Ammar bin Yassir: Kielelezo cha Subra, Elimu, Msimamo na Ucha Mungu

Machafuko ya kisiasa na kusambaratika jiji la Sabaa ndani ya Yemen kulipelekea makabila mbalimbli ya waarabu wa Yemen kuondoka nchi hiyo na kuhamia na kumanga manga sehemu mbalimbali kama vile Iraq, Najd, Yamama, Sham, Hijaz,Yathrib na kwengineko kwa ajili ya kutafuta hali bora ya maisha.Yassir (baba yake Ammar) muarabu wa Yemen kutoka kabila la Unas Mazhaj Qahtan nae aliondoka Yemen na kaka zake Harith na Malik, kwa lengo la kumtafuta ndugu yao mwengine aliyeondoka Yemen kutokana na hali ya njaa na ukame. Hata hivyo, jitihada ya kumpata ndugu yao huyo haikuzaa matunda. Hatimae Yassir (baba yake Ammar) akaamua kubakia na kuishi Makka akiwa msaidizi muaminifu wa Abu Hudhayf. Mmoja kati ya viongozi wa kabila la Bani Makhzoum.

Abu Hudhayf aliishi na Yassir kwa wema, uadilifu na mapenzi makubwa na hatimae akamuozesha mke aliyekuwa mtumwa wake, bibi Summaya bint Khayyat, ili Yassir aondokane na upweke, ugeni na kuanza maisha mapya ya kifamilia. Yassir akakubali kufunga ndoa na bibi Summaya, na wakajaaliwa kupata mtoto jasiri katika tareekh ya Kiislamu, sahaba mtukufu na maarufu Ammar bin Yassir ra. ambae kiumri alikaribiana sana na Mtume SAAW.

Familia ya Yassir ilineemeshwa kuwa familia ya mwanzo ambayo watu wake wote waliikubali nuru ya Uislamu. Na kutokana na unyonge wa familia hii, ugeni na kuwa kama wakimbizi ikafikwa na kila aina ya mashaka na mateso kutoka kwa mabwanyenye wa kikureishi hadi bibi Summaya ra. akauwawa shahid wa mwanzo akifuatiwa na mumewe Yassir.

Alikuwa ni Abu Jahl (laana ya Allah Ta’ala imshukie) ndie aliyendesha kampeni kali maalum ya kuitesa familia ya Yassir. Kwanza, kwa kuwa familia hiyo iliamua kuingia katika Uislamu. Pili, kwa kuwa ni wageni, wakimbizi na wanyonge. Tatu, kwa kuwa walikuwa chini ya kabila la Bani Makhzoum, ambalo ndilo kabila la Abu Jahl, na kwa hivyo kitendo cha kusilimu kwao Abu Jahl alikifasiri kuwa ni usaliti wa moja kwa moja dhidi ya kabila lililowapokea, kuwatunza na kuwapa hifadhi kipindi chote. Na nne, kitendo cha kusilimu kwa familia ya Yassir, Abu Jahl pia alihisi ni hatua ya kuliunga mkono kabila la Hashim, ambalo limewahi kumdhalilisha na kumfedhehesha Abu Jahl kwa fedheha kubwa isiyo na mfano. Hilo lilitokea pale aliposilimu Hamza ra. Na akaamua kumfuata Abu Jahl kumtaka aache mara moja kumnyanyasa mtoto wa kaka yake (Mtume SAAW), huku Hamza ra. akijafakharisha kwamba tayari na yeye ameshakuwa Muislamu.

Katika tukio hili Hamza ra. kwa ujasiri wa hali ya juu na kujiamini alimchoma mkuki wa kichwa Abu Jahl hadharani, kiasi cha Abu Jahl kutiririkwa na damu. Kitendo hiki ilikuwa fedheha na idhilali kubwa kwa Abu Jahl mbele ya watu. Lakini kutokana na nafasi (mustwaa) na haiba ya Hamza ra. pamoja na ushujaa na ujasiri wake, Abu Jahl alibaki kimya cha mfu na hakuweza kufanya chochote zaidi ya kuzipeleka chuki zake dhidi ya Bani Hashim. Kabila la Hamza ra. ambalo pia ndio kabila la Mtume SAAW na kuanzisha kampeni kuitesa familia ya Yassir.

Katika kulipiza kisasi kwa kipigo alichopewa Abu Jahl akaamua kuitesa familia ya Yassir kwa kuwaamrisha watumwa wake wamkamate Ammar na wamlete mbele yake, akaanza kumuhoji, na kukazuka majadiliano makali baina yao, huku Ammar kwa uhodari na ujasiri mkubwa alizipangua hoja dhaifu za Abu Jahl.

Kisha Abu Jahl akaamrisha watumwa wake: ‘Mkamateni mpumbavu huyu na mchapeni viboko labda anaweza kubadilisha misimamo baada ya kuchapwa mijeledi.’

Hapo Ammar akaanza kucharazwa viboko na kuteswa. Allah Ta’ala akateremsha Aya maalum katika Quran Tukufu kusifu msimamo wa Ammar na kuufedhehi uovu wa Abu Jahl na kumpa tahaddi (challenge) kwamba hatoweza kamwe kutoka gizani (ukafiri) na kwamba atakufa kafiri. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Allah Ta’ala anasema:

مِنْهَا أَوَمَنْ كَانَ مَيْتًا فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُورًا يَمْشِي بِهِ فِي النَّاسِ كَمَنْ مَثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ
‘Jee aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha na tukamjaalia nuru kwa nuru hiyo hutembea mbele ya watu, atakuwa sawa hali yake na alie gizani asiyeweza kutoka humo. ‘
(TMQ 6:122)

Abu Jahl hakutosheka na kumtesa Ammar pekee, bali alituma wahuni wake kuivamia na kuishambulia nyumba ya wazazi wa Ammar ra. na kuwakamata, kuwadhalilisha watu wazima madhaifu na kuletwa mbele yake kwa ajili ya mateso. Kuanzia hapo Yassir na mkewe Summaya nao wakaanza kuteswa, hatimae wakaunganishwa pamoja na mwana wao aliyefungwa minyororo. Ammar ra. alipoonana na wazazi wake akawaeleza kwamba anaendelea kuthibiti katika msimamo na akawataka na wao waendee kuthibiti katika msimamo. Baba yake Ammar, akamtaka mwanawe aendelee kuthibiti katika msimamo, kwa kuwa amebarikiwa, kwa kuwa Allah Ta’ala ameshusha aya maalum kwa mnasaba wa matendo yake mema na ibada zake.

أَمَّنْ هُوَ قَانِتٌ آنَاءَ اللَّيْلِ سَاجِدًا وَقَائِمًا يَحْذَرُ الآخِرَةَ وَيَرْجُو رَحْمَةَ رَبِّهِ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لاَ يَعْلَمُونَ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُوْلُوا الأَلْبَابِ
Jee afanyaye ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama na kuogopa akhera na kutaraji Rehma ya Mola wake (n isawa na asieyafanya hayo). Sema jee wanaweza kuwa sawa wale wanaojua na wale wasiojua? Wanaotanabahi ni wenye akili tu.’

(TMQ 39: 9 )

Abu Jahl alizidisha mateso yake kwa Familia ya Yassir na kuwataka ili wasalimike wamtukane Mtume, wauwache Uislamu na warudie kuabudu masanamu ya Lat na Uzza. Mateso yalizidi , na Mtume SAAW aliwazuru na kupiga magoti karibu na kila mmoja katika familia ya Yassir na kuwaeleza kwa kuwaliwaza na kuwapa bishara njema:

Subirini enyi familia ya Yassir, tayari mmeshaahidiwa pepo. Kisha Mtume SAAW akaelekeza uso wake mbinguni na kusema, Ewe Mola nimefanya kila ninaloweza (katika uwezo wangu kuwasaidia). Hatimae wazazi wa Ammar walikufa mashahid baada ya mateso kushtadi kama kuchomwa mikuki miilini mwao, na Ammar akabakia kuwa hai. Na akawa miongoni mwa Waislamu waliokwenda Uhabeshi mara ya pili.

Bada ya kusimama dola ya mwanzo ya Kiislamu ndani ya Madina, Ammar alikuwa mstari wa mbele katika kuilinda na kuihami dola hiyo, alishiriki kikamilifu katika kuujenga msikiti wa Mtume SAAW kiasi cha Mtume SAAW binafsi kukipangusa kichwa cha Ammar na mavumbi kwa mkono wake, kutokana kujituma katika kubeba kifusi. Aidha, Ammar ra. alishiriki kikamilifu katika vita mbalimbali vikiwemo Badr, Uhud na vita vya Handak. Na Mtume SAAW alieleza wazi katika matukio kadhaa kutamka hadharani kumwambia: ‘Ewe mwana wa Summaya, kundi potofu litakuuwa’.

Katika Khilafah ya Abubakar ra. Ammar ra. alishiriki kikamilifu kuilinda dola ya Kiislamu kwa kushiriki katika mapigano dhidi ya waasi wa raddah ndani ya Yammama hadi kukatwa sikio lake kwa upanga. Ndani ya Khilafah ya Umar, Ammar ra. aliwahi kupewa wadhifa wa kuwa Wali (gavana) wa mji wa Kufa ndani ya Iraq. Na katika Khilafah ya Uthman bin Affan, Ammar ra. alikuwa mstari wa mbele kuihisabu /kuiwajibisha dola hiyo katika matukio mbalimbali. Na baada ya kuchaguliwa Ali ra. kuwa Khalifa, na Muawiya bin Sufiyan kuasi uongozi wa Ali ra. Ammar alisimama kidete kuilinda dola halali (Khilafah ya Ali ra.) na kuulinda umoja wa Umma wa Kiislamu.
Kwa kuwa Mtume SAAW alishawahi kusema kwamba lazima kiongozi mkuu wa dola awe mmoja tu, na atakayefuata kumuasi kiongozi huyo halali basi ni wajibu apigwe vita. Kwa hivyo,

Ammar ra. aliekuwa na umri wa miaka 70 wakati huo pamoja na baadhi ya Waislamu walisimama kidete chini ya uongozi wa Imam Ali ra. kukabiliana na kikundi cha waasi kilichokuwa kikiongozwa na Muawiya bin Sufiyan katika vita vya Siffin.

Ammar ra. aliongoza kikosi cha farasi na alipigana kwa ushujaa mkubwa katika vita hivi. Ilipowadia siku ya tatu ya vita, Ammar ra. Akiwa na saumu katika medani ya vita, aliagiza aletewe kifungua kinywa baada ya jua kuzama. Akapatiwa kikombe cha maziwa kwa aljili ya futari.

Mara Ammar ra. alipokuwa anakunywa maziwa hayo alitabasamu na kucheka na kutamka: ‘Allahu Akbar’! Mtume wa Allah amesema kweli: Akaulizwa sababu ya tabasamu na tamko lake hilo. Hapo akajibu: Rafiki yangu Mtume SAAW aliwahi kunieleza kwamba, chakula changu cha mwisho katika dunia hii kitakua maziwa. Sasa ninajua kwamba wakati wa kukutana naye umewadia. Nilikuwa nikiusubiri wakati huu kwa muda mrefu sana,na kwa hamu kubwa. Hatimae huu hapa. Alhamdullillah’ Baada ya kunywa maziwa yale Ammar ra. akajitosa katika uwanja wa mapambano akapigana dhidi ya waasi na kuuwawa na kikundi kiovu kilichoasi dola halali ya Kiislamu kama alivyobashiri Mtume SAAW. Aliuwawa katika mwezi kama huu wa Saffar mwaka wa 37 Hijria.
Huu ukawa ndio mwisho wa maisha ya sahaba huyu mtukufu, ambae muhanga, subra, elimu na msimamo wake na kuilinda dola ya Kiislamu hauna mithili yake.

Leo ni wajibu vijana wetu katika Umma wa Kiislamu wajifakharishe na tareekh ya mashujaa wetu kama hawa na wengineo, na kuigiza mifano yao kwa kujitolea muhanga katika ulinganizi na kuilinda dola ya Kiislamu ya Khilafah Rashidah ambayo kurudi kwake hakuna shaka inshaAllah

#UislamuNiHadharaMbadala

(Aliuwawa safar 37 ah )

Maoni hayajaruhusiwa.