Unafiki Wa Wazi Katika Kukabiliana Na Kesi Za Ugaidi

بسم الله الرحمن الرحيم

Habari:
Mnamo Agosti 06, 2021 Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu ilitaja kesi inayomkabili kiongozi wa chama kikuuu cha upinzani (Chadema) Freeman Mbowe, anaekabiliwa na mashtaka mawili, la kula njama ya kutenda uhalifu, na la kudhamini ugaidi, wakati watuhumiwa wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba.

Maoni:
Freeman Mbowe alitekwa katika tukio la uvamizi wa usiku wa manane mnamo tarehe 21/07/2021 yeye, viongozi wengine na wanachama wenzake 11 jijini Mwanza wakiwa katika hekaheka za kushiriki kongamano lililopangwa la kudai katiba mpya. Na baada ya wiki mbili alishtakiwa kwa makosa ya ugaidi na kula njama ya kutenda uhalifu.

Tukio hilo lililaniwa kila upande na kupazwa sauti ya kulipinga kutoka kwa wanaharakati na taasisi za kutetea haki za binadamu, ambapo Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International liliitaka serikali ya Tanzania kuacha kamata kamata na manyanyaso kwa wanachama wa upinzani na viongozi wao, na kusisitiza kwa serikali kuwaachia huru mara moja, isipokuwa tu kama wana vigezo bayana vya kisheria kuhalalisha ukamataji wao.

Wakati tukiungana (na wahanga) katika hali ya machungu na matendo yasiyo ya kibinadamu na kutoa mkono wa faraja kwa Mbowe pamoja na wahanga wengine wote wa vitendo vya kamata kamata. Tungependa pia kuangazia uwepo wa hali ya undumilakuwili kwa namna zinavyokabiliwa kesi za ugaidi, kama inavyodhihirika wazi katika tukio hili.

Siku ya Alkhamis tarehe 22, 2021, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema wazi kuwa uchunguzi na upelelezi wa kesi ya Mbowe umekamilika kwa kutamka:
“Mbowe alikuwa anajua kuwa tuhuma dhidi yake kuwa zilikuwa zinachunguzwa, na kwamba angehitajika na Polisi kwa ajili ya hatua za kisheria pindi tu upelelezi utapokamilika. Tayari sasa tumeshafikia hatua hiyo”

Katika kadhia hii (kesi ya Mbowe) suala la uharakishwaji wa upelelezi na ukusanyaji ushahidi linaonekana kuzingatiwa vyema, na mtuhumiwa alifikishwa mahakamani pindi tu upelelezi ulipokamilika. Ilhali hali hii ni tofauti kabisa kwa kesi za aina hiyo hiyo zinazowahusu mahabusu Waislamu wenye tuhuma za ugaidi nchini Tanzania.

Kuna mamia ya watuhumiwa wa ugaidi katika magereza mengi katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga pamoja na Mtwara ambako wanaharakati watatu wa Hizb ut Tahrir/Tanzania; Ustadh Ramadhan Moshi Kakoso, Omar Salum Bumbo na Waziri Mkaliaganda wamekuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kubambikizwa za ugaidi kwa miaka 4 kwa kisingizio cha uonevu na dhulma cha ‘upelelezi bado unaendelea’. Jambo hili linatupa taswira ya wazi kwamba katika ufuatiliaji wa watuhumiwa wa ugaidi, kundi moja linaweza kukamatwa kwanza, kisha upelelezi ukafuatia, na kundi lingine linaweza kukamilishiwa upelelezi kwanza, kisha ndio ukamataji ukafuatia.

Kufuatia ukamatwaji wa sasa wa Mbowe, jeshi la polisi limethibitisha kuwa limempeleka mahakamani kwa sababu upelelezi wa tuhuma za ugaidi dhidi yake umeshakamilika, na kuwa walilazimika kumuachia huru mwezi Novemba mwaka jana kutokana na kutokukamilika kwa upelelezi.

Jambo hili ni zaidi ya uonevu, kwani Mbowe alikamatwa mara tu baada ya upelelezi kukamilika, ilhali serikali hiyo hiyo kwa miaka mingi imekataa kuwaachia kwa dhamana mahabusu Waislamu wanaoshikiliwa kizuizini kwa makosa kama hayo, tena kwa kushindwa wao serikali kuleta walau tembe ya ushahidi dhidi yao.
Kuna sababu kuu mbili ambazo kwa kiasi kikubwa zinaweza kuwa zimepelekea kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi kwa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani:

Kwanza, ni sababu za kisiasa za kutaka kunyamazisha na kujaza khofu kwa vuguvugu linaloendelea la kutaka katiba mpya, ambalo kwa kiasi kikubwa linaongozwa na chama kikuu cha upinzani kwa mashirikiano na wanaharakati binafsi na taasisi za kidemokrasia za ndani, kikanda na kimataifa.

Pili, jaribio hili lililoshindwa la aibu linalenga kuwalaghai Waislamu na kupoza mambo kwa kutaka kuonesha kuwa Waislamu siyo wahanga pekee wa sheria kandamizi za ugaidi, likilenga jaribio hili kutaka kuwaaminisha (Waislamu) kuwa hata wasiokuwa Waislamu na viongozi wa upinzani wanaweza kushtakiwa kwa makosa kama hayo. Hata hivyo, uhalisia wake ni kinyume chake, sasa imeshakuwa wazi zaidi kuwa walengwa wakuu wa sheria hizi ni Waislamu.
Ikumbukwe kuwa kiongozi huyu huyu wa upinzani na wanachama wenzake walikamatwa kabla tarehe 02/11/2020 wakituhumiwa kwa ugaidi lakini waliachiwa huru.

Kufuatia kukamatwa kwa Mbowe sasa, polisi imethibitisha kuwa imempeleka mahakamani kwa sababu upelelezi wa tuhuma za ugaidi dhidi yake ulikuwa umekamilika na kuwa walilazimika kumuachia mwezi Novemba mwaka jana kutokana na kutokukamilika kwa upelelezi.

Tukio hili wazi wazi limefunua unafiki, sura mbili na uonevu wa mamlaka inayohusika na utoaji wa haki nchini Tanzania. Ni muda muwafaka sasa mamlaka hiyo kujizatiti zaidi kwa kushikamana vyema na taratibu za uendeshaji kesi, kwa kuwasilisha ushahidi mahakamani dhidi ya mahabusu wote wa tuhuma za ugaidi kama walau wanao, wawaachie huru kwa dhamana, au wawaachie huru mara moja.

Imeandikwa kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Said Bitomwa
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.