16 Ramadhan

بسم الله الرحمن الرحيم

Siku kama hii mwaka wa 14 Ramadhan Hijri (kauli nyengine mwezi wa Muharram) Waislamu walipigana Vita vya Qadsiya. Vita vikubwa baina ya Waislamu na Wafursi vilivyoibuka wakati wa Khilafah ya Umar bin Khattab (R.A).

Jeshi la Kiislamu lenye idadi ya askari 28,000 likiongozwa na Sahaba mkubwa Saad bin Abi Waqqas (R.A) lilikabiliana na jeshi la Kifursi lenye majeshi 120,000 (mara 4 zaidi ya jeshi la kiislamu) likiongozwa na Jemadari wa kifursi anaeitwa Rustam.

Kabla ya vita kuanza, Waislamu walituma ujumbe wa kidiplomasia uliongozwa na Numan bin Maqran kuelekea Madain (Mji Mkuu wa dola) kwa kiongozi wa Mafursi, Kisra (Yezdgird).

Licha ya Kisra kukinaishwa kwa hatua za kidiplomasia hakukubali kuifuata haki ya Uislamu bali aliyatoa majeshi yake kwenye mji na kumtuma Jemadari Rustam kuwapiga Waislamu.

Kufika katika eneo la vita la Qadisiya, Rustam akataka mazungumzo na Waislamu. Sa’d bin Abi Waqqas akampa jukumu Kamanda Rabii bin Aamir (R.A) kuzungumza na Rustam.

Rustam nae akauliza sababu ya kuja kwa Waislamu (kama alivyoulizwa Numan), bila ya kusita Rabii ibn Amir akajibu:-

“Allah (S.W) ametutuma ili tumtoe amtakaye kuabudia viumbe kwenda kwenye ibada ya Allah, na kuwatoa (watu) kutoka kwenye dhiki ya dunia kuelekea kwenye ukunjufu wake, na kuwatoa kwenye mifumo jeuri kuelekea kwenye uadilifu wa Uislamu.”

Baada ya ushindi wa Waislamu katika Vita vya Qadsiya vilivyopiganwa kwa siku nne, mamlaka ya dola ya kifursi (Sassanian) yalikuwa taaban, kwa kuwa kabla ya vita hivi kulikuwa na Vita vya Dhi Qar. Hata hivyo, Vita vya Nahavand baada ya Vita vya Qadsiya ndivyo vilivyokuja kumaliza kabisa utawala wa mafursi na kufungua ukurasa mpya wa Fursi chini ya Uislamu.

Masoud Msellem

16 Ramadhan 1441 H – 09 Mei 2020 M

 

Maoni hayajaruhusiwa.