na kuwekeza katika kamari. Yaani inatokea mtu akachukua hata pesa ya matumizi ya msingi nyumbani akaenda “kubeti”, na familia kubaki na njaa. Hali inayopelekea kusababisha kutoelewana katika familia. Tamaa ya utajiri wa haraka na uzugwaji wa akili (hadaa) na makampuni ya mabwenyenye wanaonufaika na kamari imewafikisha vijana wetu katika hali hiyo.

Katika baadhi ya familia vurugu na sintofahamu zimesababishwa na vijana kuchelewa kurudi nyumbani kutokana na kusubiri mechi mpaka usiku sana ili kujua kama wameshinda katika kamari au hawajashinda. Baadhi ya shule na vyuo imepelekea kushuka ufaulu kwa baadhi ya wanafunzi wachezaji wa kamari hii, huku baadhi kusimamishwa masomo kutokana na kamari hii na baadhi wamekuwa wakipoteza muda mwingi katika “kubeti”. Hivyo, kukosa muda wa kujiosomea. Taifa, vijana na ustawi wa jamii unateketea na kuangamia kutokana na kushamiri kwa kamari hii. Hii ni hasara iliyoje kwa vijana na taifa kwa ujumla.

Madhara ya kamari yoyote ni mengi na makubwa kwa ubinadamu. Allah (S.W) kupitia kitabu chake kitukufu cha Quran katuonya na kutuharamishia moja kwa moja:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنصَابُ وَالأَزْلاَمُ رِجْسٌ مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ (المائدة: 90

“Enyi Mlioamini! Bila ya shaka ulevi na kamari na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi za shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa.” (TMQ 5: 91)

Kwa bahati mbaya na kama inavyotarajiwa kwa serikali zetu zinazodandia fikra za kibepari za kidemokrasia haziwezi kamwe kuondoa janga hili. Bali watalihamasisha kamwe! Kwa kuwa mfumo wa serikali hizo, yaani ubepari umejengwa juu ya msingi wa kuzingatia maslahi na sio zaidi. Hata kama jamii itadamirika na kuangamia. Cha kushangaza ! serikali ya sasa ya Tanzania imejigubika kiuwongo kauli mbiu ya “hapa kazi tu”, na kuwahi kutangaza kukabiliana na vijana wanaocheza ‘pool’ asubuhi.

Lakini ukiangalia kwa makini, lengo sio vijana, bali ni kutokana na serikali kutofaidika na hizo pool. Lakini katika upande wa hizi kamari, kwa kuwa serikali inafaidika kwa tozo na kodi huwa hakuna haja ya kuwasakama wachezaji wala wamiliki, iwe muda wowote utakaokuwa. Kwa msingi huo, kamwe haiwezekani kuondoshwa kamari hizi, licha ya kila mtu kukiri na kuona madhara na maafa yake wazi wazi. Na badala yake, serikali imekuwa ikishirikiana kikamilifu na makampuni haya ya kamari katika kuwaibia na kuwadhulumu raia wanyonge kimali na kifikra na kuangamiza muundombinu nyeti wa jamii, yaani vijana na familia. Tanzania na serikali zote duniani zimekuwa zikisajili kihalali kampuni hizi na kujikusanyia kodi kwa gharama ya kuangamiza na kuongeza umasikini kwa raia wao. Na hii ni kutokana na udhaifu wa mfumo wa kibepari kutegemea kodi zaidi katika vyanzo vya mapato yake. Licha ya kuwepo rasilimali mbali mbali za kuweza kujipatia mapato,kama maadini nk. Kilichopo hapa Tanzania ni rasilmali hizo kukabidhiwa makampuni makubwa ya kibepari kuchota watakacho, ati kisha kuwabana raia walipe kodi zaidi ili kukuza uchumi.

Uislamu kupitia dola yake la Khilafah ina vyanzo vingi vya mapato badala ya kodi kama hizi za dhulma. Pia itajihusisha na biashara kikamilifu. Hivyo, itaharamisha uovu huu, kama ulivyoharamishwa na Muumba. Na bado itakuwa na uwezo wa kuhudumia jamii bila ya kutetereka.

Kamari hizi ni changamoto kubwa kwa wasiokuwa Waislamu wajionee kwa jicho la yaqini (lisilo na shaka) namna mfumo wa kibepari na serikali zake ulivyokosa uwezo na uhalali wa kumhudumia mwanadamu. Kwa kuwa si mfumo wa uadilifu. Humdhulumu raia kwa kujiongezea maslahi. Basi haujafika muda kwenu kutafiti mfumo mbadala ambao ni Uislamu?

Amma Waislamu, nyinyi hamna namna ila kuunga mkono bega kwa bega juhudi za kurejesha tena nuru ya utawala wa Kiislamu wa Khilafah ulimwenguni. Kwa kuwa ndio utawala pekee wenye ghera na suluhisho la kukabiliana na kila dhulma ikiwemo kamari, inayomsababishia mwanadamu dhiki, tabu na kuzuwa uadui, bugudha na ugomvi kwa kumuondolea thamani yake kama kiumbe kilichotukuzwa na Muumba wake.

إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَنْ يُوقِعَ بَيْنَكُمْ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَنْ ذِكْرِ اللَّهِ وَعَنْ الصَّلاَةِ فَهَلْ أَنْتُمْ مُنتَهُونَ (المائدة: 91

“Hakika shetani anataka kukutilieni uadui na chuki baina yenu kupitia ulevi na kamari na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi jee mmekatazika” (TMQ 5 : 91)

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari

Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.