Tuhuma za Ugaidi Zazidi Kuliza Familia

Na Bakari Mwakangale

Taasisi za kutetea haki za Binadamu zimetakiwa kujitokeza na kutoa msukumo kwa Serikali izingatie haki kwa mahabusu wenye tuhuma za ugaidi watekelezewe haki zao za kisheria ili kesi zao zianze kusikilizwa.

Wito huo umetolewa na wawakilishi wa familia tatu ambao ndugu zao wapo mahabusu zaidi ya miaka miwili sasa kwa tuhuma za ugaidi katika Gereza la Lilungu Mkoani Mtwara, huku kesi yao ikitajwa kila baada ya wiki mbili na kurudishwa mahabusu, kwa maelezo kuwa upelelezi haujakamilika.

Akiongea kwa niaba ya wenzake Julai 9, 2020, Magomeni Makuti Jijini Dar es Salaam, Bw. Tiba Moshi Athumani Kakoso, waliojitambulisha kwa majina ya Salum Omar Bumbo pamoja na Faizuna Juma Issa, alisema wanawakilisha kilio kutoka katika familia tatu.

Akiongea mbele ya Waandishi wa Habari, alizitaja familia hizo kuwa ni familia ya Mzee Kakoso, familia ya Mzee Bumbo pamoja na familia ya Bw. Suleiman Mkaliaganda ya Mtwara, ambao kwa ujumla vijana wao walichukuliwa na watu walijitambulisha kuwa ni Usalama wa Taifa, katika mazingira tofauti.

“Tumewaita hapa kuelezea kilio, masikitiko na sononeko letu kutokana na masaibu ya wanafamilia wetu ambao ni Omar Salum Bumbo (51), Ustadh Ramadhan Moshi  Kakoso (41) na Waziri Suleiman Mkaliaganda (33), wote hao wapo mahabusu  katika gereza la Lilungu Mkoani Mtwara kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa.” Amesema Bw. Kakoso. Kutokana na mwenendo wa kesi zote za ugaidi nchini, Bw. Kakosa, akazitaka Taasisi za kutetea haki za Binadamu, kuingilia kati na kuililia Serikali kukamilisiha upelelezi wa kesi hizo ili zianze kusikilizwa.

“Sisi wanafamilia wa watuhumiwa hao watatu tunachukua fursa hii kupitia vyombo vyenu vya Habari, kupaza sauti zetu kuitaka Serikali ambayo imejipambanua kuwa inasimamia haki na kutetea wanyonge, isimamie haki kwa ndugu zetu pamoja na mahabusu wengine kama hao wanaoendelea kusota Mahabusu.”

“Watekelezewe haki zao kisheria ili kesi zao zisikilizwe, kama ushahidi haujakamilika, basi wapatiwe dhamana na kama ushahidi haupo, waachiliwe huru kuliko kuendelea kuwashikilia, hali inayatoa sura ya uonevu kwani uadilifu na haki huzaa furaha na utangamano, lakini dhulma na uonevu huzaa chuki na uadui.” Amesema Bw. Kakoso.

Alisema, ndugu zao walikamatwa kwa nyakati na mazingira tofauti, ambapo wawili walikamatwa Jijini Dar es Salaam, na mmoja Mjini Mtwara kisha kwa pamoja walishitakiwa kwa makosa ya ugaidi.

Akielezea mazingira ya kukamatwa kwa ndugu zao hao alisema, masaibu yalianza kumfika Omari Salim Bumbo, ambaye ni fundi ujenzi na mkaazi wa Tandika Relini, Dar es Salaam, Oktoba 27, 2017. “Alinyakuliwa na kutekwa na wanaoaminika kuwa ni maafisa wa Usalama, baada ya kumpigia simu kwamba angetaka waonane ili kumpatia kazi ya ujenzi na alipofika eneo aliloahidiwa kukutana nae maeneo ya Tabata, alitekwa na kumsweka garini, na kutoweka nae kusiko julikana,” amesema Bw. Kakoso.

Alisema, siku tatu baada ya tukio la kutekwa Omar Bumbo, Oktoba 30, 2017,

Ustadh Ramadhan Moshi Kakoso, ambae ni mwalimu wa dini ya Kiislamu na mfanyabiashara, alitiwa nguvuni akiwa nyumbani kwake Magomeni Makuti, Dar es Salaam, mbele ya familia yake na watu waliojitambulisha kuwa ni maafisa wa Usalama.

Katika tukio hilo, Ustadh Kakoso, na familia yake walitoa shinikizo la kuwataka watu hao kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, ambapo mbele ya Mwenyekiti, walitoa maelezo kuwa taarifa za Ust. Kakoso, zingepatikana katika kituo cha Polisi cha karibu yake. Hata hivyo, alisema kwa wawili hao zilipita wiki kadhaa bila ya  kupatikana taarifa zozote za mahala walipo licha ya jitihada kubwa za familia, ndugu na marafiki kufuatilia katika vituo mbalimbali vya Polisi, Jijini Dar es Salaam, jambo lililoashiria  kutokuwepo kwa nia njema kwa vyombo vya dola dhidi yao.

Alisema, baada ya siku nyingi kupita taarifa za ndugu zao hao ziliibukia Mkoani Mtwara, ambako waliunganishwa na Mwalimu Waziri Suleiman Mkaliaganda, aliye Mwalimu wa Sekondari hapo Mtwara Mjini, aliyekamatwa Oktoba 21, 2017, jirani na nyumbani kwake mtaa wa Kiyangu Mtwara mjini.

Alisema, wakati wao wanahangaika kuwatafuta Jijini Dar es Salaam, walipata taarifa kuwa walishitakiwa kimyakimya Mkoani Mtwara kwa makosa ya ugaidi Disemba 5, 2017. Na kuanzia hapo, alisema Bw. Kakoso, kuwa ndugu zao hupelekwa Mahakama ya Wilaya ya Mtwara kila baada ya wiki mbili kwa ajili ya kutajwa kesi yao na kurudishwa gerezani, kwa maelezo kuwa ushahidi haujakamilika.

(Gazeti la An-nuur, Ijumaa, 17 Julai 2020)

“Bofya Hapa uDownload Pdf”

#KomeshaUkandamizajiWaKisheriaNaUtekaji
#StopOppressiveLawsAndAbduction

Maoni hayajaruhusiwa.