Barua ya Wazi Kwa Sheikh Alhad Mussa

16 Oktoba 2020 / 29 Safar 1442 Hijria
Kwa Sheikh Alhad Mussa Salum
Sheikh Mkuu wa Mkoa,
Dar es Salaam.
Asalaam alaykum,
YAH: NASAHA ZA KIISLAMU KUFUATIA KAULI YAKO YA KUOMBA DUA KWA JINA LA YESU
Kwa kuwa dini yetu imefaradhisha kuamrishana mema na kukatazana mabaya na kupeana nasaha za kutufikisha katika uchaMungu, tunakufikishia nasaha hizi adhimu kama ifuatavyo:
Mnamo tarehe 14 Oktoba 2020 katika ushiriki wako katika kampeni ya mgombea uraisi kwa CCM jijini Dar es Salaam katika kumuombea dua mgombea huyo ulitamka neno la kufru kwa kuomba dua kwa kupitia jina la Yesu kama wanavyotenda wakiristo. Jambo hilo ni kinyume na Uislamu, kama Allah SWT anavyosema:
وَلِلَّهِ الأَسْمَاءُ الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا ………(الأعراف: 180).
‘Na Allah ana majina mazuri mazuri basi muombeni kwa hayo’
Kitendo kile cha kutumia uslub/mtindo wa kikiristo kufanya ibada ya dua kimewahuzunisha sana Waislamu jumla kwa kuwa kimegusa aqida yao, kimetia aibu, fedheha na kuwashangaza wengi katika waliohudhuria na wasiohudhuria.
Katika kitendo kile Sheikh uliunganisha pamoja na jina la Mtume Muhammad SAAW ili kujaribu kupoza na kutengeneza uhalali wake. Hata hivyo, na bila ya tembe ya shaka kutokana na kuwa kwako mstari wa mbele katika harakati za ‘dini mseto’ kitendo kile hakina tafsiri yoyote, zaidi ya kukuza na kuendeleza dhana ya ‘dini mseto’ ambayo ni ukafiri wa wazi kwa mujibu wa Uislamu.
Kama utawahi kukumbuka Sheikh, wanaharakati wa Hizb ut Tahrir Tanzania tuliwahi kukuletea waraka wa nasaha mnamo mwezi wa Julai 2016 kukuhadharisha juu ya ukafiri wa fikra ya ‘dini mseto’. Waraka ule wa nasaha uliambatana pamoja na nakala ya makala yetu kutoka katika kijitabu chetu cha ‘Fikra za Hatari za Kuushambulia Uislamu na Kuimarisha Mtazamo wa Kimagharibi’ kinachofafanua pamoja na fikra nyengine ukafiri, dhambi, na khatari ya fikra hiyo ya ‘dini mseto’.
Aidha, tarehe 24/08 /2020 wakati Jumuiya yenu ya dini mseto (maridhiano) ilipofanya kinachoitwa kongamano la dua ya kuombea taifa jijini Dodoma, dua iliyoshirikisha watu wa dini nyengine pia nilitoa nasaha kwako kwa barua ya wazi kukuhadharisha juu ya uovu wa kitendo hicho.
https://web.facebook.com/pg/Afisi-ya-Habari-Hizb-ut-Tahrir-Tanzania-400663900784023/posts/?ref=page_internal
Tunakunasihi Sheikh na kukumbusha tena fikra ya ‘dini mseto’ unayoifanyia kazi na kuipigia debe ni fikra haramu ya wazi inayoweza kumtoa mtu katika Uislamu, na zaidi ni fikra isiyoingia hata katika mantiki, kwa kuwa kila dini ina misingi, imani, vigezo na ibada zake na namna ya utendaji wa ibada hizo. Na lau ingekuwa dini ziko sawa, basi kusingekuwa na dini zaidi ya moja. Kwa ufupi ni fikra inayolazimisha kisichowezekana.
Kumbuka Sheikh Uislamu umeweka kwa dalili za kukata, amma ni Uislamu au kisichokuwa Uislamu, na hakuna cha kati na kati.
فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلاَّ الضَّلاَلُ فَأَنَّا تُصْرَفُونَ (يونس: 32
‘Na kipo kitu gani baada ya haki (Uislamu) ila upotofu tu? Basi huwaje mkageuzwa?
Pia Uislamu umekataza kuchanganya baina ya haki na batil
وَلاَ تَلْبِسُوا الْحَقَّ بِالْبَاطِلِ وَتَكْتُمُوا الْحَقَّ وَأَنْتُمْ تَعْلَمُونَ (البقرة: 42).
‘Wala msichanganye haki na batil na mkaificha haki ilhali mnajua’
Sheikh tunamalizia nasaha zetu kwa nukta mbili kubwa:
Awali, hadhara ya Kiislamu inatufundisha kukupa wewe dhana njema (husni dhanni) kwamba pengine kwa kauli yako ile hukudhamiria wala hukuitakidi moyoni, bali pengine umetegemea taawil ya kimakosa, na kwa kuwa mafundisho ya Uislamu yanaiporomosha hata hukmu ya ‘hadd’ lau kuna shubha fulani fulani, hivyo kamwe hatuwezi kukutoa katika mila (Uislamu). Hata hivyo, katika hali kama hiyo Sheikh, Uislamu unakutaka kwa ikhlasi kabisa ufute kauli yako na ukiri makosa yako hadharani (kwa kuwa uliitoa hadharani), ujute na uombe maghfira kwa Mola wako.
Pili, lau Sheikh kwa kauli yako ile ya kuomba dua kwa jina la Yesu uliitoa kwa kukinai na kuitakidi moyoni, katika hali hiyo kihukmu utakuwa ‘murtad’ uliyetoka katika Uislamu.
Mola wangu shuhudia nimefikisha nasaha hizi.
أُبَلِّغُكُمْ رِسَالاَتِ رَبِّي وَأَنَا لَكُمْ نَاصِحٌ أَمِينٌ (الأعراف: 68
“Nakufikishieni risala kutoka kwa Mola wangu, na mimi kwenu ni mtoa nasaha muaminifu”
Sheikh Mussa Kileo
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano ya Umma
Hizb ut Tahrir Tanzania
Mob: 0684 393995

 

Maoni hayajaruhusiwa.