Athari Mbaya Ya Ubepari Kuunganisha Elimu Na Rizki
بسم الله الرحمن الرحيم
Ni dhahiri kwa mwenye macho na anayefuatilizia kwa umakinifu kuona kuwa nidhamu ya elimu katika mfumo wa kirasilimali/ kibepari imefeli. Hii ni kutokana na kule kuambatanishwa moja kwa moja na suala la riziki au ajira na mafanikio ya kiuchumi.
Dalili ya haya ni kauli mbiu ambayo husikika mara kwa mara wanafunzi wakihimizwa na walimu au wazazi kuweaka bidii ya juu masomo ili kuweza kujipatia kazi nzuri (mfano mzuri ni wimbo maarufu wa ‘someni vijana’). Serikali nazo zimechangia pakubwa tatizo hili katika kuweka mfumo wa alama (grading system) unaoleta dhana kuwa mwanafunzi atakayehitimu masomona alama za chini ameharibikiwa maishani.
Fahamu hii fisidifu imechangia pakubwa kuwepo majanga katika sekta ya elimu yakiwemo:
1)Uzalishaji wa washindani, watu wanaoamini na kupenda ushindani, hivyo washindi huiteka jamii yote. Walioshinda hujiona kama wao wanastahili fursa walizozichuma kwa tabu. Huku walioshindwa wakionekana kama wanaostahili hatma yao, yaani wale wanaofeli shuleni huonekana kuwa hawana ‘akili’ na hivyo hawastahili kazi na fursa nzuri za maisha, na hujiongeza namna ya kuendeleza maslahi yao binafsi kupitia biashara, kazi za ufundi,ajira za viwandani nk. bila ya kutilia maanani tena kutumia kiwango cha elimu alichofikia.
2)Wazazi kuwekeza jitihada kubwa kiasi cha kuchanganyikiwa na kutumia rasilimali nyingi kuwasomesha watoto, na pale watoto hao wanapopata matokeo kinyume na matarajio yao, hilo huwapa hali ya kuchanganyikiwa kupita mipaka kwa wanafunzi, wazazi na walezi kwa kudhani kwamba wameshakosa fursa ya ukombozi wao wa rizki na hata baadhi huchukua maamuzi ya kujitoa uhai kabisa.
3)Wakati mwingine huzuka tafrani kiasi kikubwa kwa kuharibu mahusiano mazuri mahala pa kazi (maofisini) baina ya mmiliki/ mwajiri na mwajiriwa/mfanyakazi, kwa kuwa bosi hutaraji uaminifu katika kazi yake ilhali mwajiriwa ana dhana kwamba ajira aitumikiayo ndio chanzo cha rizki na mapato yake yote kwa ujumla, yaani imma iwe kwa kusaidia ndugu, kujenga,kumiliki usafiri binafsi, kuoa na kuhudumia familia, hata kama anacholipwa si kiasi kingi hivyo cha kuweza kukidhi mahitaji yote hayo, mwajiriwa hulazimisha kuweza kupata hata kwa njia zisizo halali kama kuiba,kufanya ubadhirifu kwenye mali au miradi au kutengeneza mazingira ya rushwa, ilimradi apate kazini hapo. Kwa kuwa huona kazi hiyo ni matunda ya elimu yake aliyosotea miaka mingi, hivyo haina budi imfute jasho lake lote.
4)Wanafunzi kugeuka kuwa makasuku wa kukariri masomo kwa ajili ya kupata alama za juu za kutafutia ajira badala ya kuwa mufakkireena (thinkers).Tumefikishwa zama ambazo hakuna tena motisha ya kutafuta elimu isipokuwa ni uchu wa kutafuta makaratasi ili kupata ajira. Kwa wahadhiri wa vyuo limekuwa ni jambo la fursa la kutengeneza fedha watakavyo kutoka kwa wanafunzi wao kuwawezesha kupata alama za juu, na hili linatendeka kwa uwazi vyuo vingi.
5) Msongo wa mawazo kwa walimu na wanafunzi pale wanafunzi wanaposhinikizwa na wazazi, na walimu wakishinikizwa na bodi za shule kupata alama za juu ili kuzitafutia soko shule hizo. Natija yake ni yale tunayoshuhudia ya kukithiri udanganyifu katika mitihani ya kitaifa, wasimamizi wa mitihani hupewa hongo na baadhi ya wazazi kwa kushirikiana na walimu ili kuwaibia mitihani au kuwafanyia mitihani watoto wao kwa kuwabadilishia namba za watoto wengine na tuhuma zingine kama mashule kuteketezwa kwa moto ambapo yadaiwa baadhi ya walimu pia walihusika na kupanga matokeo kwa baadhi ya shule za binafsi. Malalamishi haya pia yamewahi kutolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA) bwana Athmani Almasi akisema amezifungia shule 24 matokeo ya darasa la saba amabazo zimethibitika kupanga na kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022 ,hivyo baraza limevifungia vituo hivyo hadi litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa shughuli za uendeshaji wa mitihani ya taifa.
Ama katika Uislamu, elimu na riziki ni vitu viwili tofauti wala havifai kuchanganywa au kimoja kufanywa kuwa sharti ya chengine. Chini ya serikali ya Kiislamu ya Khilafah, msingi wa siasa ya elimu ni Aqeeda ya Kiislamu. Nayo ni kumfahamisha mwanafunzi kuwa lengo kuu la kusoma ni kujitafutia radhi za Allah (s.w) kwa kunufaika nayo elimu yake na kuwanufaisha wengine. Na riziki kama mojawapo ya masuala ya aqeeda, haiko mikononi mwetu bali yatoka kwa Allah SWT peke yake na sio kwa mwanaadamu, na hili linatufanya tusiwe na babaiko la nafsi kwa kuwa yale tunayoyaona bila shaka ni hali tu ambazo hutokea rizki humo .
Zipo aya nyingi zenye dalili za kukata kwamba rizki inatoka kwa Allah SWT peke yake na wala si kwa mwingine.
إِنَّ اللَّهَ يَرْزُقُ مَنْ يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ (آل عمران:
“Mwenyezi Mungu humruzuku Amtakaye bila ya hisabu”.
(TMQ 3:37)
إِنَّ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ لاَ يَمْلِكُونَ لَكُمْ رِزْقًا فَابْتَغُوا عِنْدَ اللَّهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ
“Hakika hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa”. (TMQ 29:17)
وَكَأَيِّن مِنْ دَابَّةٍ لاَ تَحْمِلُ رِزْقَهَا اللَّهُ يَرْزُقُهَا وَإِيَّاكُمْ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ (العنكبوت: 60)
“Na wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi Mungu anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua”.(TMQ 29:60)
Amma Hadithi za Mtume SAAW zenye kutaja maudhui ya rizk ya mtu kwamba tayari imeshapangwa na kugaiwa kwa kiwango maalumu na kamwe mwanadamu hatoweza kulibadilisha hilo ziko nyingi, hapa tutaje hii moja:
لَوْ أَنَّ ابْنَ آدَمَ هَرَبَ مِنْ رِزْقِهِ كَمَا يَهْرُبُ مِنَ الْمَوْتِ لَأَدْرَكَهُ رِزْقُهُ كَمَا يُدْرِكُهُ الْمَوْتُ : وَسَلَّمَ عَنْ جَابِرٍ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ
Kutoka kwa Jabir ra. Anasema: amesema Mtume SAAW: ‘Lau mwanadamu ataikimbia rizki yake kama anavyoyakimbia mauti, itamfikia rizki yake kama yanavyomfika mauti” (Hadith Sahih)
Hatahivyo, Allah Taala amewaamrisha waja wake kufanya kazi na uwajibu huo unaangukia kwa kila mwanamme aliyebaleghe, mwenye akili timamu na mwenye uwezo wa kufanya kazi, kinyume na mwanammke, mtoto, mzee, mgonjwa na mwenye ulemavu usiomruhusu kufanya kazi. Hivyo, amri yamtaka mwanaume kuwa na shughuli inayoweza kumpatia kipato cha halali kinachomwezesha kupata/kupata mahitajio yake ya msingi ikiwemo chakula, mavazi na nyumba ya kuishi.
Na pia Allah Taala Amewajaalia waja wake uwezo wa kuchagua hali ambazo huja humo rizki, hivyo wao ndio ambao hufanya kwa khiyari yao moja kwa moja hali ambazo huja humo rizki yao lakini hali hizi sio sababu za rizki na wala wao sio ambao wanaleta rizki kama lilivyokuwa hili liko wazi katika aya zilizotangulia, bali Allah SWT ndio anawaruzuku
Lau tujaalie kwa mfano wa kupatikana kile kinachodaiwa kuwa ni kisababishi cha rizki, kama vile mtu kumiliki shahada ya elimu ya juu au kuwa na ajira ya uhakika na mshahara lakini utaona kuwa kuna wakati mwingine haidhamini upatikanaji moja kwa moja wa maisha mazuri ingawaje kazi anafanya na mshahara wake anaingiziwa kwenye akaunti yake lakini hutahamaki kujiona hana maendeleo, ndio wengine hudiriki kusema kazi au biashara nafanya, lakini pesa siioni, sio kwamba zinaibwa bali ashindwa kufahamu hakika ya mambo ya rizki ndivyo yakuwavyo kupita kwako kama daraja tu na wengine wanufaike. Na katika upande mwingine huwa inakosekana rizki pamoja na kuwepo kwa sababu hizo, na hili linaonyesha kuwa hizo ni hali na wala sio sababu. Mifano dhahiri ni kuwa wasomi wangapi wana maisha ya dhiki na duni hata machinga ana nafuu au ni matajiri wangapi waliotoroka shuleni au wakafeli kusoma lakini leo ndio wameajiri na kuwatumikisha wasomi kwenye biashara zao.
Hivyo, ifahamike wazi kuwa kupita au kutopita mtihani wa shule sio kipimo kinachoashiria kiwango cha riziki atayokuwa nayo mtu. Ajira au fani hutegemea uhodari au ujuzi wa mtu alioubeba akilini mwake katika fani fulani pasi na kuzingatia alama zilizoandikwa katika makaratasi ya mtihani. Mtazamo huu utawashajiisha wanafunzi kusoma kwa ajili ya kuwa wajuzi imara na sio kwa ajili ya kupita mitihani na baada ya hapo kusahau waliosomeshwa. Pia lengo la siasa ya elimu katika Uislamu chini ya serikali ya Khilafah litakuwa kuwasomesha wanafunzi elimu yenye maana kwao katika mambo ya kimaisha badala ya kuwabebesha mzigo wa masomo usiowaletea faida yoyote maishani mwao baada ya kuhitimu masomoni.
Kimsingi, dola ya Khilafah itachukua jukumu la kuwekeza katika tafiti na teknologia kwa lengo la kukuza vipaji katika fani mbalimbali zinazochangia kuboresha maendeleo na kubuni fursa muafaka zitakazo wawezesha raia wake kujikimu kimaisha ima kama wafanyakazi wa umma au wa kibinafsi, na dola kubeba jukumu lake la kusimamia upatikanaji wa mahitaji msingi ya mwanadamu na kuweka sera na usimamizi madhubuti kwenye usambazaji na matumizi ya rasilimali zote ikiwemo ardhi,maji na nishati mbalimbali ili kuhakikisha manufaa kwa raia wote.
Salum Maulid
Risala ya Wiki No. 160
12 Dhu al-Qi’dah 1444 Hijria / 01 Juni 2023
Afisi ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.