Mikopo ya Riba Inavyoangamiza Mataifa Machanga

Punde baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya ulimwengu, ulimwengu ulipita katika hali tete ya kiuchumi ijulikana kama Economic Depression iliyodumu kuanzia mwaka 1929-1933.Baada ya hali hii ambayo iliyaathiri mataifa ya Ulaya yaliyokuwa vinara katika vita vya ulimwengu kama vile Uingereza, Ujerumani, Ufaransa nk.

Kutokana na hali hiyo iliyodhoofisha uchumi wa Ulimwengu kiujumla ilipelekea kuongezeka kwa mwamko mkubwa ndani ya bara la Afrika kudai uhuru na kujikomboa kutoka hali ya ukoloni mkongwe. Ikumbukwe kabla ya vita vya ulimwengu mataifa yaliyokuwa yakikoloni hasa bara la Afrika yalikumbana na upinzani mkubwa katika makoloni yao.

Kwa upande wa Tanganyika wajerumani walikumbana na upinzani mkubwa wa mara kwa mara (Active Resistance) hasa maeneno ya kusini mwa Tanganyika ambapo kulishuhudiwa mapigano makali yaliyojulikana kama Vita vya Majimaji bila kusahau mapambano dhidi ya Mtemi Mkwawa huko iringa. Kwa upande wa Kenya nako kulishuhudiwa mapigano makali hasa vita vya Maumau dhidi ya ukoloni wa kiingereza bila kusahau Vita ya Chimulenga iliyokuwa Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe) na sehemu nyingine za bara la Afrika.

Hivyo, baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vuguvugu la kudai uhuru (nationalism) na kujikomboa kutokana na ukoloni mkongwe lilishika kasi, hali hii ilipelekea mataifa ya kigeni kuweka misingi mipya hasa ya kithaqafa/ kifikra ili kuhakikisha athari ya ukoloni wao inabaki kwa sura mpya ya ukoloni mamboleo (neo colonialism).

Wakoloni walihakikisha kuwa mwelekeo wa kudai uhuru unafuata njia ambayo wao wameichora na hapa wakaandaa thaqafa maalumu (colonial education) lengo lake likiwa ni kuwaandaa hasa wapigania uhuru kutabanni/ kushikilia misimamo ya mitazamo na fikra za kikoloni zitakazowaongoza katika kuyaangalia mambo, iwe upande wa kiuchumi, kisiasa au wa kijamii.

Mara baada ya kupata uhuru mataifa ya Afrika na matafaifa machanga kwa jumla yalijikuta yanaingia katika mtego wa mikopo ya riba kutoka Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Thaqafa/ mtizamo wa kifikra wa kikoloni uliacha athari mpaka leo katika mataifa haya machanga kiasi kwamba katika upande wa kiuchumi mataifa hufuata mwelekeo ule uliochorwa na wakoloni, hata imekuwa sio aibu tena bali ni fakhari kuchukua mikopo ya riba kubwa.

Mataifa haya ya ulimwengu wa tatu pindi wanapozungumzia kujikomboa kiuchumi utawakuta wananadi sera zenye kumakinisha ukoloni kama vile uwekezaji, ubinafsishaji, soko huru, mikopo ya riba nk. Huku mataifa haya ya nchi changa ni wanachama wa mashirika ya kikoloni kama vile IMF WTO nk yaliyoanzishwa kwa ajili ya kunyonya mataifa machanga na kulinda maslahi ya mataifa makubwa. Sera za mashirikia haya ya kinyonyaji ziko wazi kiasi kwamba Katika hali tete kama hii mataifa machanga hujikuta yamenasa katika mtego wa kikoloni.

Kutokana na mzigo wa mikopo ya riba ndani ya bara Afrika, kumepelekea mdororo wa kiuchumi kwa wananchi wake, kutokana na sehemu kubwa ya makusanyo ya kodi kutumika kulipa riba ya mikopo jambo ambalo limepelekea kuzorota kwa upatikani wa huduma za kijamii kama vile hospitali mashule nk.

Katika taarifa ya Fitch Solution Report iliyotolewa Disemba mwaka 2019 inaonyesha kuwa nchi za Afrika Mashariki zitatumia zaidi ya asilimia 40 ya mapato yake kwa ajili la kulipa madeni, huku Shirika la Fedha duniani (IMF) likionya ongezeko kubwa la deni katika nchi hizo, linaweza kuwa sio himilivu. Pia wachambuzi katika masuala ya uchumi kutoka taasisi ya ya Institute of Chartered Accountants ya Uingereza na Wales ilitabiri kuwa mwaka 2020 kutashuhudiwa ongezeko la deni kwa asilimia 6.1% ikilinganishwa na asilimia 6.3% ya mwaka 2019.

Aidha taarifa hiyo inaonyesha kuwa deni la nje la Kenya limefikia dola bilioni 58.1, Tanzania dola bilioni 22.5, Uganda dola bilioni 12, Rwanda dola bilioni 5.4. Huku ukanda wote wa Afrika Mashariki katika kukuza uchumi wake unategemea sekta za kilimo, utalii, ujenzi miundombinu na usafirishaji, sekta ambazo hazijafanya vizuri.(The Citizen Jan 7 2020).

Bila shaka ongezeko hilo la deni katika ukanda huu na ukuaji mdogo wa uchumi katika bara la Afrika ni kutokana na sera ya mikopo ya riba inayotumiwa na mataifa makubwa hasa Marekani, mataifa ya Ulaya na China ili kuendelea kuzinyonya nchi changa.

Karibuni tumeshuhudia tishio kutoka China kwa nchi ya Kenya ambayo ilikopa mkopo wa zaidi ya dola bilioni 5 kwa ajili ya mradi wake wa reli ya kisasa (Standard Gauge) ambayo tayari uendeshaji wake umekuwa wa kusuasua. China imetishia kuichukua bandari ya Mombasa ikiwa deni lake halitolipwa kwa muda uliowekwa.

Mkaguzi mkuu wa Hesabu wa Kenya bwana FT Kimani kwenye ripoti yake ya mwaka 2019 alisema mradi wa reli ya kisasa nchini Kenya ulikuwa unaipendelea Benki ya China (Exim Bank) kutokana na kuweka riba kubwa inayokuwa kila mwaka. Aidha Dr FT Kimani alidokeza kuwa kutokana na mkataba ulivyo, mapato yanayopatikana katika mradi huo yatakuwa yanawekwa kwenye akaunti (maalum) ambayo itakuwa inasimamiwa na mtu wa tatu ambaye hajulikani kwa niaba ya Benki ya Exim ya China na Shirika la Reli la Kenya (KRC). Hivyo, ikiwa China itaichukua bandari ya Mombasa, Kenya itaungana na nchi nyingine duniani zilizoathirika na mikopo ya riba kubwa inayongezeka kila mwaka (compound Interest), kama Sri Lanka ambayo Disemba mwaka 2017 ilipoteza bandari yake Hambantota itakayomilikiwa mapato yake na China kwa miaka 99 baada ya kushindwa kulipa deni lake, pia nchi ya Zambia nayo Septemba 2018, ilipoteza kiwanja chake cha ndege cha Kenneth Kaunda International Airport kama Sri Lanka.

Bila shaka mikopo hii ya riba hasa kwa nchi changa ni mwendelezo wa ukoloni mamboleo wenye lengo la kupora rasilimali zao kiujanja kwa kisingizio cha kuweka dhamana kutokana na madeni yasiyolipika.

Bara la Afrika licha ya utajiri mkubwa ulionao kama vile gesi, ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo, bahari na nk. bado raia wake wanaishi maisha magumu kutokana na sera katili za kikoloni zilizomakinishwa ili kundeleza ukoloni. Bila ya kupepesa macho aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa IMF Christine Lagarde wakati akijiuzulu nafasi yake tarehe 12 Septemba 2019 alisema (hata vita vinavoendelea Iraq, Syria na maeneo ya bara la Afrika ni vita vya kiuchumi, ili nchi kubwa dhidi ya nchi changa kuzifanya nchi changa na watu wake kuwa masikini wa kutupwa na kupokonya utajiri wao mpaka washindwe kupata mahitajio ya msingi ya kila siku mpaka serikali hizo zishindwe kutimiza mahitajio ya rai wake kwa kushindwa mishahara yao na kuendeleza migomo kwenye kazi na kumakinisha hali ya siasa isiyo thabiti. (Aljazeera)

Huo ndio ubepari uliogeuza dunia kuwa pahala pa dhiki na tabu na pori ambalo wanyama wenye nguvu huwala na kuwatesa wanyama dhaifu.

Katika Uislamu, nidhamu yake ya kiuchumi ni tofauti na nidhamu ya kiuchumi katika ubepari, kwa kuwa haikumwacha mwanadamu huru kumiliki kwa njia aitakayo yeye au kile atakacho, kama vile kumiliki kwa riba, wizi, ujambazi nk. bali umemwekea sheria za kumiliki umekataza kumiliki mali kwa riba sawasawa iwe ndogo au kubwa.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنْ الرِّبَا إِنْ كُنتُمْ مُؤْمِنِينَ (البقرة: 278).
“Enyi Mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu na acheni yaliyobakia katika riba ikiwa mmeamini” (Baqara : 278)

Aidha, Uislamu ukafafanua kuwa unapomkopesha mtu ni kitendo kitukufu unachostahiki kupata thawabu. Na pindi mdaiwa anapodhikika hawezi kulipa deni kwa wakati, kutokana na hali yake ya kiuchumi, sheria imemtaka mdai asubiri mpaka (mdeni) aimarike kiuchumi, na ikiwa anataka atamsamehe ni bora na kuna ujira mkubwa.
وَإِنْ كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَى مَيْسَرَةٍ وَأَنْ تَصَدَّقُوا خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ (البقرة: 280).
“Na kama(mkopaji) ana dhiki basi mdai angoje mpaka afarijike. Na kama nyinyi (mnaodai mkizisamehe deni zenu) mkazifanya sadaka basi ni bora kwenu ikiwa mnajua haya” (Baqara : 280)

Pia, baada ya Uislamu kuonyesha ubaya wa riba na kuikataza kwa makatazo makali imeweka njia mbadala katika miamala ya watu kwa kusaidiana na kuleta faraja kiasi fulani kwa kufaradhisha ibada ya zaka, ya kutoa kiwango maalum cha mali kutoka kwa matajiri na kupewa masikini kama ilivyofafanuliwa kwa kina ndani ya fiqhi ya Kiislamu.

Hali hii ilidhihirika zaidi wakati wa Khilafah ya Abu Jaafar Mansour (Abassiya ambapo zaka na sadaka zilikuwa zikisafirishwa kutoka Baghdad na kupelekwa bara Hindi. Inakadiriwa kuwa wastani wa sadaka kwa kila raia aliyekuwa akipokea ndani ya Bara Hindi wakati huo kwa thamani ya leo ni sawa na dola 1800 kwa kiwango cha leo.

Huo ndio Uislamu unaomsukuma mwanadamu kufanya vitendo kwa kudiriki fungamano lake na Mola wake, huku lengo lake kuu ni kupata radhi za Allah Taala, tofauti na ubepari ambao umemfanya mtendaji kufanya vitendo kwa kuangalia maslahi na manufaa yake murua wala ubinadamu.

Ust. Issa Nasibu
#UislamuNdioUfumbuziSahihi
Risala ya Wiki No. 69
02 Jumada al-thani 1441 / 27 Januari Miladi
Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.