Nafasi Ya Baba Katika Familia Ya Kiislamu

بسم الله الرحمن الرحيم

Ubaba ni jukumu muhimu sana na la msingi katika Uislamu, ni msingi wa utambulisho kwa Waislamu wote, Allah(swt) anasema:

ادْعُوهُمْ ِلأَبَائِهِمْ هُوَ أَقْسَطُ عِنْدَ اللَّهِ ِ

“Waiteni (watoto) kwa ubini wa baba zao, maana huo ndiyo uadilifu mbele ya Allah” (Al Ahzab 33:5)

Kuwa baba kunatengeneza msingi wa majukumu kwa watoto wako kama vile kuwa muadilifu kwao, kuwa karibu nao, kuwapa huduma za kifedha, kuwapa thaqafah ya Kiislamu, kuwafundisha misingi ya imani yao, kuwafundisha adabu, tabia njema nk. Hakika kazi ya baba ni zaidi ya kutoa majina kwa watoto wake wa kike na watoto wa kiume.

Ubepari huzingatia kizazi chema kwa kumjenga mtoto kwa kumjaza mtoto elimu ya madania, fikra na thaqafah ya kimagharibi ili aweze kuyamudu maisha na kujikusanyia mali kwa hali yoyote ile, hii ni kutokana na kuitikia miito ya kibepari eti kuwa elimu ndio huleta riziki.

Hivyo, huwa msingi wa malezi katika ubepari ni elimu itakayompa mtoto maisha mazuri hata kama atamsahau Muumba wake katika nyanja zote za maisha. Kwahiyo zikatungwa sheria na kanuni mbalimbali kandamizi kwa baba ili kumuwezesha mtoto kufikia lengo la kupata maisha mazuri. Baya zaidi sera na sheria hizo zinalenga kumtenganisha mtoto na wazazi na badala yake kulelewa na vituo maaalum (shule) ili kuweza kupata elimu na tija yake ni baba kukosa kabisa udhibiti kwa mtoto.

Vita dhidi ya kudhoofisha nafasi ya ubaba imekuwa kubwa, umefanywa muda wa malezi kwa mtoto ni miaka 18 na baada ya hapo mtoto huwa huru kujiamulia katika maisha yake asiwe na haja ya kupata muongozo wa baba. Uvamizi huu katika thaqafah ya Kiislamu umepelekea jamii ya Kiislamu kuzidiwa na ufisidifu na hivyo kushindwa kumudu nguvu za ufisadi.

Ifahamike kuwa mfumo huathiri jamii, jamii nayo ndiyo inaathiri mtu binafsi. Hivyo, juhudi kubwa zinazoonekana kumpokonya baba nafasi yake ni kutokana na mfumo ambao ndiyo umepelekea familia kuongozwa na wanawake kama athari ya haki sawa kati ya mama na baba katika familia, akina baba kushughulishwa na kutafuta kiasi cha kushindwa kuzipa malezi familia zao.

Kutengemaa kwa baba kunategemea sana kutengemaa kwa jamii na zaidi kuwepo kwa mfumo thabiti unaoweza kumpa kila mtu haki yake katika familia, yaani baba, mama na mtoto. Mfumo fisidifu wa ubepari umeonesha kushindwa kwa hali ya juu katika hili kwani kila muda unavyozidi kusonga mbele katika ndiyo uharibifu mkubwa unavyozidi kutokea kama tulivyoona hapo awali.

Ubepari pia huzingatia kuwa nafasi ya baba ni kumpa mtoto maadili ya kizalendo na kumjenga kuwa muovu dhidi ya taifa lingine kwa kipimo cha eti kuipenda nchi yake, na tija yake huwa ni kumtengenezea ubaguzi na chuki ambayo inagharimu maelfu ya maisha ya wanadamu leo hii.

Uislamu kwa upande wake unamtazama baba kuwa ndiyo kioo cha jamii na unampa jukumu la ulezi na usimamizi wa familia ili kuijenga familia yake katika misingi bora ya Uislamu kwa kuhakikisha fikra na nafsia ya Kiislamu zinakita kwa familia yake ili kupata radhi za Muumba wake, kwani shabaha hasa siyo tu kupata maslahi kutokana na mtoto au mtoto kupata maslahi ya kimada pekee kutoka kwa baba.

Mtume wa Allah (saw) alifananisha mafundisho yake kwa Ummah kama mafundisho ya baba kwa familia yake, akasema: “Hakika mimi ni kama baba kwenu, kwa jinsi ninavyowafundisha” (Sunan Abu Dawd)

Mtume wetu Muḥammad (saw) alilea kizazi chote cha wanawake na wanaume, akaweka misingi ya dini ambayo imeendelea kuwa dira ya Ummah mpaka leo. Alikuza na kulea watoto wake wanne wa kike ambao wamekuwa mfano kwa Ummah huu kwa muda wote. Alimlea Ali Ibn Abi Twalib (ra) Khalifah wa nne wa Waislamu, aliyekuwa mtoto wa baba yake mdogo aliyekuwa masikini. Alimlea Zayd Ibn Haritha (ra) na mwanaye Ussama (ra) kwa wema, na alikuwa kwa masahaba wake na vijana mwalimu bora mwenye subra Mtume (saw) aliwafundisha thaqafah vijana wa Kiislamu, akawawekea mapenzi na imani yao na akawafundisha kupendana, adabu na utii.

Ni waumini hawa wanaume na waumini hawa wanawake waliolelewa na Mtume SAAW ndiyo walioweka utawala kwa yale aliyoteremsha Allah SWT na baada ya kuondoka Mtume SAAW wakaendeleza utawala huo kwa kutandika dola ya Khilafah kwa njia ya Mtume kama zao la mafundisho ya Mtume (saw).

Masahaba walikuwa mababa wawajibikaji wakikabili majukumu tofauti tofauti kwa umakini, mfano ukamanda wa majeshi, kuwa waume bora kwa wake zao, majirani wema,n.k

Baba katika Uislamu ni rafiki ni mwalimu, mshauri na muadabishaji kwa watoto wake. Mtume(saw) alikuwa mpole, mwenye heshima katika kuwalea watoto wake wote.

Anasimulia Aisha(ra), Mama wa Waumini:

“Sijaona yeyote anayefanana na Mtume katika maneno, na adabu kama Fatima(ra), pindi Mtume alipomuona akija kumtembelea alisimama, akambusu, akamshika mkono wake na kumkalisha mahali alipokuwa amekaa yeye. Na pindi Mtume alipomtembelea alimsalimia, akasimama na kumbusu”(Al Adab Al Mufrad)

Pia Abu Huraira anasimulia kuwa; Al Aqra’ Bin Habis alimuona Mtume(saw) akimbusu Hassan. Akasema “nina watoto kumi na sijawahi kumbusu yeyote kati yao, Mtume akasema: “asiyewahurumia watoto, na yeye hatahurumiwa (Muslim),

Baba katika Uislamu, anapaswa kuwapenda na kuwajali watoto wote bila kubagua wala kupendelea baadhi yao.

An-Nu’man bin Bashir (ra) anasimulia ” baba yangu alinichukua mpaka kwa Mtume ili Mtume awe shahidi wa kitu alichonipa, Mtume akamuuliza: una watoto wengine? Akajibu: ndiyo. Kisha Mtume akamuuliza: kwanini huwalei kwa usawa? (An Nasai)

Baba wa Kiislamu anapaswa kuwahurumia watoto na kujua mahitaji yao kama watoto. Anapaswa kuwa kama mtoto anapokuwa na watoto na kuwa mwanaume jasiri inapohitajika. Ubaba wa mwanaume wa Kiislamu utokane na uimara wake katika ufahamu wa dini na utekelezaji wake. Pia baba mchamungu wa Kiislamu anapaswa kubadili marafiki waovu na kuwa na marafiki wema kwani anasema Mtume(saw):

“Mtu hufuata mwenendo wa rafiki yake, basi na aangalie mmoja wenu nani wa kumfanya rafiki(Abu Dawud)

Kimsingi kila tukitaka kutazama namna nzuri ya kuwa baba katika jamii yetu basi ni lazima tutamgeukia na kumuangalia Mtume SAAW kama kiigizo chetu kwa ajili ya kulinda dunia yetu na akhera yetu kama akina baba.

Kwahiyo, akina baba wa leo wafikirie na wabebe kwa makini majukumu yao mbele ya Allah SWT kuhusu watoto wao, katika kipindi hiki cha mpito chenye changamoto nyingi ambacho Ummah unajiandaa kushuhudia bishara njema ya Mtume ( saw) ya kurejea kwa Khilafah ikikamilika.

Waandae akina baba wa Kiislamu kutoka katika nyumba zao vijana madhubuti watakaokuja kubeba majukumu ya Uislamu ipasavyo kwa ulimwengu mzima.

 

Risala ya Wiki No. 124

17 Jumada al-Thani 1443 Hijri / 20 Januari 2022 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania

http://hizb.or.tz/

Maoni hayajaruhusiwa.