Tumo Katika Ramadhani Na Hali Yetu Bado Ile Ile
بسم الله الرحمن الرحيم
Tunamshukuru Allah Rahima na Rehma zende kwa tumwa Karima, na aali zake Kirama na swahaba zake Adhima.
Amma baada ya hayo,
Tumo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mara nyengine tukiwa hatuna msemaji wala mtetezi anayeweza kutuunganisha kuwa wamoja na kufahamiana hata katika ikhtilafu zetu ndogo ndogo.
Tumo mwezi wa Ramadhani na Ummah wa Kiislamu tukitofautiana katika ibada tukufu ya funga. Baya Zaidi hatutafautiani kwa sababu za ikhtilafu za kifiqihi ambazo kimsingi Uislamu unazikubali, bali kwa michoro ya mistari (mipaka) iliyochorwa na makafiri wakoloni ambao hadi leo ndio wanaoendeleza tofauti hizi na kuzidhamini.
Tumo katika mwezi wa Ramadhani na wengi katika Umma wa Kiislamu wanafunga na hawajui nini watafutari ikifika magharib. Lakini kwa shauku yao ya dini na taqwa yao hufunga hivyo hivyo. Waislamu hao wanyonge wanafunga katika hali hiyo ilhali watawala katika miji ya Waislamu wanavuruga rasilmali za Ummah kwa upuuzi kama inavyofanya Saudia na ajenda yake ya mpira nk. Pia baadhi ya Waislamu walioruzukiwa riziki kunjufu kwa kukosa taqwa wanavuruga na kumwaga vyakula holela. Bila ya kusahau pia baadhi ya maskini wapo waliogubikwa na uroho, kiasi kwamba hata wakipata ziada hawakumbuki kuwagawiya wenzao. Bali kubwa zaidi yote haya ni kwa sababu hatuna Khilafah itakayosimamia mafukara na masikini katika Ummah wa Kiislamu.
Tumo mwezi wa Ramadhani ilhali Waislamu wa Gazza, Yemen, Syria, Somalia, Yemen, Iraq, Turkistan Mashariki, Kashmiri, Sudan nk. wakiendelea kukabiliwa na mateso, mauaji na maangamizi.
Amma Waislamu wa Gazza hata kabla ya kuanza Ramadhani, walishaanza kufunga kwa zaidi ya miezi mitano wakikabiliwa na vita vilivyoambatana na njaa, kiu, maradhi nk. Na vibaraka wa nchi za Waislamu kama Misri, Jordan, Saudia, Iran, Uturuki, Pakistan nk. baadhi wakishirikiana moja kwa moja na mayahudi kuangamiza Gazza, na baadhi wakiwa kimya cha mfu, baadhi wakibwekabweka kwa masuluhisho ya kikafiri na baadhi kama Saudia wamefurutu ada kiasi cha kudiriki hata kukataza kuwaombea dua Waislamu hao wa Gazza wanaoangamizwa. Na ukweli vibaraka hao wanajua fika kuwa suluhisho la Kiislamu na la kudumu ni kupeleka majeshi yao na kuondoa kabisa kijidola cha Israil. Bila ya kutaja kuna maelfu ya Waislamu dunia nzima ikiwemo hapa Tanzania wanaofunga Ramadhani wakiwa wamesekwa magerezani kwa kisingizio cha ugaidi, wakiendelea kushikiliwa bila ya kesi zao kusikilizwa wala kuachiwa huru.
Tumo mwezi wa Ramadhani bado Quran haijafanya kazi kivitendo kuwaongoza watu duniani kama Allah Taala alivyoisifia kuwa ni Muongozo kwa watu wote, na sio kwa Waislamu peke yao. Na ili Quran iwe Muongozo kivitendo ni lazima iwepo dola ya Kiislamu ya Khilafah itakayotawalisha Quran kwa watu wote, huku kwa wasiokuwa Waislamu wataruhusiwa kuendelea na mambo yao ya kiibada, na hawatolazimishwa kuingia ndani ya Uislamu kwa nguvu. Bali watalinganiwa kwa khiyari lakini kutokana na uadilifu na neema ya Uislamu wengi wao wataingia katika dini kwa makundi na kwa khiyari.
Tumo mwezi wa Ramadhani, huku ibada hii ya Swaumu ikitekwa nyara na baadhi ili kumakinisha fikra hatari za kisekula na dini mseto. Fikra ambazo ni za makafiri na hazina nafasi yoyote ndani ya Uislamu. Wanaoidandia ibada hii kwa maslahi ya wanasiasa wa kidemokrasia na kuleta ukuruba baina ya dini wanajua fika kwamba ibada hii ni ya Waislamu na Uislamu na iko kando na wanayoinasibisha, lakini wanatenda hayo kwa dhihaka na dharau na kufurutu uadui wao kwa Umma wetu na dini yao. Allah Taala Anasema:
وَلَنْ تَرْضَى عَنْكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ
“Hawatokuwa radhi juu yako Mayahudi wala Manasara mpaka ufuate mila yao..”(TMQ 2:120)
Tunamuomba Allah Taala Ajaalie Ramadhani ijayo tuwe chini ya bendera moja, dola moja na kiongozi mmoja (Khalifah) atakayetuma majeshi kuwakomboa Waislamu Palestina na Masjid Aqswa, Sudan, Kashmiri, Turkistan ya Mashariki , Mynamar nk. Na pia Khalifah huyo ndie atakaeutangazia Umma wa Kiislamu dunia nzima siku moja ya kufunga na kufungua pasina kuzingatia michoro ya kijahili inayotukhitalifisha iliyochorwa na makafiri wakoloni kwa jina la ati mipaka baina yetu.
Na kauli yetu ya mwisho tunasema Al-hamdulillahi Rabbil-aalaimina
Risala ya Wiki No. 172
6 Ramadhan 1445 Hijria | 16 Machi 2024 Miladi
Afisi Ya Habari – Hizb ut Tahrir Tanzania
Maoni hayajaruhusiwa.