Kukosekana Kwa Amani Duniani: Ubepari Ndiyo Chanzo
بسم الله الرحمن الرحيم
Tarehe 20, Septemba ya kila mwaka huadhimishwa kuwa Siku ya Amani Duniani. Mabepari baada ya kushindwa kuleta amani, usalama, utulivu na ustawi wa ulimwengu wakabuni siku ya kuwarubuni watu kuhusu suala la amani ya ulimwengu, huku wao wakiwa ndiyo chanzo na wahusika wakubwa wa upotevu wake.
Mfumo wa kibepari ulianza takriban kuanzia karne ya 12 CE hivi ukitokamana na mfumo wa kiujima (feudalism) katika Ulaya ya Magharibi, hii ilisababishwa na maendeleo ya uvumbuzi wa mashine mbalimbali. Uliendelea kukua mfumo huo ukitumia ukoloni kama mbinu yake kuu ya kufikia malengo yake ambayo ni unyonyaji.
Ubepari unaamini katika kutenganisha dini na maisha (usekula) na kipimo cha maslahi. Mambo mawili hayo ndio huzingatiwa katika nidhamu zake zote za kimaisha iwe siasa, jamii, uchumi nk. Wakaathirika mabepari na mitazamo hiyo na wakasonga mbele katika kuifanyia kazi na hatimaye kwa fikra hizo wakakoloni dunia nzima katika karne ya 19 CE
Kwavile lengo la ubepari na mabepari ni maslahi, kwa kupitia unyonyaji na ukoloni wameleta madhara makubwa yasiyomithilika katika uso wa ulimwengu, na kubwa zaidi ni la ukosefu wa amani.
Tangu uvamizi na uporaji wao ulipoanza sehemu mbali mbali, matokeo yake ulipingwa na watu wote duniani. Kupitia biashara ya utumwa pekee waliyofanya kuanzia karne ya 15 CE, zaidi ya watu milioni 180 waliuawa wengi wao wakitokea Afrika.
Si hayo tu bali ubepari kwa kupitia ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo umeleta na unaendelea kuleta vita na machafuko mengi duniani. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 19 CE na mwanzoni mwa karne ya 20 CE dunia imeshuhudia vita zaidi ya 1200 na machafuko makubwa yasiyohesabika yaliyogharimu maisha, rasilmali watu na vitu.
Vingi katika vita hivi ikiwa ni vya kupinga ukoloni na vita vya kimaslahi ya wakoloni kama ilivyokuwa Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya ulimwengu kati ya miaka ya 1914 mpaka 1918 na 1939 mpaka 1945.
Taarifa zinasema tangu mwaka 1900 vita ndani ya ulimwengu zimesababisha vifo vya watu zaidi milioni 187. Hii ni zaidi ya mara tatu ya watu wote wa nchi kama Tanzania, kwa sasa, na bado wanaendelea kusabibisha vita zaidi. Hii leo kama inavyoonekana maeneo mbalimbali ulimwenguni kama Iraq, Afghan, Yemen, Libya, Palestina, Somalia, Congo nk.
Ubepari hauwezi kamwe kuleta amani duniani, kwani ni mfumo wa kinyonyaji na ni maumbile ya mwanadamu anaponyonywa kupinga unyonyaji husika. Hivyo, mabepari kwa kuwa hunyonya walimwengu, na watu dunia nzima hupinga unyonyaji wao, na hii ndiyo sababu kubwa inyoleta vita, vurugu, machafuko, mauaji , na kukosekana kwa amani ya ulimwengu kiujumla.
Kwa msingi huo, ni ndoto na ni kukosa maarifa kwa mtu kuwaza na kudai kuwa chini ya mfumo huu wa kibepari kuna siku dunia itakuwa na amani, haijawahi kutokea, haitokei, na haitatokea kamwe mpaka pale ubepari na mabepari wakoloni watakapokuwa wamedhibitiwa.
Ubepari ulistawi baada ya Waislamu kuacha kutabikisha Uislamu wao kivitendo na hatimaye kupelekea kuanguka kwa dola ya Kiislamu duniani (Khilafah), kuanzia hapo ulimwengu ukaanza kukosa mlinzi wa amani yake na amani ya ulimwengu kwa jumla.
Hivyo, ili kurejesha tena amani ya kweli ya ulimwengu tunapaswa kurejesha tena serikali ya kiulimwengu ya Kiislamu (Khilafah) ambayo itasimamia haki, amani, na uadilifu katika dunia hii kwa Waislamu na walimwengu kwa jumla.
Said Bitomwa
Risala ya Wiki No. 88
0 8 Safar 1442 / 25 Septemba 2020 Miladi
Maoni hayajaruhusiwa.