Baba Mzazi Wa Waziri Mkaliaganda (Mtuhumiwa Wa Ugaidi) Amefariki Dunia

Kwa huzuni na masikitiko makubwa tumepokea kutoka Mtwara Mjini taarifa ya kufariki dunia baba yetu mzee Suleiman Ismail Mkaliaganda, baba mzazi wa mwanaharakati wa Hizb ut Tahrir ambae amekuwa mahabusu kwa miaka 4 sasa kwa tuhuma za uonevu za ugaidi.
Mzee Suleiman Mkaliaganda anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 85 alifariki dunia usiku wa kuamkia leo huko Mtwara Mjini, baada ya kuwa na changamoto nyingi za kiafya kwa muda mrefu. Itakumbukwa kwamba katikati ya mwezi wa Juni mwaka huu, baadhi ya wanaharakati wa Hizb ut Tahrir Mtwara waliwahi kumtembelea marehemu kumjuulia hali na kumfariji kwa mtihani wa maradhi na kuwa mbali na mtoto wake.
Kwa mujibu wa taarifa za wanafamilia, maziko ya marehemu yatafanyika kesho Jumanne 27 Julai 2021 InshaAllah saa 4.00 asubuhi, katika makaburi ya Mswafa hapo hapo Mtwara mjini, ambapo Swala ya Jeneza itaswaliwa Masjid Nuur (hapo hapo Mtwara mjini), muda mchache kabla ya kuelekea makaburini.
Msiba huu unapaswa kuwa somo na mazingatio makubwa kwa vyombo na taasisi za kusimamia haki kutenda majukumu yao kwa uadilifu, kwa kuwa umekuja kumuongezea majonzi juu ya majonzi ndugu yetu Waziri Mkaliaganda, sio tu kwa kuondokewa na baba yake, lakini kwa kukosa kumuuguza mzazi wake (mtu mzima) na kushindwa kumzika kwa kuendelea kushikiliwa mahabusu kwa tuhuma za uwongo na za dhulma za ugaidi ambazo kwa miaka 4, Jamhuri imeshindwa kuleta hata kijipande cha ushahidi kuzithibitisha.
Hizb ut Tahrir Tanzania inatoa mkono wa ta’azia na kumfariji ndugu yetu Waziri Mkaliaganda, wanafamilia wote, wanaharakati wa Hizb ut Tahrir ndani ya Mtwara, ndugu jamaa na marafiki kwa msiba huu mkubwa.
Tunamuomba Allah SWT Awalipe wafiwa ujira mkubwa, Awamakinishe kwa subra katika kipindi hiki kigumu cha mtihani. Pia Tunamuomba Mola kwa unyenyekevu mkubwa katika mwezi huu mtukufu AWATIE MKONONI wale wote wanaomshikilia mtoto wa marehemu na wengine mfano wake kwa dhulma na uonevu.
Mwisho, tunamuomba Allah Taala Amsamehe mzee wetu, Amrehemu na kumuingiza katika Jannat-ul Firdaus.
Amiin
26 Julai 2021 M / 16 Dhul-Hijja 1442 Hijri
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.