Wimbi la Upinzani Kuhama Hama Vyama Tanzania

Habari:
Katika miezi ya karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuhusu wimbi kubwa la wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania kuhama vyama vyao na kujiunga na chama tawala (CCM). Tukio la karibuni zaidi linamhusisha Mbunge wa Chadema wa Jimbo la Ukonga, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, wabunge wengine wa upinzani na madiwani, ambapo wote wametangaza kuachana na vyama vyao vya upinzani na kujiunga na chama tawala (CCM).

Maoni:
Sakata hili linafedhehi uhalisia wa vyama vya kidemokrasia na wanasiasa wake, kuwa wapo kwa ajili ya maslahi binafsi na siyo kwa ajili ya Ummah, kinyume na daima wanavyohubiri na kuulaghai Ummah, kwa kuwa uhamaji huu huwaacha wanachama na wapenzi wa vyama vilivyohamwa katika huzuni na mtafaruku mkubwa.

Wimbi hili la uhamaji kutoka upinzani kwenda chama tawala limekuja kipindi ambacho serikali imepiga marufuku mikusanyiko ya kisiasa na kusambaa mshikemshike ya wengi miongoni mwa viongozi wa upinzani kwa kushtakiwa ama kwa kufanya mikutano ya hadhara bila kibali au kwa kumkashifu Raisi wa Jamhuri. Ilitarajiwa sana na Ummah katika nyakati ngumu kama hizi viongozi wa upinzani kusimama imara na kupaza sauti zao kukemea, lakini wapii! kwa bahati mbaya kinyume chake wanahama vyama vyao na kujiunga na chama tawala kwa hoja zisizokinaisha kamwe. Na mara nyingi wengi katika waliokuwa wabunge na wawakilishi wengine wa kuchaguliwa kama madiwani husimama kugombea tena majimbo yale yale kupitia chama tawala. Wachambuzi wengi wamehusisha qadhia hii kama “ mchezo wa kuuza’ kunakosukumwa na maslahi binafsi.

Kwa upande mwingine, hama hama hii kutoka upinzani kwenda chama tawala imeongeza nguvu dhana kuwa uongozi wa sasa wa CCM unalenga kuangamiza upinzani nchini kwa gharama yeyote, ikiwemo kuwapa viongozi wa upinzani wanaohamia chama hicho nafasi za kugombea tena mara ya pili katika majimbo yale yale kupitia tiketi ya CCM. Bila ya kutaja uwepo wa tuhuma za rushwa kuwarubuni wapinzani katika michakato hii ya uhamaji, ambapo mwaka jana mmoja miongoni mwa viongozi wa Chadema aliwasilisha ushahidi wa video ya muamala wa rushwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa lakini taasisi hiyo iliukataa ushahidi huo.

Hapana shaka hama hama hii hufuatiwa na chaguzi ndogo za marudio ambazo hugharimu pesa nyingi za Ummah. Kwa mfano, uchaguzi katika majimbo matatu na kata sita mapema mwaka huu zilitumika karibu Tsh bilioni 3.1 na matumizi mengine zaidi yanatarajiwa kwa kuwa hama hama hii bado inaendelea. Ufujaji wa fedha hizi za Ummah usiokuwa wa lazima ungeweza kusaidia vijana wengi wasio na ajira ambao wanahitaji mitaji midogomidogo tu ili kuasisi biashara ndogondogo. Zaidi ya hayo, pia zingeweza kuimarisha huduma za Ummah kama afya, ambapo ripoti zinaonesha kuwa hata katika yale maradhi yanayodhibitika na kutibika kama malaria, pneumonia na matumbo ya kuendesha huangamiza maisha ya watoto 270 chini ya miaka mitano kila siku. Zaidi ya hayo, kuna sababu nyingi za kijamii na kiuchumi, pamoja na mazingira ya kijografia yanayochangia vifo vya watoto, hususan kukosekana usawa wa upatikanaji na matumizi ya huduma za afya.

Huu ndio uhalisia wa vyama vya kidemokrasia ndani ya Tanzania na ulimwenguni kote. Hutegemea usuhuba suhuba/kujuana, ukabila, na zaidi ya yote vimejengwa juu ya maslahi binafsi. Kwa kuwa demokrasia ni nidhamu ya kujitafutia na kujiongezea maslahi zaidi na zaidi kwa gharama yoyote, iwe kwa khiyana/usaliti, mauwaji, urongo nk.

Kwa upande wa Waislamu, ni lazima tujipinde kufanya juhudi kurejesha mfumo mbadala wa haki wa Uislamu chini ya serikali yake ya Khilafah Rashidah. Na kwa wasiokuwa Waislamu tunawanasihi wausome na kuutafiti Uislamu kama mfumo mbadala, kwani ni wazi mifumo ya Ubepari na Ujamaa imeshashindwa.

#UislamNiHadharaMbadala

Imeandikwa na Said Bitomwa
Mjumbe wa Afisi ya Habari Hizb ut-Tahrir Tanzania
Kwa ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Maoni hayajaruhusiwa.