Adhabu Ya Viboko Kwa Wanafunzi
بسم الله الرحمن الرحيم
Adhabu ya viboko mashuleni imekuwa ikipingwa kitaifa na kimataifa. Itakumbukwa kwamba aliyekuwa Naibu waziri wa Elimu William Ole Nasha (marehemu) aliwahi kutamka bungeni kuwa anayeruhusiwa kuchapa wanafunzi ni Mkuu wa shule, makamu wake au mwalimu mwingine yeyote aliyepewa ruhusa ya kimaandishi, na idadi ya viboko visivyozidi vinne kwa makosa makubwa na hayo yawekwe katika katika kitabu cha kumbukumbu. (https://www.bbc.com/swahili/habari-45398915)
Kwa tamko kama hilo la Naibu Waziri ambalo bila ya shaka ni matokeo ya kampeni kimataifa dhidi ya adhabu ya viboko mashuleni, tunashuhudia juhudi kubwa zinaendelea kujenga uelewa kwa jamii, walimu, wanafunzi na wadau mbalimbali kwa kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina, mijadala nk. ili kutoa uelewa kuwa adhabu ya viboko kwa wanafunzi eti ni ukatili, unyama na hujuma.
Kwa hakika ufahamu huo ni wa kimakosa na wa hatari kuubeba katika kulikabili jukumu kubwa na zito la malezi ya watoto. Ni vyema katika kulizungumzia suala hili kugusia misingi miwili mikubwa inayotumika kutilia nguvu katika kumakinisha kampeni dhidi ya viboko.
a. Kuwepo kwa matukio kadhaa ya matumizi mabaya ya viboko kiasi cha kupatikanwa wanafunzi kujeruhiwa vibaya, kuzimia na wengine hata kuuwawa kama ilivyotokea kule Bukoba kwa mwanafunzi Kibeta Sperius Eradius (13) wa shule ya msingi.
b. Haja ya kuwepo adhabu mbadala badala ya viboko.
Kabla ya kuigusia nukta (a) kwa kina, lazima iwe wazi kwetu kwamba msukumo wa kupinga adhabu ya viboko mashuleni ni fikra inayotokamana na mfumo wa kibepari na fikra zake za ‘uhuru’. Yaani kumpa mwanadamu fursa atende atakalo, na kamwe haisukumwi na msingi wa ubinadamu. Kwa sababau kama ni suala la ubinadamu, madola ya kibepari ndio vinara wa kushiriki katika vita moja kwa moja au kuwasaidia vibaraka, vita ambavyo wahanga wake wakubwa ni watoto, vizee na wanawake. Hili liko wazi kuanzia vita vya Iraq, Afghanistan, Syria, Yemen nk. Kimsingi mfumo wa kidemokrasia wanaitumia fikra ya ‘uhuru’ kijanja, wakidai kwamba watu wawe huru kufanya watakavyo, ilhali ukweli wanautumia mwanya huo kupeleka maovu na ufisadi wao kama , zinaa, ulevi, ushoga nk. Ndio maana utaona wanapinga ndoa kwa wanafunzi wakidai bado wadogo, lakini hawapingi zinaa wala hawana mkakati wa kuwahifadhi watoto wa kike katika hayo mashule.
Kwa hivyo, lengo la kampeni dhidi ya viboko ni kujenga jamii fisidifu, wakijifanya kwamba wana imani na watoto, kwa kunadi kwamba utumiaji wa bakora ati ni ukatili, kiasi kwamba kwa kupitia mikataba na maazimio mbalimbali ya kimataifa hulazimisha nchi changa kufuata wimbi hilo, kwa guo la kuhifadhi haki za watoto.
Amma uwepo wa matukio ya walimu kuruka mipaka katika kuadhibu kwa viboko na bakora, hilo haliwezi kukanushwa, lakini sio hoja ya kupiga marufuku. Kwa sababu hakuna mahala ambapo watu hawaruki mipaka katika ubebaji wa majukumu yao. Wapo askari ambao hutumia silaha kinyume, wanasiasa kutumia madaraka vibaya na hata viongozi wa dini wako wanaopinda mafundisho kuhalalisha vitendo vyao vya kuruka mipaka.
Pia lazima iwe wazi kuwa ualimu ni sehemu ya ulezi. Hivyo, si kila mwenye cheti hufaa kuwa mwalimu/ mlezi, ilipaswa kuwe na uchanganuzi wa hali ya juu/ intensive vetting ili mtu kupatiwa jukumu hili, huku mlezi huyu akitengenezewa mazingira mwanana yakumpa utulivu kuweza kulitenda jukumu lake bila ya kuwa na hali ya kuchanganyikiwa. Hivi mara ngapi tunashuhudia kwa waliokosa fursa ya kazi wanazozipenda hujiunga na ualimu ili tu wasikae bure katika nchi yenye ufinyu wa fursa za ajira?
Wapo walimu wangapi ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu ikiwemo kutembea masafa marefu bila ya uhakika wa usafiri, uhaba wa vifaa vya kufundishia, idadi kubwa ya wanafunzi katika darasa sambamba na uduni wa mshahara usioweza kukidhi hata kula yake ya mwezi, seuze mahitaji ya ziada, wengine wakiandamwa na makato makubwa ya mikopo ya masomo na mikopo nk. Hivi, mwalimu wa aina hii aliyezongwa kimawazo na kuchanganyikiwa kama hivi tunatarajia nini akipewa jukumu la kuwaadhibu wanafunzi kwa viboko? Baadhi ya wazee wasiokuwa na uoni wa mbali wamefurahia katazo hili mashuleni bila ya kuzingatia kuwa huo ni mtego tu, ambao shule ni eneo la kuanzia tu, baada ya kutengeza uelewa sawasawa na kumakinishwa wanafunzi dhidi ya adhabu ya bakora, katazo hilo litapelekwa majumbani rasmi, na wazee kamwe hawatakua na fursa tena ya kuwakanya na kuwaongoza watoto wao.
Kitu cha kuzingatia ni kuwa katika nchi za magharibi ambapo bakora haitumiki tunakuta ndizo zinazoongoza katika mporomoko wa kutisha kimaadili zikilinganishwa na nchi changa zikiwemo nchi za Waislamu. Nchi za magharibi ndizo zinazoongoza katika ubakaji, ulawiti, utoaji wa mimba kwa wasichana wa umri mdogo, ubaradhuli, ushoga, usagaji nk.
Amma nukta (b) ya kuweka adhabu mbadala wa viboko, hilo nalo limekuwa janga, kwa sababu msingi wa mamabo ni urukaji mipaka katika kuadhibu, na hili hujiri hata ikiwa kuna adhabu mbadala. Imekuwa jambo la kawaida kumkuta mtoto wa darasa la pili amebebeshwa ndoo ya maji anasafisha choo huku akiwa hana hata ndara miguuni eti anatumikia adhabu mbadala bila ya kujali afya yake na kusibiwa na maradhi ya mripuko. Tahamaki wanafunzi watapewa adhabu wanazostahiki wafungwa magerezani kwa kisingizio cha adhabu mbadala. Suala msingi hapa ni urukaji mipaka katika kuadhibu, kitu ambacho vyanzo vyake havijakabiliwa vilivyo.
Iwe bayana pia kuwa tunapozungumzia kuadhibu kwa bakora ni kiasi cha kumuadabisha tu mwanafunzi na wala si kumpiga kama kiwango cha adhabu ya mhalifu. Hivyo, mwalimu, mzazi na mlezi hodari hujua busara ya matumizi ya bakora/ viboko kwa watoto kulingana na umri, kosa nk. na kamwe haitakua hujuma ya kumuangamiza.
Katika Uislamu licha ya kuwa dola ya Khilafah ni mchunga wa moja kwa moja kwa jamii, lakini pia umelifanya suala la malezi ni dhima kubwa kwa wazazi na walezi kwa jumla akiwemo mwalimu. Kwa dhima hii itabidi wahusika watakuwa ni wenye kuwajibika kwa Muumba kwa namna walivyobeba uchunga wao. Kama alivyosema
Mtume SAAW:
“Kila mmoja wenu ni mchunga, na kila mchunga ataulizwa juu ya uchunga wake”
Kwa msingi huo, Uislamu umempa mlezi mamlaka bila ya kuruka mipaka kutumia bakora/ viboko kama ala, chombo na mbinu nzuri katika kuadabisha na kumnyoosha mtoto katika mchakato wa malezi.
Imepokewa kutoka kwa Abu Thuraiyah Sabrah bin Ma’bad Al-Juhani (R.A) kuwa Mtume SAW amesema :
: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم
«مُرُوا أولادَكم بالصلاةِ وهم أَبْنَاءُ سَبْعِ سِنِينَ، واضْرِبُوهُمْ عليها، وهم أَبْنَاءُ عَشْرٍ، وفَرِّقُوا بَيْنَهُمْ في المَضَاجِعِ»
‘‘Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapofika umri wa miaka saba, na wachapeni wanapofika miaka kumi (wakikataa kuswali) na watengeni katika vitanda vya kulalia”
(Abu Dawud na Tirmidhi).
Yassin Thabit
Risala ya Wiki No. 151
12 Rajab 1444 Hijri / 03 Februari 2023 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.