Dhana Ya Kupotezwa Watu Bila Ya Khiyari

بسم الله الرحمن الرحيم

Kupotezwa bila ya khiyari (enforced disappearance) ni kitendo cha kumpoteza binadamu bila ya khiyari yake na ghafla. Kupotezwa kwa lazima kwa raia imekuwa ni hali ambayo imejenga khofu kubwa sana kwa raia kwani raia wengi inapotokezea hali hii, wamekuwa wanaishi kwa hofu kubwa sana.
Tamko la Kimataifa la kuwalinda watu wote dhidi ya kupotezwa bila ya khiyari linakataza suala hili kwani humyima mtu haki zake za msingi.
Ili tukio liweze kutambulika kwamba ni kupotezwa bila ya khiyari ni lazima kuhusishwe na serikali hususan vyombo vya dola, kukataliwa kutajwa mahala alipo na kukandamizwa utu wake.
Katika siku za hivi karibuni nchini Tanzania watu wengi wamekuwa wanapotea na taarifa zao zimekuwa zinasambaa katika mitandao ya kijamii juu ya kupotea kwao.
Kupotea huko kumekuwa kunazua hali ya sintofahamu na taharuki ya hali ya juu. Baadhi ya watu ambao kupotea kwao kwa karibuni kulizua hali ya taharuki kubwa katika mitandao ya kijamii nchini Tanzania ni pamoja na Edgar Mwakalebela maarufu kama Sativa, Deusdedith Soka, Dionis Kipanya na wengineo ambao taarifa za kutekwa kwao zilisambaa kupitia mitandao ya kijamii.
Baadhi ya waliopotea walikuja kujitokeza hadharani na kutoa madai ya kwamba walipotezwa bila khiyari na vyombo vya dola.
Suala hili la kupotezwa bila ya khiyari si jambo geni kiulimwengu kwani Jumuiya ya kimataifa ilitunga kanuni tangu mwaka 1930 kupinga, na inalitambua kwamba hili ni tatizo, na ikateua siku maalumu ya kuwakumbuka watu wanaokumbwa na kadhia hiyo ambayo ni Agosti 30 ya kila mwaka.
Mwaka 2021 Shirika la Kimataifa la Kupinga Matukio ya Kupotezwa bila ya Khiyari liliripoti kesi takribani 46,490 za watu kupotezwa duniani ambapo kesi 4,785(10.3%) zilitoka nchi za Afrika. Katika kesi zilizotoka barani Afrika kesi nyingi zilitoka katika mataifa ya Algeria (3,253), Misri (289), Burundi (250), Sudan (177), Moroko (153) na Ethiopia (113)
Nchini Tanzania mwaka 2021, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (Legal and Human Right Centre) kilirekodi matukio 12 ya watu kupotezwa katika mikoa ya Lindi na Dar es Salaam pekee, kuanzia mwaka 2016 mpaka 2024 Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society) kilielezea matukio 83 ya watu kupotea ambapo yalinasibishwa na kupotezwa bila ya khiyari.
Matukio haya licha ya kuzua wasi wasi mkubwa nchini Tanzania pia yamesababisa kuwepo na mjadala mkubwa hususan baada ya taarifa za kupotea kwa mwanachama mwandamizi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo bwana Mohamedi Kibao
Licha ya juhudi kadhaa kufanyika katika kujaribu kukemea suala hili kama vile makongamano na maandamano baridi, lakini hali haijabadilika kwani ilipofika mnamo tarehe 13/11/ 2024 zilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii za watu waliokuwa wanamjaribu kumteka mfanyabiashara bwana Tarimo katika hoteli ya Rovenpick Resort iliyopo maeneo ya Kiluvya jijini Dar es salaam bila mafanikio
Sababu zinazoelezwa kushamiri kwa matukio haya kiulimwengu ni pamoja na kukosekana uvumilivu wa kisiasa, ambapo mbinu hiyo hutumika kuwadhibiti wakosoaji wa serikali, magenge ya uhalifu, uwepo wa sheria za kibaguzi kama za ugaidi nk.
Kwa ufupi, sababu msingi zaidi ni athari za mfumo fisidifu wa kibepari na ukoloni mamboleo.
Kwa mfano, katika siasa, kwenye chaguzi za kidemokrasia za siasa za kibepari tunashuhudia matukio mengi sana ya watu kupotezwa bila ya khiyari zao, na baadhi wamekuwa wanapatikana wakiwa tayari wameshafiriki na miili yao kutupwa katika maeneo mbalimbali. Na hii ni kutokana na ukweli kuwa mfumo wa kibepari na siasa yake ambayo inalenga zaidi maslahi na haudhamini usalama wala maisha ya watu. Kwa maneno mengine, siasa katika mfumo huo ni kutenda chochote ili kufikia malengo bila ya kujali uhai au utu. Na hiyo ndio tabia msingi ya mfumo huo.
Amma hili la magenge ya uhalifu mara nyingi huwa ni la kundi fulani kujipatia fedha za fidia kwa kumteka na kumpoteza mtu mashuhuri au kumuuwa kabisa ikiwa ni tishio kwao, masuala ya madawa ya kulevya na usambazaji wakje nk. Hapana shaka wakati mwengine makundi haya huwa yana mikono ya wenye ushawishi serikalini. Na dunia imeshuhudia makundi makubwa ya kimataifa yanayojuulikana kwa uhalifu kama huo kama Mafia (Italia), Russian Bratva (Urusi), The Sinaloa Cartel (Mexico) nk.
Jengine ni uwepo wa sheria kandamizi zinazowapa maafisa wa usalama nguvu ya kuwakamata na kisha kuwapoteza watu wanaonekana kama ni tishio kwa serikali bila ya kushitakiwa mahala popote pale. Sheria hizi kandamizi kama vile sheria za ugaidi zimetoa mwanya na ruhusa kwa wana usalama kutumia nguvu katika zoezi la kuwakamata washukiwa wa ugaidi kuwapoteza, kuwatesa, bali hata kuwauwa, huku zikitoa msamaha wa kutoshitakiwa kwa wanausalama hao pindi wanapokuwa wanatekeleza majukumu hayo.
Sheria hizi za ugaidi ni matokeo ya serikali za nchi changa hutekeleza matakwa ya mataifa makubwa ya kimagharibi kwa kupitisha kwa lazima sheria hizo ambazo huwadhuru raia wake kwa kuwapoteza bila ya khiyari, kuwatesa au hata kuwauwa ili tu kuwaridhisha mabwana wakubwa wa kimagharibi na kuendelea kupata posho zinazoitwa mifuko ya kupambana na ugaidi.
Janga la kupotezwa bila khiari lina athari kubwa kwa jamii, kwani uhai wa mtu hauna mbadala, jamii zinapoteza watu madhubuti na wenye uwezo. Wahanga wa karibu zaidi ni familia za watu wanaopotezwa ambao wao huathirika moja kwa moja kwa kutumia muda wa kumtafuta, kupoteza rasilimali, kusambaratisha familia, na kuathirika kiuchumi kwa jamii kama aliyepotezwa ni mtegemewa katika familia husika.
Matukio ya kupotezwa watu yanaonesha wazi kwamba mfumo wa kibepari, siasa yake ya demokrasia na sheria za kibaguzi za ugaidi ambavyo vyote ni matakwa ya wakoloni kikoloni kamwe haviwezi kulinda na kuthamini uhai, utu na usalama wa raia. Kwani ni mfumo huo ni aina ya utumwa kutoka nchi za magharibi na msingi wake umejengeka katika misingi ya kujali maslahi tu hata kama utu utaathirika.
Risala ya Wiki No. 198
29 Rajab 1446 Hijri | 29 Januari 2025 Miladi
Afisi Ya Habari – Hizb Ut Tahrir Tanzania
Imeandikwa na Kaema Juma

Maoni hayajaruhusiwa.