Kongamano la Urusi na Amerika Jijini Helsinki

Swali

Maraisi wa Amerika na Urusi walifanya kongamano lao jijini Helsinki, mji mkuu wa Finland, mnamo Jumatatu 16/7/2018. Je hii ina maana kuwa taharuki kati ya nchi mbili hizi imekwisha? Je, kuna maana yoyote ya kufanywa kwa kongamano hili baada ya kongamano la nchi za NATO mnamo 12/7/2018 na taharuki iliyojitokeza kati ya Amerika na washirika wake wa Ulaya? Je, ina athari yoyote juu ya uhusiano wa Urusi na China? Je, kuna athari yoyote ya kongamano hili juu ya maamuzi nchini Syria?

Jibu
Katika kujibu maswali haya kuhusu kongamano la Amerika na Urusi jijini Helsinki, tunasema: kwamba baada ya takriban kipindi kirefu cha taharuki katika mahusiano kati ya Amerika na Urusi, iliyoanza mnamo 2014 wakati Urusi ilipoiunganisha Crimea nayo, na Amerika na Ulaya kujibu kwa kuiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi. Na taharuki kati ya nchi mbili hizi kuongezeka kwa kumalizika utawala wa Obama ambao uliituhumu Urusi kuingilia uchaguzi wa Amerika kwa manufaa ya mgombezi Trump, tangu wakati huo ilifutilia mbali kivitendo mikutano ya ngazi za juu kati ya pande mbili hizi … ingawa maraisi wawili hawa walikutana mara mbili kabla ya kongamano hili; walikutana pambizoni tu mwa kongamano la G20 mjini Hamburg, Ujerumani mnamo Julai 2017, na kukutana pambizoni mwa baraza la kikao cha ushirikiano wa kiuchumi (APEC) nchini Vietnam mnamo Novemba 2017. Lakini, mikutano hiyo haikuinuka kufikia kiwango cha kongamano; ilikuwa ni mikutano mifupi na wala haikujadili kwa kina faili muhimu baina yao. Wakati wa kipindi cha mwaka mmoja na nusu cha utawala wa Trump, Urusi ilitafuta kwa ari kongamano baina ya maraisi hawa wawili, lakini Amerika ilikuwa ikiliakhirisha, na ilikuwa ikiuchukulia uakhirishaji huu kama mbinu ya kutilia shinikizo Urusi. Urusi imekuwa ikiusubiri mradi wa Trump ili kuimarisha mahusiano kati yao, lakini ilitambua ugumu wa kufanya hivyo kwa sababu ya wimbi kuu la upinzani katika upande wa Raisi Trump. Athari ya hili iliibuka wakati wa uchunguzi wa wazi dhidi ya Urusi na kujiuzulu kwa wanachama wa kundi la Trump juu ya madai kuwa na uhusiano na Urusi. Hivyo basi, mkutano wa kiwango kikubwa katika ngazi ya kongamano umekuwa ndio ndoto kuu ya Urusi ambayo Urusi ilishindwa kuifikia. Iliwezekana tu baada ya Marekani kukubaliana nayo: “Msemaji wa Baraza la Usalama wa Kitaifa la Marekani Garrett Marquis alitangaza Alhamisi ya mwisho 21/6/2018 kuwa Mshauri wa Raisi wa Usalama wa Kitaifa, Bolton, atazuru Moscow mwishoni mwa mwezi huu na atajadili maandalizi ya kongamano kati ya Urusi na Marekani.” Shirika la Kirusi la Sputnik 24/6/2018. Kwa hiyo, jambo muhimu zaidi kuzingatia katika kongamano hili, liliofanyika tarehe 16/7/2018 ni kwa nini Marekani iliamua (na sio Urusi) kuandaa kongamano kati ya marais hawa wawili, na nini inataka kupata kutokamana nalo? Ili kufafanua hili,
tunasema:
1- Viashiria vyote vinaonesha kuendelea kwa shinikizo la Marekani juu ya Urusi. Siku mbili kabla ya kongamano hilo, Marekani iliwatuhumu maafisa wa kijasusi wa Urusi kwa kuhusika katika uharamia wa uchaguzi wa Marekani: “Idara ya Haki ya Marekani imewatuhumu maafisa 12 wa Kijasusi wa Urusi kwa udukuzi wa akaunti za maafisa wa chama cha Kidemokrasia wakati wa uchaguzi wa urais wa 2016, kwa mujibu wa Rod Rosenstein, naibu waziri wa haki, kwamba watuhumiwa walitumia jumbe za kupenyea zijulikanazo kama ‘phishing’ na barnamiji mbaya za komyuta … Ikulu ya White House ilisema kuwa mkutano kati ya Trump na Putin Jumatatu utaendelea.” Gazeti la Misri Al Ghad 14/7/2018. Mara baada ya Mkutano wa Trump na Putin kumalizika huko Helsinki, kituo cha runinga cha al-Jazeera kiliripoti mnamo tarehe 16/7/2018, tamko la Marekani la kukamatwa kwa mwanamke Mrusi huko Washington kwa mashtaka ya ujasusi kwa Urusi. Kwa vitendo hivi vilivyofanywa na mashirika ya serikali ya Marekani, kupunguza shinikizo kwa Urusi hakutarajiwi kuwa kama Urusi inavyotaka, licha ya kongamano hilo kati ya marais hawa wawili.
Hii ina maana kwamba kuna sababu nyingine ambazo zimeisukuma Marekani kukubali ombi la zamani la Urusi la kutaka kongamano kati ya Maraisi Trump na Putin. Mambo haya yanadhihirishwa na dhurufu za kongamano hilo …

2- Kongamano la Marekani na Urusi lilifanyika katika dhurufu ambayo Marekani imejiingiza vita vya kibiashara dhidi ya mahasimu wawili wakuu, Muungano wa Ulaya na China, na inaonekana kwamba Marekani iliamua kufanya kongamano hilo kwa kucheza kadi ya Urusi dhidi ya mahasimu hao wawili kwa pamoja! Kuhusu Muungano wa Ulaya, Marekani ilichagua wakati wa kongamano hilo na Urusi punde tu baada ya kongamano la nchi za NATO, liliofanyika jijini Brussels huku kukiwa na sintofahamu kubwa kati ya Muungano wa Ulaya na Marekani. “Kongamano la NATO lilizinduliwa jijini Brussels leo huku kukiwa na matarajio kuwa litasheheni taharuki, hasa kati ya Washington na washirika wake wa Ulaya kwa msingi wa tofauti za kibiashara na matumizi katika ulinzi na makubaliano ya kinuklia ya Iran. Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alikiri kuwepo kwa “sintofahamu na maoni tofauti miongoni mwa washirika’ (Russia Today, 11/7/2018), na Raisi wa Marekani Trump aliutaja Muungano wa Ulaya kama ‘mpinzani’ hadharani kwa mara ya kwanza katika historia ya mahusiano kati ya pande zote za Atlantiki. Kongamano na Urusi lilikuwa mojawapo ya ala muhimu zaidi ya shinikizo la Marekani dhidi ya Ulaya. Na hii ndio namna yake:
A- Raisi wa Marekani amewatishia Ulaya na rufaa ya Urusi kuhusu Ukraine, Raisi wa Baraza la Ulaya,
Donald Tusk, alisema kuwa: “Raisi wa Marekani Donald Trump amemwambia kuwa madhumuni ya sera ya
Urusi kwa Ukraine yalikuwa yanamvutia kwake, Trump alikiri kwamba shauku yake kwa Ukraine ni kidogo
sana, Tusk aliongeza katika mahojiano yake na TVN24, kituo cha habari nchini Poland: “Katika mazungumzo
kadhaa na mimi, Rais Trump hakuficha kwamba alihisi shauku kidogo kwa Ukraine na kuelewa zaidi ilichofanya Urusi nchini Ukraine,” (Russia Today, 15/7/2018) Hili ni jambo nyeti barani Ulaya. Ulaya imevitazama vitendo vya Ukraine kama vyenye kuingilia usalama wote wa Ulaya, hilo haliwezi kuvumiliwa, na taarifa ya Trump inachukuliwa na Muungano wa Ulaya kuwa ya hatari kwa Ulaya, inamaanisha kuwa Urusi yaweza kuharibu mpaka wa Ulaya na ramani kutoka upande wa mashariki!

B- Tishio la Raisi wa Marekani Trump kwa Ulaya la kuirudisha Urusi katika G7: “Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Ijumaa, 8/6/2018, alitoa wito kwa wenzake wa G7 kuzingatia kurudi kwa Urusi katika kundi hilo. Trump alisema kabla ya kuelekea nchini Canada kushiriki katika kongamano la G7 huko La Malbaie katika jimbo la Quebec: “Waliitupa Urusi nje … Wanapaswa kuiruhusu Urusi kurudi tena ndani, kwa sababu tunapaswa kuwa na Urusi katika meza ya majadiliano”. Urusi ilifukuzwa kutoka G8 baada ya kuiteka na kuiunganisha Crimea nayo na hivyo kundi hilo likajumuisha nchi saba tu.”
(Chanzo: Al Arabiya.net, 8/6/2018).

C- Al-Jazeera iliripoti mnamo tarehe 15/7/2018, yaani baada ya kumalizika kwa kongamano la NATO (viongozi wa Ulaya wana wasiwasi juu ya maridhiano kati ya Urusi na Marekani). Kinachoashiria wasiwasi mkubwa wa Ulaya kuhusu maridhiano ya Marekani na Urusi ni kile alichosema Waziri wa Kigeni wa Ujerumani: “Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani alimuonya Raisi wa Marekani Donald Trump juu ya mikataba yoyote ya upande mmoja kwa gharama ya washirika wake wa Ulaya wakati wa mkutano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Mass aliliambia gazeti la ‘Bild am Sonntag’: “Mikataba ya upande mmoja kwa gharama ya washirika itakuwa na madhara kwa Marekani, pia. Mtu anayewapiga washirika wake anajihatarisha hatimaye (Russia Today, 15/7/2018). Maridhiano kati ya Marekani na Urusi yanaweza kuharibu Muungano wa Ulaya, kama vikwazo vya Ulaya vilivyoekewa Urusi, ambavyo hufanywa upya kila baada ya miezi sita kwa sababu ya Crimea na Ukraine, vitadhaifishwa na hapo Urusi kutojali nchi za Ulaya basi.
D- Raisi wa Marekani Trump, ambaye amekosa hekima ya kisiasa, anaendelea kuushambulia Muungano wa Ulaya hadharani, hasa Ujerumani, juu ya kadhia ya ununuzi wa gesi ya Urusi, kama tulivyotaja katika jibu la swali la tarehe 17/07/2018 … Wakati mwingine anautaja kama “hasimu” yaani “adui” na mara nyingine anachochea dhidi yake kama ilivyo katika ushauri wake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza wakati wa mkutano wao wa jijini London: “Katika mahojiano na BBC, May alisema akijibu swali juu ya ushauri wa Trump alisema:
“Aliniambia kuwa niushtaki Muungano wa Ulaya. Sio kuingia katika majadiliano” (BBC 15/7/2018).
Uingereza, licha ya kutangaza nia yake ya kujiondoa katika Muungano wa Ulaya, lakini ina maoni sawa na ya nchi za Ulaya juu ya Urusi, na hakuna uwezekano kwamba Uingereza kuichokoza Urusi ni kulivuruga
kongamano kati ya Urusi na Amerika, “Tovuti ya Mil Radar, inayo shughulika na uchunguzi wa trafiki angani,
iliripoti kuwa ndege ya upelelezi ya kikosi cha angani cha Uingereza ilifanya uchunguzi karibu na pwani ya Crimea ya Urusi.” (Russia Today, 15/7/2018).
Hivyo basi, kwa shinikizo la Marekani juu ya Ulaya na tishio lake la kuiregesha Urusi katika G7 na kudokeza
kuitambua Crimea kama sehemu ya Urusi, na Marekani kutofautiana juu ya msaada wa Ukraine mbele ya
shambulizi la wafuasi wa Urusi upande wa mashariki (Donetsk na jimbo la Luhansk) na kuboresha uhusiano
wa Marekani na Urusi kupitia kongamano hilo, ingawa si kwa njia ya moja kwa moja lakini ni tishio kubwa kwa Ulaya kwa haja ya kutimiza matakwa ya Marekani na kuongeza matumizi ya ulinzi katika NATO … yaani,
Marekani imezifinya nchi za Muungano wa Ulaya kupitia maridhiano yake na Urusi, na hii ni mojawapo ya
malengo makuu ya Marekani ya kufanya kongamano kati ya Trump na Putin.
3- Kuhusu upande wa China, ni kama ifuatavyo:
A- Kongamano kati ya Marekani na Urusi pia lilifanyika nyuma ya vita vya kibiashara vinavyoongozwa na
Marekani dhidi ya Beijing. Mara tu Marekani ilipokwisha tumia vya kutosha huduma za China kwa kupitia
kulainisha msimamo wa Korea Kaskazini na kuiweka kwenye njia ya suluhisho ya amani na kuondoa tishio
la vita kutoka katika bara la Korea. Hii iliwakilishwa na kongamano kati ya Marekani na Korea Kaskazini nchini Singapore tarehe 12/6/2018. Rais wa Marekani aliishukuru China kwa juhudi zake katika hilo. Mara tu
baada ya matukio haya kufanyika, Marekani ilitekeleza sera zilizotangazwa na Trump dhidi ya China hata kabla ya kuwa raisi … Marekani iliweka ushuru wa forodha kwa bidhaa za kutoka China wenye thamani ya dola bilioni 50 kwa mwaka, China ilijibu kwa kuweka ushuru wa forodha kwa thamani sawa kwa bidhaa kutoka Marekani. Marekani kisha ikatangaza mpango mpya wa kulazimisha ushuru wa forodha kwa bidhaa nyingine za kutoka China wenye thamani ya dola bilioni 200, ambazo China haiwezi kwa njia hiyo hiyo, kwa sababu bidhaa zote jumla kutoka Amerika ni dola bilioni 130, huku bidhaa inazosafirisha kwenda Amerika ni dola bilioni 500, ambayo inasababisha China kufikiria njia nyingine za kukabiliana na vita vya kibiashara na Marekani.
B- Mojawapo ya njia hizi zilizochaguliwa na China ilikuwa ni maridhiano na Urusi. Shirika la Shanghai
lilifanya mkutano wake wa mwisho nchini China mnamo 10/6/2018 kwa ushirikiano na mkutano wa nchi saba zilizoendelea-G7 (ambayo Urusi ilifukuzwa uanachama wake mwaka 2014) uliofanyika Canada mnamo
9/6/2018. Mikutano hii miwili imeonyesha mgawanyiko duniani. Magharibi inakutana nchini Canada na Mashariki inakutana nchini China, na hili halikupendelewa na Amerika baada ya kuanzisha utawala wake wa
kiulimwengu baada ya kuanguka kwa Muungano wa Kisovieti mwaka wa 1991. Amerika iliona pasi na shaka
kwamba nchi hizi mbili zilizochangamfu katika Shirikala Shanghai, China, ambayo Marekani imetangaza vita
vya kibiashara dhidi yake, na Urusi, ambayo Marekani imeiwekea vikwazo vikali na vyenye kukua dhidi yake.
Kwa upande mwingine, Amerika iliona kwamba Urusi na China zinaweza kutegemeana zaidi chini ya sera ya
Marekani dhidi yao, kwa kuzichukulia kama mahasimu katika biashara na siasa za kimataifa, kwa mujibu wa
sera hii ya Marekani kwa China na Urusi, Amerika imeona kwamba sera yake ina zisukuma nchi hizo mbili
katika ushirikiano wa karibu, ikiwa upande wa kijeshi. Urusi na China zinahisi kuwa zinakabiliwa na adui
mmoja, yaani Marekani, na kwamba ushirikiano wao unaimarisha nguvu zao. Ujumbe wa waziri wa ulinzi wa
China uliweka wazi sana hisia hii. “Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Schweigo alimpokea mwenzake wa China, Wei Fenghe, ambaye aliwasili jijini Moscow kama kinara wa ujumbe wa kijeshi ili kushiriki katika kongamano la Usalama wa Kimataifa. Ujumbe wa China uliwasili ili kuwaonyesha Waamerika mafungamano thabiti kati ya majeshi ya China na Urusi, hasa katika hali iliyoko sasa.” Waziri wa China alithibitisha: “Tulikusaidia. Upande wa China uko tayari kuonyesha, pamoja na upande wa Urusi, wasiwasi wetu na msimamo wetu wa pamoja juu ya masuala muhimu ya kimataifa.’’ (Russia Today, 3/4/2018)

C- Hivyo basi Amerika iliona kuwa kufungua mlango kwa ajili ya maridhiano ya Urusi na Marekani kutapelekea kuwepo kwa utengano kati ya Urusi na China, na hatimaye kuvunja muungano wao tete kabla ya kumalizika kwa nguzo zake, hususan katika jeshi. Hii nikwa sababu Amerika inatambua kile ilichonacho Urusi katika upande wa uwezo wa kijeshi, na kuziweka nguvu hizi au sehemu yake pamoja na China kutaipa nguvu na kuiruhusu kupinga sera ya Marekani, yaani, kutotimiza matakwa ya Washington. Washington ililiona hili kama jambo rahisi kulifanya. Urusi inakwenda China kama mkakati mpya kwa sababu ya mahusiano yake duni na Magharibi. Ikiwa Marekani inaonyesha maridhiano yake na Urusi, shinikizo kwa
Urusi itapunguwa na haitakwenda China. Kwa sababu ya yote haya, Washington iliona kuwa
ni sharti ifungue mlango wa matarajio kwa Urusi ili kuregesha mahusiano yake na Marekani katika
msimamo uliokuwa mwanzoni kupitia kongamano hili baina ya maraisi wawili hawa, yaani, kuisitisha Urusi
kwenda China. Ingawa ni mapema mno kuhukumu juu ya kupatikana kwa malengo haya ya Mrekani kutokana na kongamano hili pamoja na Urusi, na inategemea hatua za mbeleni za maridhiano kati ya Washington na Moscow, lakini Marekani yaweza kuuvunja kiurahisi “muungano” huo tete, mpaka kufikia sasa, kati ya Urusi na China. Marekani inachukua hatua kadhaa katika upande huu, baadhi ya wakati upande wa Urusi kama ilivyo katika kongamano hili, na baadhi ya wakati upande wa China. Kwani maslahi ya kibiashara ya China na Marekani yana kipaumbele kikubwa zaidi jijini Beijing kuliko uhusiano wowote ambao China iko nao na Urusi.
4- Kuongeza athari ya jumbe kali za Trump kwa Muungano wa Ulaya na China, Trump ililifanya
kongamano hili kuwa mkutano wa wazi kulipeleka kila anapoona haja ya kulipeleka. Yaani ni mwanzo wa hatua zinazofuatia! Hivyo basi alisema baada ya mkutano wake wa faragha na Putin jijini Helsinki kuwa kongamano hili lilikuwa “mwanzo mpya” kwa mujibu wa kituo cha habari cha Urusi cha Russia Today mnamo 16/7/2018. Katika mkutano na waandishi wa habari uliopeperushwa moja kwa moja na Russia Today, alitangaza makubaliano kati ya nchi mbili hizo ili kuanza majadiliano juu ya kupanua makubaliano ya kusitisha silaha za kinuklia baina yao ya mnamo 2010, ambayo yatamalizika mnamo 2021, na Raisi wa Marekani Trump ametangaza kuwa mahusiano na Urusi yalikuwa katika hali mbaya baina yao masaa
manne yaliyopita, lakini sasa hali imebadilika… Na haya yalikuwa mazungumzo jumla ambayo yanaafikiana
barabara na yale yaliyotangazwa na John Bolton, Mshauri wa masuala ya Usalama wa Kitaifa wa ikulu ya
White House aliyesema katika kipindi cha “This Week” katika kituo cha ABC network “Tumeomba, na Warusi
wamekubali, kwamba kimsingi hayatakuwa na muundo.
Sisi hatutafuti matunda thabiti,” Balozi wa Marekani nchini Urusi, John Huntsman aliliambia shirika la habari
la NBC: “Sio kongamano… ni mkutano… kwa hivyo hili ni jaribio la kuona kama twaweza kutatua na kuondoa baadhi ya visa, na kuweka wazi zaidi baadhi ya hatari, katika uhusiano huu kwa sasa. (Reuters, 16/7/2018)

5- Haya yanathibitisha kuwa Marekani bado haijapanga kuimarisha mahusiano yake na Urusi na ingali
inafuatilia sera ya shinikizo juu yake. Lakini kwa sababu zihusianazo na hali ya kimataifa na vita vya kibiashara vya Marekani na Muungano wa Ulaya na China, ilitaka kuiogopesha Ulaya kwa maridhiano yake na Urusi. Na iliamua kufungua nafasi ya matarajio kwa Urusi ya kukomesha kutengwa kwake kimataifa na ya kuimarisha mahusiano yake na Marekani, yote ni kwa ajili ya kuiweka mbali na maridhiano na China kwa upande mmoja, na upande mwengine, Urusi huenda ikaitikia matakwa ya Marekani katika kadhia nyenginezo za kimataifa, kama ilivyo fanya katika kusaidia sera ya Marekani nchini Syria, kwa kuibakisha serikali kibaraka wa Marekani nchini Syria madarakani! Hivyo basi, kongamano hilo lilikuwa si la kutatua kadhia maalumu za kimataifa bali ni la kutuma ujumbe mkali ulioelekezewa China na Muungano wa Ulaya. Vyenginevyo, mazungumzo yalikuwa jumla na yalijadili kila kitu na sio vitu maalumu, kama ilivyothibitishwa na taarifa za pande zote mbili. “Trump alisema kuwa mazungumzo yake na Putin yatashughulikia “kila kitu, kuanzia biashara, masuala ya kijeshi, makombora, na “kumalizia” na China, tutazungumza kifupi kuhusu China na rafiki wetu wa pamoja, Raisi Xi” huku “Raisi wa Urusi Vladimir Putin akimwambia Raisi wa Marekani Donald Trump mwanzoni mwa kongamano lao jijini Helsinki kuwa wakati umewadia kuzungumza kuhusu mahusiano kati ya Moscow na Washington. Aliongeza kuwa pia wanapaswa kujadili kadhia nzito za kimataifa kati ya pande mbili hizo.” (Reuters, 16/7/2018). Waziri wa Kigeni Sergei Lavrov alithibitisha kuwa kongamano hilo la Helsinki litazungumzia “kadhia zote nzito ambazo misimamo yetu inatofautiana ili tufanye kazi kuyaleta karibu maoni yetu kutatua matatizo haya,” na akataraji kufikiwa makubaliano. (Tovuti ya Al Jazeera.net, 16/7/2018) Ujumla huu unaonyesha nia ya kongamano hilo ya kutotatua kadhia za kimataifa, na hili liko dhahiri kutokana na matokeo ya kongamano hilo ambayo baadhi ya vyombo vya habari vimeripotia. Kwa mfano, pande mbili hizo zilikubaliana juu ya usalama wa umbile la Kiyahudi. Trump alisema “kutoa usalama kwa “Israel” ni jambo ambalo Putin na mimi tungependa kuliona sana.” (Reuters, 16/7/2018) na kwamba pande mbili hizo zinataka Syria kurudi katika hali ya kijeshi iliyoafikiwa mnamo 1974 baada ya kumalizika kwa mapigano kusini mwa Syria … Yote haya si mageni, Marekani na Urusi
zimekuwa zikiyasema hadharani kwa muda mrefu, hili si jambo ambalo viongozi wa Marekani na Urusi
wanakutana kwa ajili yake. Hili ni sawia na kukomesha silaha za kinuklia baina ya nchi zao. “Raisi Donald
Trump alisema kuwa tatizo la kukomesha silaha za kinuklia ni tatizo msingi ambalo halina budi kutatuliwa
na Marekani na Urusi. Trump alisema katika mahojiano na shirika la habari la Fox News kuwa “asilimia 90 ya
silaha za kinuklia ulimwenguni zinamilikiwa na Urusi na Marekani, akitaja kuwa mtangulizi wake, Raisi Barack Obama, alikadiria kuwa mvuke na viwango vya joto la kiulimwengu ndio tatizo muhimu mno, ambalo ni sharti liangaziwe.” (Russian Today, 17/7/2018) … na kila mwenye maono anajua kuwa Marekani na Urusi hazikutani kukomesha silaha zao za kinuklia kwa khiari, lolote watakalosema, hivyo basi, mkutano wao si kwa lengo hili…
6- Ama kuhusu athari ya kongamano hilo juu ya uwanja wa Syria, inaweza kusemwa kuwa hakuna lolote jipya katika kongamano hili kuhusiana na sera za Marekani na Urusi nchini Syria. Nchi mbili hizi zinakubaliana kikamilifu juu ya kuyamaliza mapinduzi ya Syria, zote zinasubiri kupata hili pamoja na kukubaliana kikamilifu juu ya hilo, tangu baada ya mkutano kati ya Obama na Putin mnamo 29/9/2015, Urusi imetekeleza sera ya Marekani nchini Syria na kwa ushirikiano nayo, huku Urusi ikijihusisha na matendo ya moja kwa moja ya kijeshi kama umwagaji mabomu wa mji wa Daraa na viunga vyake, Marekani inaisaidia, kama ilivyo katika barua iliyotumwa kwa upinzani nchini Syria eneo la kusini, kuwa “Marekani
haitawapa usaidizi wowote wakati wa shambulizi la Daraa.” Hakuna jipya kuhusu juhudi za Urusi za kumaliza
mapinduzi ya Syria kijeshi na urahisishaji wa Marekani kwa hilo.
Ama kuhusu suluhu ya kisiasa nchini Syria, Marekani inaiakhirisha mpaka serikali ya Damascus na Urusi
zikamilishe mchakato wa kumaliza upinzani wa kijeshi. Hapo, ndipo Marekani itaongoza mchakato mpana wa kisiasa nchini Syria kwa mujibu wa maslahi yake, kwa dori ya Urusi au pasi kwa dori ya Urusi. Na mchakato huu wa kisiasa haukujadiliwa katika kongamano hilo ishara kuwa Marekani inauakhirisha au haitaki Urusi iwe na dori ndani yake, au yote mawili … Hakuna uwezekano kuwa Urusi inatambua kuwa malengo ya sera ya Marekani nchini Syria hayaruhusu Urusi kushiriki ndani yake, lakini Urusi inataraji kuwa Marekani haitaizuia nchini Ukraine, hususan Crimea… Trump aliifurahisha Urusi kwa matamshi yake kuhusu Crimea, kama ilivyo tajwa juu, alipotangaza katika kongamano la G7. Mwezi uliopita wa Juni vyombo vya habari vilitangaza kuwa Trump alitangaza wakati wa kongamano la G7 kuwa Crimea ni eneo la Urusi kila mmoja huko anazungumza Kirusi (Russia Today, 15/7/2018). Hii ni hatari mno kwa Ulaya, inayoamini kuwa Urusi inaharibu mipaka na ramani ya Ulaya kutokea upande wa Mashariki. Pengine Urusi itatumbukia ndani ya maangamivu yake kwa taarifa za Trump, na kwa hakika itatumbukia, na kufedheheka mbele ya Waislamu kutokana na uhalifu wake iliowafanyia dhidi yao kwa ajili ya maslahi ya Marekani! Na hili litabakia katika kumbukumbu ya Waislamu dhidi ya Marekani na Urusi na wapambe wao na wafuasi wao, kwa sababu zama zitabadilika, na uhalifu hautawaokoa wale walioutekeleza.

سَيُصِيبُ الَّذِينَ أَجْرَمُوا صَغَارٌ عِنْدَ اللَِّ وَعَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا كَانُوا يَمْكُرُونَ

“Utawafika wale waliohalifu udhalilifu mbele ya Allah
na adhabu kali kutokana na vitimbi walivyokuwa
wakivifanya”

[Al-An’am: 124]

8 Dhul Qi’dah 1439 H
21/7/2018 M

Maoni hayajaruhusiwa.