Maumivu Na Uonevu Wa Kinachoitwa Mapambano Dhidi Ya Ugaidi
Siku ya Ijumaa ya tarehe 25 Juni 2021, Masjid Rahma, Buguruni mara baada ya Swala ya Ijumaa, Ustadh Abu Ayman (kwenye picha) ambaye ni mwalimu wa Madrasat Imaniya iliyopo jirani na msikiti huo, pia akiwa miongoni mwa maimamu wasaidizi msikitini hapo aliongea mazito kuhusiana na uonevu wa kinachoitwa mapambano dhidi ya ugaidi na sheria yake.
Ustadh Abu Ayman akizungumza na Waumini siku hiyo mara baada ya Swala ya Ijumaa alisema, ilimlazimu kutoa dukuduku lake baada ya kuona kwa wiki kadhaa khutba za Ijumaa na bayan za msikitini hapo zimekuwa zikiongelea suala zima la dhulma za waziwazi, maonevu na mateso ya kinachoitwa mapambano ya ugaidi na sheria yake thaqili na ya kibaguzi
Ustadh Abu Ayman akizungumza na Waislamu kwa uchungu mkubwa msikitini hapo, aliwambia waswalihina kuwa, mnapowaona makhatibu na wazungumzaji mbalimbali hapa wanaongelea kwa hisia na maumivu makali mada ya vita dhidi ya ugaidi na sheria yake, jueni kuwa wanachosema ni kweli na muwaelewe kwa udhati wake, kwa kuwa masaibu wanayoyasema yanatukuta na kutugusa wengi.
Aliendelea na nasaha zake Abu Ayman kwa kutolea mfano wa kilichomkuta mdogo wake aliyekamatwa mwaka 2018 wilayani Kahama kwa uonevu wa kisingizio cha ugaidi.
Abu Ayman alielezea kuwa, ndugu yake huyo ambaye alikuwa mwalimu wa dini ya Kiislamu huko Kahama alikuwa akitoka nyumbani alikopanga mapema kwenda msikitini, kisha kwenye shughuli zake, na kurudi nyumbani muda mwingi, kwa sababu ya shughuli zake za kimaisha na kusomesha dini maeneo kadhaa.
Mwenye nyumba aliyopanga akenda kumripoti ndugu yake Abu Ayman kwa vyombo vya dola kwamba ni gaidi, kwa hoja kwamba anatoka alfajiri mapema, anachelewa kurudi, anaongea kiarabu kwenye mawasiliano ya simu na pia haonekani kuchanganyika na wapangaji wengine (wakiwemo wapangaji wa kike).
Abu Ayman aliendelea kueleza kwamba, baada ya mwenye nyumba kwenda kupeleka ripoti kwa kuambatanisha madai na hoja zake hizo, vyombo husika vikamfuata mdogo wake huyo alfajiri mapema wakati akitoka, kumtia nguvuni na kumuweka mahabusu kwa tuhuma za ugaidi.
Ustadh huyo (ndugu wa Abu Ayman) akawekwa mahabusu kwa dhulma na uonevu kwa miezi 7. Baadae akaachiwa huru bila ya hatia yoyote, baada ya jamaa yao mwanajeshi kuingilia kati na kumfuatilia usiku na mchana.
Huo ni mfano mmoja kati ya mingi inayodhihirisha bayana uonevu, dhulma na ukandamizaji kwa mgongo wa kupambana na ugaidi na sheria yake ya kibaguzi na ya kishenzi ya ugaidi.
Aidha, tujiulize kuna watuhumiwa wangapi wa ugaidi mfano wa mdogo wake Abu Ayman ambao amma walishikiliwa au bado wanaendelea kushikiliwa bila ya hatia, kesi zao hazisikilizwi na wakiwa hawana mtu mwenye ushawishi kuwapigania uhuru wao?
Tunaposema sheria ya ugaidi ni sheria ya kibaguzi na haipaswi kuwepo kwa mifano kama hii ni mwenye chuki au mtu duni ndio hatotuelewa. Ustadh huyu amewekwa mahabusu kwa miezi 7, kwa sababu tu anatoka nyumbani mapema, kuchelewa kurudi, kuvaa kanzu, kuongea kiarabu na kutojihusisha na uchafu wa kuchanganyika na wapangaji hususan wanawake. Kana kwamba hayo aliyokuwa akiyafanya ni jinai katika nchi hii. Lakini tafsiri inayopatikana hapa ni kuwa kwa Muislamu kutenda hayo ni jinai, na ndio maana akapewa adhabu ya kuwa kuzuizini katika mazingira duni kwa miezi 7.
Ikiwa vigezo duni na dhaifu kama kuongea kiarabu, kuvaa kanzu, kwenda msikitini alfajiri nk. ndio vinavyosukuma ukamataji wa wengi wa watuhumiwa wa ugaidi, ni wazi kesi za ugaidi hazitoweza kukosa milele kisingizio maarufu cha ‘ushahidi kutokamilika’ kwa miaka. Kwa sababu kuanzia ukamataji wa watuhumiwa huwa kumekosekana mashiko na uthabiti wa kesi, na hivyo wasimamizi wa kesi za aina hii huchelea aibu, fedheha na idhilali kiasi cha kushindwa hata kuruhusu uendeshaji wake, lakini kwa kisingizio cha kutokamilika ushahidi.
Kwa upande mwengine, hatupingi kwamba ajenda ya mapambano dhidi ya ugaidi na sheria yake ni ajenda ya nje kutoka madola ya kibeberu hususan Marekani ambayo wamelazimisha kwa mabavu nchi changa ikiwemo Tanzania. Katika hali hiyo ilipaswa tuziulize nchi changa ikiwemo Tanzania zinazotenzwa nguvu kwa ajenda hii ya kikoloni, jee mabeberu kwa maumbile yao wanapolazimisha ajenda yao kwa watu au nchi fulani, kweli huwa wana nia njema kwao?
Swala hili likipata jibu sahihi hapo ndipo nchi changa ikiwemo Tanzania zitakapotanabahi na kuwa na hadhari kubwa juu ya ajenda hii ya hatari yenye kujenga chuki na kuleta maumivu makubwa ndani ya jamii kwa kulilenga na kulinasibisha zaidi kundi moja na ugaidi.
Japo kwamba lazima tukiri upo uwezekano wa kuwepo baadhi ya Waislamu wanaojihusisha na vitendo vya ugaidi, lakini pia upo uwezekano wa kuwapo pia watu wa dini nyengine katika vitendo hivyo. Kwa kuwa ubaya na uovu hauna dini, taifa wala kabila.
Ajenda ya mapambano ya ugaidi imeleta maumivu makubwa, lakini maumivu hayo yataendelea kuwa makubwa zaidi na zaidi lau hatua za kutibu na kuyaondoa hazikuchukuliwa kwa haraka.
Ni muda muwafaka sasa kwa vyombo vinavyosimamia haki kuacha kubeba dhana ya ‘kutokamilika ushahidi kwa miaka, dhana iliyogubikwa na dhulma na uonevu wa wazi. Wajibu unaohitajika kwa haraka ni kuwaachia huru watuhumiwa wote wa kesi za ugaidi au vyombo hivyo kujiamini kwa kuanza mara moja kusikiliza kesi zote za aina hiyo.
تَتَّخِذُونَ أَيْمَانَكُمْ دَخَلاً بَيْنَكُمْ أَنْ تَكُونَ أُمَّةٌ هِيَ أَرْبَى مِنْ أُمَّةٍ
“Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa tu, kundi moja lina nguvu zaidi kuliko kundi jingine”? (TMQ 16: 92)
Risala ya Wiki No. 105
18 Dhu al-Qi’dah 1442 Hijri / 29 June 2019 Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.