Bonde la Olduvai: Fakhari au Fedheha?

Karibuni tumeshuhudia sherehe ya kifakhari katika Bonde la Olduvai (Oldupai), Ngorongoro kuadhimisha miaka 60 tangu ugunduzi wa fuvu la sokwe linaloitwa Zinjanthropusboisei lililopatikana ndani ya mwaka 1959. Fuvu linalodaiwa kuwa asili ya binadamu wa mwanzoni. Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na maafisa wakubwa wa serikali akiwemo Waziri Mkuu, Waziri wa Utalii na Waziri wa Utamaduni, pia yaliambatana na uzinduzi wa mnara wa makumbusho ulionakshiwa kwa sura za mafuvu mawili makubwa ya masokwe wa zama damu (Zinjanthropusboisei na Homohabilis) ili kuvutia wageni kutembelea makumbusho hayo na kutambua kuwa hapo ndipo ‘chimbuko halisi la mwanadamu’

Ugunduzi wa fuvu la sokwe Zinjanthropusboisei (1959) uliofanywa na familia ya kiengereza ya bwana Louis Leakey unachukuliwa kuwa ni ugunduzi muhimu zaidi, kwa kuwa mabaki ya sokwe huyo yanahusishwa na kizazi cha kale zaidi cha kizazi cha Australopithecus ambacho hudaiwa kuwa ni cha mapema katika ‘chimbuko halisi la wanadamu. Sokwe huyo anadaiwa kuishi zaidi ya miaka milioni na nusu iliyopita.
Ugunduzi huo katika Bonde la Olduvai na ule wa Raymond Dart (1924), Robert Broom (1936) ndani ya Afrika ya Kusini na sehemu nyengine ndani ya Afrika unafasiriwa na ‘wanahistoria’ kwamba chanzo cha wanadamu kilikuwa Bara la Afrika.

Harakati hizi za ugunduzi zinashabihiana sana na zile harakati za wanaoitwa wavumbuzi (majasusi) na ujio wa wamisionari waliokuwa wakala wa ukoloni. Wao pia walilenga upande maslahi ya kimfumo kwa kumakinisha ukoloni, uwe wa kifikra, kisiasa au kiuchumi. Wakati nchi changa ikiwemo Tanzania zikijifakhiri kwa ugunduzi kama huu, madola ya kimagharibi wanafungamanisha na kinachoitwa ugunduzi huu kukuza na kutangaza ubwana wa fikra zao na madola yao.

Itakumbukwa kuwa mwasisi wa harakati za ugunduzi katika Bonde la Olduvai bwana Lous Leakey ni muingereza aliyezaliwa Kenya na familia ya wamisionari katika zama ukoloni wa kiengereza nchini humo, pia aliwahi kuwa idara ya ulinzi ya koloni la Uingereza nchini Kenya katika kitengo cha ujasusi. Hivyo, ni jambo lisilo na tembe ya shaka kwamba alikuwa wakala na mtumishi mtiifu wa dola ya Uingereza. Na hapana shaka kwamba kinachoitwa ugunduzi kimefanikiwa sana kukuza haiba ya Uingereza kimataifa.

Kwa upande wa Marekani nayo ilipoona imeachwa nyuma kukosa usemi na athari katika qadhia ya Olduvai, haraka nayo ndani ya mwaka 1986 kwa maslahi ya kukuza jina la dola yao ikajitosa katika ugunduzi nyongeza, ambapo jopo la wanahistoria wa kimarekani wakafukua mabaki ya mifupa 302 inayodaiwa kuwa na miaka milioni 1.8 https://www.livescience.com/40455-olduvai-gorge.html

Ugunduzi katika Bonde la Olduvai unamakinisha, kukuza na kuendeleza kutuhubiria fikra duni, isiyoingia akilini na ya kikoloni kama tutakavyodokeza mbele, kwamba chimbuko la mwanadamu katokana na kizazi cha sokwe kufuatia mchakato sadfa/ bahati nasibu wa mabadiliko ya hatua baada ya hatua (evolution) yaliyotokea mamilioni ya miaka. Fikra iliyokuja kupewa sura kwa upana na Mwingereza Charles Darwin 1859 katika kitabu chake cha “On the Origin of Species “ fikra ambayo leo hulazimishwa kufundishwa mashuleni.

Msingi wa fikra hii ni kukanusha uwepo wa Muumba, na kwamba uwepo wa mwanadamu na viumbe vyengine ni matokeo tu ya mabadiliko ya kimaumbile, tena mabadiliko ya sadfa (bahati nasibu). Fikra hii haikinaishi akili timamu, bali kimsingi hata akili ya mtu wa kawaida haiwezi kulikubali hili.

Kukanusha uwepo wa Muumba ni jambo lisilokubaliana na uhalisia, kwa kuwa kuna viumbe vilivyoenea, ni sawa na kukanusha kwamba hakuna muundaji wa gari ilhali magari yapo mbele ya macho yako. Lakini lau tukubali kuwa chanzo cha binadamu ni matokeo ya mabadiliko ya kimaumbile, japo sio kweli, bado hubakia swala msingi, nani aliyeleta maumbile hayo yaliyopangika kwa namna mwanana, jambo ambalo ni muhali kusema ni la bahati nasibu (sadfa)?

Aqidah ya Kiislamu kwa kuwa imejengwa katika msingi wa kukinaisha akili inakiri waziwazi kwamba kuna Muumba wa viumbe vyote, kwa kuwa ni ujuha wa kiwango cha juu kukiri uwepo wa viumbe lakini ukakanusha uwepo wa Muumba. Muumba huyo ndio Mwenyezi Mungu, hatendi jambo kwa sadfa au kubahatisha, ndio maana kila kiumbe au kiungo cha kiumbe kimeratibiwa katika hali ya umakini wa hali ya juu, kulingana na mazingira, matumizi na haja ya kiumbe hicho.

صُنْعَ اللَّهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ (النمل: 88

“……Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu, aliyekitengeneza kila kitu kwa uzuri. Hakika Yeye ni Mjuzi wa myatendayo” (TMQ An-Naml: 88)

Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake vyote kamfanya mwanadamu kuwa kiumbe kitukufu na chenye hadhi ya hali ya juu kwa kuwa ndio msimamizi wa ulimwengu (khalifah). Kamwe hakumfanya mwanadamu kuwa mnyama wala kutokamana na mnyama. Bali wanyama na viumbe vyote vimeumbwa na kudhalilishwa kwa ajili ya kumnufaisha mwanadamu. Quran inasema:

وَسَخَّرَ لَكُمْ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ جَمِيعًا مِنْهُ إِنَّ فِي ذَلِكَ لآياتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ (الجاثية: 13
“Na amevidhalilisha kwa ajili yenu vilivyomo mbinguni na ardhini, vyote kutokana nae. Hakika katika hayo zimo ishara kwa wanaofikiri.” (TMQ Al-Jaathiya : 13)

Kwa kuwa ‘unyama ni uduni na udhalili’ kamwe mwanadamu hakuumbwa katika hali ya uduni, na ndio maana akapewa akili. Isipokuwa mwanadamu huyo baada ya kuumbwa na kupewa utukufu huo, anaweza mwenyewe kujiingiza katika darja duni ya unyama.

Wapo wanadamu kutokana na maovu yao walilaaniwa na kupewa adhabu ya kugeuzwa wanyama kutokana na kuruka kwao mipaka. Hao walikuwa ni mayahudi walioadhibiwa kwa kugeuzwa wanyama, na hilo ni kama ilivyokuja katika ushahidi usio na shaka (nass). Allah SW anasema:

مَنْ لَعَنَهُ اللَّهُ وَغَضِبَ عَلَيْهِ وَجَعَلَ مِنْهُمْ الْقِرَدَةَ وَالْخَنَازِيرَ ِ (المائدة: 60

“Ni Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani na kumkasirikia, na amewafanya miongoni mwao manyani na nguruwe….. (TMQ Al-Maidah : 60)

وَلَقَدْ عَلِمْتُمْ الَّذِينَ اعْتَدَوْا مِنْكُمْ فِي السَّبْتِ فَقُلْنَا لَهُمْ كُونُوا قِرَدَةً خَاسِئِينَ (القرة65

“Na hakika mlikwishayajua ya wale miongoni mwenu walioruka mipaka katika Jumamosi (siku ya mapumziko), basi tukawambia : Kuweni manyani wadhalilifu”
(TMQ Al-Baqara :65 )

Pia mwanadamu anaweza mwenyewe kujitumbukiza katika darja duni ya unyama kama alivyofanya Darwin na wafuasi wake, pale anapokosa kuitumia vyema akili yake, hapo huwa kajifunika uduni wa mnyama au zaidi ya mnyama. Quran Tukufu inasema:

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِنْ الْجِنِّ وَالإِنسِ لَهُمْ قُلُوبٌ لاَ يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لاَ يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لاَ يَسْمَعُونَ بِهَا أُوْلَئِكَ كَالأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ أُوْلَئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ (الأعراف: 179).

“Na kwa hakika tumewaandalia moto wa Jahannam wengi katika majini na watu,(kwa sababu) Wana nyoyo lakini hawafahamu, na wana macho lakini hawaoni, na wana masikio lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walioghafilika”.
(TMQ Al-A’araf :179)

Charles Darwin, wafuasi na waumini wake wa dhana ya mabadiliko ya kihatua (evolution) kuwa ndio chanzo cha mwanadamu wamejiingiza kwa khiyari yao katika hili kundi la pili, kwa kushindwa kwao kutumia vyema akili zao kutambua jambo jepesi kama hilo. Cha kushangaza! uduni huo ambao ni stahiki yao wameutawanya kwa wanadamu wote.

Fikra ya ‘evolution’ sio tu imekuzwa na kupigiwa debe na wafuasi wake baada ya kuondoka Darwin, bali kama nilivyosema awali ni fikra ya kikoloni. Ilitumika na bado inatumika kuhalalisha utumwa, ukoloni, ubeberu, ubaguzi na dhulma kwa jumla.

Kwa kuwa fikra ya ‘evolution’ inahubiri kwamba wanadamu katika kufikia hapa alipo hupitia hatua mbalimbali kuanzia sokwe kupitia mchakato wa mabadiliko, mtazamo huo wa hatari ndio uliofasiriwa kwamba jamii za wasiokuwa wazungu hususan za Afrika au watu weusi kwa jumla bado ni ‘nusu watu’ (sub human), hawajafikia darja ya kuamiliwa kama wanadamu kamili. Hoja hizo ziliibuka sana kuhalalisha utumwa, ukoloni na hata ubaguzi wa leo. Ndio maana mpaka leo miongoni mwa istizai za kiubaguzi wanazotendewa watu weusi katika nchi za kimagharibi ni kunasibishwa na kima nk. Mitazamo hiyo ni athari ya fikra ya Darwin ambayo imeota mizizi katika nchi za magharibi na watu wao, na ndio maana ubaguzi kwao umebakia kuwa ni saratani iliyokita.

Hii ndio fikra ya ‘evolution’ ya Darwin inayofundishwa katika mashule yetu, inayotukuzwa na kujifakhiri kwa alama zake (shaair) kama bonde hili la Olduvai. Vipi tunaukataa ukoloni, utumwa na ubaguzi lakini fikra inayohalalisha hayo tunaikumbatia, kuitukuza, kuiunga mkono na kuipigia debe?

Afrika na nchi changa kwa jumla zinahitaji mapinduzi makubwa ya kifikra. Zinahitaji fikra pana itakayokomboa rasilmali na utajiri mkubwa uliopo, kwa kuwa ukombozi wa kila alichonacho mwanadamu hutegemea uthabiti na upana wa fikra anayobeba.

Masoud Msellem

Risala ya Wiki No. 52

06 Dhu al-Hijjah 11440 Hijri / 07 Agosti 2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.