Wajibu wa Kuwaandaa Ahli Zetu Kwa Da’awa

Bila shaka tunafahamu kwamba tunafanya harakati ya kurejesha maisha ya Kiislamu kupitia Serikali ya Kiislamu ya Khilafah. Na ili kufikia lengo  hilo, tumechukua manhaji ya Mtume (SAAW), ambayo ni ya Ulinganizi wa daawa yake (SAAW) katika darul- kufru ya Makkah.

Tukiangalia harakati ya Mtume (SAAW) iliwajumuisha wanaume pia na wanawake. Na wanawake hao waliipa kipaumbele harakati hiyo. Aidha, wanawake hao walikuwa chachu muhimu kwa kuonesha msimamo makini wa imani usioyumba pamoja na kuwaliwaza na kuwapa moyo waume zao kwa yale wanayoyapata ya kuudhi na ya kukatisha tamaa katika daawa. Kama ilivyodhirika kwa Mtume mwenyewe (SAAW), alikuwa akipata faraja na moyo kutoka kwa mke wake kila anaporudi nyumbani pale anapopata linaloumiza moyo na kukatisha tamaa katika harakati za daawa yake. Mfano mzuri, wakati Mtume (SAAW) hajapata suluhisho la matendo maovu yanayotendwa na mujtamaa wa Makkah, na hakupenda kuona maovu hayo yakitendwa ilhali akiangalia, aliamua kutumia muda wake mwingi kwenye pango la Jabal Hiraa. Huko ndiko ambako baadae Jibril (AS) alimshushia wahyi na kumdhihirishia Utume. Tukio hilo lilimfadhaisha sana (SAAW) jambo lililomfanya kukimbilia nyumbani akiwa anatetemeka kwa khofu na woga. Lakini baada ya kumuhadithia mke wake bibi Khadija bint Khuwelid (RA) alimliwaza kwa kumwambia;

“Wewe si mtu wa kuwa na khofu. Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu (SWT), hatokudhalilisha milele. Kwa hakika wewe unaunga udugu na unabeba uzito wa wanyonge, unasaidia masikini, unakirimu wageni, na unasaidia katika matatizo ya kweli”.

Mtume (SAAW) akapata faraja baada ya kupata maneno hayo na hali yake kurudi ya kawaida.

Aidha,wakati Mtume SAAW alipokuwa akielezea wasifu wa mke wake Bibi Khadija (RA) alinukuliwa akisema :

“Aliniamini wakati waliponipinga, alinisadikisha wakati waliponikadhibisha, alinishirikisha katika mali yake wakati watu waliponinyima………..”.

Pia tusisahau msimamo wa Shahidi wa mwanzo, Mama Sumayya (RA) na msimamo wa dada yake Umar bin Khataab (RA), yaani Fatma bint Khataab (RA) nk. Vyote hivi ni visa maarufu hata kwa wasiokuwa walinganizi, kwa hiyo sina haja ya kuvirejea.

 Ni jambo la kusikitisha sana kuona wanaume kwamba, tumebeba ujumbe wa Ulimwengu na tunafanya kazi ya kuutawalisha ujumbe huo katika ardhi, huku familia zetu zikiwa hazina tofauti na familia zilizoathiriwa na fikra za kidemokrasia upande wa kimaadili na kiufahamu juu ya dini yao na hata katika ubebaji daawa ya Uislamu. Pia tutambue kuwa pamoja na kiudhahiri baadhi ndani ya Ummah wanatupinga lakini kihakika wanatukubali na kuelewa nafasi yetu katika jamii husika, kwani ujumbe tuliobeba ni ujumbe uko sambamba na maumbile ya binaadamu. Na Ndio maana wanaharakati walinganizi huangaliwa kwa jicho la ziada katika jamii, kwa kuangaliwa pale wanapojikwaa au kukosea jamii huwachukulia kuwa ni kiroja kwa walinganizi kufanya kitendo fulani kiovu. Au pia kuonekana tunalingania lakini ahli zetu na maharimu zetu wanaranda mitaani bila hijabu nk. Hayo ni hoja inayothibitisha kwamba Umma unatukubali kimaumbile kwa kutuona kwamba kwa nafasi yetu hatukustahiki kukosea hata kama makosa mengine ni ya kibinaadamu.

Pamoja na kwamba, wanaharakati sio mashine ambazo hufanya kazi bila khitilafu kwa vipimo vya kihandisi. Kwa kuwa wabeba daawa ni binaadamu kama binaadamu wengine katika jamii, ambao kuna uwezekano wa kukosea, lakini hatuna budi kuwa tofauti na jamii zetu ambazo zimeathiriwa zaidi na fikra za kidemokrasia kuliko za Kiislamu. Kwa sababu sisi ndio wakombozi wao. Kwa maana hiyo, juhudi za makusudi zinahitajika katika kuwathaqafisha ahli zetu hususan maharimu zetu ili waweze kuufahamu Uislamu wao na kutambua majukumu yao, ili waweze kuyatekeleza kikamilifu kwa msukumo wa uchaji Mungu.

Mbinu mbali mbali zinaweza kutumika kufikia huko, kama kuwazungumzia Khilafah na uzuri wa nidhamu yake, ukafiri wa demokrasia na ubaya wa nidhamu yake, kuwaonesha masuluhisho ya Kiislamu katika matatizo yetu hata yaliyomo majumbani mwetu, kuonyesha kwamba matatizo tuliyonayo yamesababishwa na nidhamu inayotutawala, bila ya kusahau kuwaalika mashababati kwa makusudi majumbani mwetu kwa ajili ya kuwachangamsha ahli zetu na maharimu zetu kwa ujumla.

Huu ni wajibu wa lazima tuutekeleze kwa mbinu zilizomo ndani ya mzunguko wetu ikiwemo pia kutenga muda khasa kuwapa thaqafa jumla ya Uislamu, miongoni mwa fikra, hukmu za kisheria, seerah, lugha, tafsiri ya Qur’an nk. Na tusisahau pia kuwajuvya hali halisi/waqia wa mambo yanayotokea katika ulimwengu na masuluhisho yake Kiislamu na kuwakumbusha lengo la kuumbwa kwetu na mahusiano ya maisha haya na yatakayokuja mbele yetu.

Twapaswa tujitambue kwamba, lengo letu ni kufikia kilele cha kuusimamisha Uislamu katika maisha yetu, kwa kuifanya nidhamu ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuhukumu katika maisha haya, hapo itakuwa ni wakati wa kuamrisha mema na kukataza maovu kwa vitendo. Lakini  hata kabla ya kufikia huko, tuna dhamana ya uongozi katika familia zetu, ambao ni uongozi wa kimaumbile tuliopewa na Mwenyezi Mungu (SWT).

Hatuna budi kuwasisitiza ahli zetu na watoto wetu juu ya dhima yao mbele ya Muumba pale wanapokuwa wazito katika utekelezaji wa faradhi hii adhim ya kurejesha Khilafah na faradhi nyengine. Kwani kwa Muislamu hakuna khiyari katika utekelezaji wa maamrisho ya Allah (SWT) na kuacha makatazo Yake.

Kwa kumalizia, jukumu la kurejesha maisha ya Kiislamu kupitia Serikali ya Kiislamu ya Khilafah si jukumu la wanaume tu, bali ni jukumu la kila Muislamu mwanamme na mwanamke, isipokuwa katika yale ambayo ni kikwazo katika maumbile ya mwanamke. Lakini, suala la kuufahamu Uislamu na ukafiri kimfumo, na pia kuulingania Uislamu kimfumo katika mazingira yasiogongana na maumbile ya kike lazima washiriki kikamilifu. Kwa hiyo, hatuna budi kuwachangamsha wanawake katika ahli zetu, maharimu wetu na familia kwa ujumla katika qadhia hii ya kufa na kupona, ili tuweze kuwa na familia ambazo ni kigezo kwa jamii na zilizotofautika na familia zilizoathirika na fikra chafu za kidemokrasia.

Allah Taala Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ (التحريم: 6

“Enyi Mlioamini! Ziokoweni nafsi zenu na watu wenu na moto, ambao kuni zake ni watu na mawe…..”.

(TMQ 66: 6)

Khamis Saleh

Maoni hayajaruhusiwa.