Demokrasia Inapoteza Imani na Mvuto Kwa Ummah

بسم الله الرحمن الرحيم

Kufuatia kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2020 wa Raisi, Wabunge, na Madiwani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Raisi wa Zanzibar, imezidi kudhihirika kuwa watu wamekata tamaa na mfumo wa kirongo wa kidemokrasia, lau si mawakala wa wakoloni na mitagaa yake katika nchi changa ungezikwa kabisa.
Tangu Wakoloni walivyotoa uhuru wa bendera kwa nchi zinazokoloniwa (dunia ya tatu) kisha kuweka watawala watakaotawala kwa niaba yao kupitia ukoloni mpya (mamboleo) na hatimaye kulazimisha mfumo wao wa maisha (ubepari) na mfumo wa kiutawala wa kidemokrasia kama ndio mfumo pekee wa kiutawala mwanzoni mwa miaka ya 1990, nchi changa hazijanufaika na chochote ila maafa yasiyosemeka.
Uhalisia wa Demokrasia ni ndoto isiyofikiwa, katika nchi kubwa kama Amerika huwa watu wachache huamua kiongozi na wananchi wa kawaida hupotezewa muda kwa kupiga kura ambazo huchukuliwa kuwa ni maoni tu yasiyolazimika kufanyiwa kazi.
Amma katika nchi changa (zinazokoloniwa), wakoloni huchagua wamtakae, amma kashinda kwa kura au la. Na mara nyingi mtawala huwa na mamlaka yote, mara nyengine huamua kwa niaba ya wakoloni kuhusu tume ya uchaguzi, lini uchaguzi ufanyike, nani ahesabu, nani ashinde na ashinde kwa kiasi gani nk.
Takwimu zinaonesha kila siku zinavyosonga mbele ndivyo demokrasia na ubepari wake unavyozidi kupoteza mvuto kwa watu, hususani watu wanyonge, wanaonyonywa, na waliokata tamaa.
Watu hawa ambao ndiyo walio wengi na ndiyo hudanganywa na kupotezewa muda kila baada ya miaka mitano au minne wakiambiwa eti wao huchagua viongozi, hali ya kuwa uhalisia wake hawachagui kamwe bali hupotezewa tu muda kwani mtawala katika nchi changa wakoloni ndio huwa wenye maamuzi juu ya kila kitu, na katika nchi kubwa za kibepari mabwenyenye kupitia wajumbe wachache huamua nani awe kiongozi.
Kushuka kwa ushiriki wa wananchi katika chaguzi ni kielelezo tosha kuwa jamii duniani inaongeza ufahamu wake kuhusu kutokufaa kwa nidhamu ya kidemokrasia, nidhamu ya kikoloni ya ubepari.
Watu wanajionea kivitendo kuwa demokrasia kuwa ni ndoto, ulaghai, urongo, isio na tija kwao, na lau si hongo ya madaraka, pesa kwa mawakala wapiga debe wa mfumo huu mchafu basi kutoweka kwake ingekuwa ni rahisi kama kupepesa macho.
Kwa mujibu wa takwimu nchini Tanzania kwa mfano, mwaka 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) ilifanikiwa kuandikisha idadi ya wapiga kura 22,658,247 Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(ZEC) iliandikisha wapiga kura 503,193 idadi ambayo ilifanya jumla ya wapiga kura kuwa 23,161,440. Waliopiga kura katika Uchaguzi wa Kiti cha Rais walikuwa 15,596,110 na tume ilimtangaza Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Mgombea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi kuwa mshindi wa kiti cha Rais kwa kupata Kura 8,882,935.
Mwaka 2020 idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ilifikia takribani milioni 29.8 na Idadi halisi ya waliopiga kura ni takribani milioni 15.0, hivyo takribani watu milioni 14.8 hawakupiga kura na mshindi wa kiti cha uraisi alipata takribani kura milioni 12.5
Mpaka hapa tunaona kuwa idadi kubwa ya wapiga kura huenda ilichangiwa na sababu nyingine kama kutaka kadi kwa ajili ya utambulisho hasa kufuatia ugumu wa kupatikana vitambulisho vya taifa.
Aidha, tunaona hapa utofauti mkubwa kati ya watu waliojiandikisha kupiga kura, waliopiga kura, na waliomchagua mshindi wa kiti cha uraisi.
Hakuna cha kuelezea hapa zaidi ya watu kukosa imani na mfumo huu fisidifu wa demokrasia, wamechoshwa na urongo wakidanganywa kuwa wao ndiyo huchagua viongozi na uhalisia uko kinyume na hayo.
Ni muda sasa Waislamu kusimama kidete kuonesha ubora wa Uislamu kama mfumo mbadala katika siasa na mengine kwa kupitia dola yake ya Khilafah.
Aidha, jamii kwa ujumla wakiwemo wasiokuwa Waislamu muda umefika ijitathmini kutokana na kiwango kikubwa cha hasara kama mauaji, chuki, mateso, kutekwa watu, visasi, ubakaji nk. Yote haya yameletwa na hili jinamizi la urongo la demokrasia.
Risala ya Wiki No. 98
16 Jumada al-awal 1442 Hijri 31 Disemba 2020 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

 

Maoni hayajaruhusiwa.