Ni Kipi Kilicho Nyuma ya Oparesheni ya Uturuki “Olive Branch” Kaskazini Mwa Syria?

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali

Imegunduliwa kwamba harakati za Erdogan nchini Syria zimetulia kwa kiasi fulani baada ya oparesheni ya kuhami Furaat na kutelekeza kwa Erdogan mji wa Aleppo, na kuiruhusu serikali kuchukua udhibiti juu ya Aleppo, lakini akaregelea tena oparesheni hiyo kwa jina la ‘Olive Branch’ ikielekea eneo la Afrin tangu Jumamosi, 20/01/2018, kupitia mashambulizi ya anga ya silaha na makombora. Kwa mujibu wa taarifa iliyo tolewa na mkuu wa majeshi ya Kituruki mnamo Jumapili 21/01/2018: oparesheni ya Olive Branch, iliyoanza mnamo Jumamosi kwa mujibu wa mpango wake uliochorwa, na operesheni ya ardhini ikaanza mnamo Jumapili asubuhi. (Chanzo: Turk Press, 21/01/2018) na ambayo inaendelea, sasa ni kipi kilicho nyuma ya oparesheni hii ya “Olive Branch”? Allah akulipe kheri.

Jibu

1- Kabla ya kuanza kuchambua yaliyotokea, ni lazima tutulizie makini jambo moja muhimu mno linalounda msingi wa sera ya sasa ya Uturuki, litakalo angazia juu ya harakati za Erdogan na matendo na taarifa zake, kwa kuwa Erdogan wa Uturuki ni kibaraka waziwazi wa Amerika, anafanya hivyo kwa badali ya usaidizi wa Amerika ili kubakia mamlakani kama ilivyomleta mamlakani. Dalili ya hili ni yale yaliyotajwa na gazeti linalounga mkono serikali ya Uturuki la As-Sabah mnamo 18/4/2017: “Jana usiku Raisi wa Amerika alimpigia simu Raisi wa Uturuki Erdogan kumpongeza kwa matokeo ya kura ya maamuzi ya Aprili 16 juu ya marekebisho ya katiba na nidhamu ya uraisi”.

Erdogan alimtajia kwamba “alianzisha kampeni nzuri kwa ajili yake na kwamba aliisimamia yeye mwenyewe”. Alimwambia Erdogan: “Natilia maanani urafiki wetu na kuna vitu muhimu sana ambavyo tutafanya pamoja”. Hivyo basi sera ya Erdogan nchini Syria kwa kweli ilikuwa ikisaidia mipango ya Amerika ya kumakinisha serikali ya Syria na kushinikiza makundi ya wapiganaji kujiondoa kutoka maeneo muhimu ya serikali hiyo. Mfano wa hili ni agizo la hivi karibuni la kuisalimisha Aleppo, na kuipa uwezo serikali hiyo, alibuni kadhia na kuyaondoa makundi ya wapiganaji yasipigane ndani ya maeneo yao ili yasiizuie serikali hiyo kuingia ndani ya maeneo hayo kwa kisingizio cha vita vya kuihami Furaat. Katika wakati ambapo serikali hiyo ilikwenda Aleppo na kuangazia mashambulizi yake huko, ikijua kuwa vita vya kuihami Furaat tayari vilikuwa vishapata baraka za Amerika, Uturuki iliingia eneo la Jarabulus mnamo 2016 kwa ushajiisho kutoka kwa Amerika wakati aliyekuwa Makamu wa Raisi wa Amerika Joseph Biden alipokuja  jijini Ankara na kutangaza huko uungaji mkono wake wazi kwa kuingia jeshi la Uturuki mnamo 24/8/2016 na kuyataka majeshi hayo ya Uturuki ya vitengo vya ulinzi kujiondoa kutoka kwa majeshi ya Kituruki chini ya jina la ngao ya Furaat. Tumetaja katika Jibu la Swali mnamo 25/9/2016 kwamba: “Ili kuifanya mipango ya Amerika ifanye kazi, inayo angazia Aleppo, vikosi vya Uturuki ni sharti viekewe vizingiti vipya, na hapa Amerika imetumia mashoka mawili kuregesha uvamizi wa Aleppo: Kwanza: kuingiza jeshi la Uturuki kaskazini mwa Syria, kuanzia eneo la Jarabulus huku wakati huo huo Uturuki ikitangaza oparesheni “Kuhami Furaat” na kutoa wito kwa waasi wanaounga mkono Uturuki kutoka kusini mwa Aleppo kupigana na kundi la ISIS, yaani, kudhoofisha maeneo halisi ya mapambano mjini Aleppo! Na kuunda maeneo mapya ya mapigano na kuyasukuma makundi mengi zaidi ya upinzani kutokana na kupigana mjini Aleppo! nk”. Hivi ndivyo namna Erdogan alivyo yaondoa makundi yaliyo na utiifu kwake kwenda kupigana katika maeneo ya Al-Bab na kuiacha Aleppo kuwa karibia huru kutokana na upinzani wowote, isipokuwa kwa waumini wachache waliosimama kidete. Huku haya yakijiri makundi mengi yaliitikia wito wa Erdogan wa kuihami Furaat na anarudia khiyana hii kwa mara nyengine tena.

2- Harakati hizi bado zingalipo zinazoiwezesha serikali ya Syria kuchukua udhibiti wa sehemu muhimu mjini Idlib na kuyaondoa makundi tiifu ya wapiganaji kwa maagizo ya Uturuki kuangazia juu ya Afrin na kusahau ardhi yao asili ya Idlib; ambayo serikali ya kihalifu inaisongelea kwa ushirikiano na Amerika, lakini chini ya kisingizio cha mizozo kati ya Uturuki na Amerika kuzuia matayarisho ya wanajeshi wapya wanao nasibishwa na Amerika! Tambua kwamba Amerika inasongea kutokea Uturuki kuelekea Syria na kuyahami kisilaha makundi yake vibaraka, ikiwemo vitengo vya ulinzi vya Wakurdi, ambao ndio idadi kubwa katika majeshi ya Kidemokrasia ya Syria yanayo nasibishwa na Amerika, ambapo Erdogan alifungua kambi ya Incirlik … Hivyo basi Erdogan anairudia hali ya Kuhami Furaat kurahisisha kuingia kwa serikali hiyo mjini Idlib. Oparesheni ya Olive Branch ilipangwa kurahisisha kuingia kwa serikali hiyo mjini Idlib.

Serikali ya Syria huku ikisonga kuelekea Idlib na kuuzingira uwanja wa ndege wa Abu al-Duhur, Erdogan ameyasukuma mapigano kuelekea Afrin!

Takriban makundi ya upinzani elfu 25 yanashiriki katika oparesheni hii kama ilivyo thibitishwa na kamanda wa kijeshi katika kikosi cha Sham, Yasser Abdul Rahim, kwamba takriban wanajeshi waliojihami elfu 25 kutoka Jeshi Huru la Syria wanashiriki katika oparesheni ya kijeshi ya Uturuki mjini Afrin (Chanzo: Russia Today, 23/1/2018), yanayo julikana na Amerika pamoja na kuyapasisha kwake. Waziri wa Kigeni wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu alisema kuwa alijadiliana na Waziri wa Ulinzi wa Amerika James Mattis juu ya mgogoro wa Syria na kadhia ya vitengo vya usalama mipakani mnamo Jumatatu jioni (15/1/2018) nchini Canada. Alisema kuwa pia alikutana na Waziri wa Kigeni wa Amerika Tillerson mnamo Jumanne jioni (16/1/2018) baada ya mkutano wa Mawaziri wa Kigeni juu ya usalama na uthabiti kwa kisiwa cha Korea jijini Vancouver, Canada. Çavuşoğlu alisema kuwa Mattis alisema:

“Tumeulizwa kutoziamini habari zinazo chapishwa kuhusu (kuundwa kwa jeshi jipya kaskazini mwa Syria),” akiongeza kuwa alikuwa “anaifuatilia kadhia hii yeye mwenyewe na atadumisha mawasiliano yake nasi.” (Chanzo: Anadolu news agency 17/1/2018)

3- Hili linathibitisha taarifa za Amerika katika muda wa siku mbili zilizopita. Yanathibitisha kuwa Olive Branch, kadhia ya Afrin na harakati za jeshi la Uturuki na Jeshi Huru la Syria yote ni kwa kupasishwa kikamilifu na Amerika na Urusi, iliyo ingia Syria kwa ushirikiano na Amerika, hizi hapa ni baadhi ya taarifa hizo:

– Kampeni ya kijeshi ya Uturuki mjini Afrin ilianza jana Ijumaa, kwa hatua za kwanza za mashambulizi ya mabomu kwa baadhi ya maeneo ya Afrin kwa kasi kuu tangu Alhamisi/Ijumaa usiku, kwa kuanza kwa kujiondoa kwa polisi wa kijeshi wa Urusi kutoka Afrin na vitongoji vyake. Nurettin Canikli aliikadiria kama “mwanzo wa mashambulizi ya ardhini,” kwa mujibu wa runinga ya Al Jazeera … Al-Araby Al-Jadeed iligundua kutoka kwa chanzo cha Kituruki kwamba: “Ofa nyengine ilifanywa, kwa ajili ya kuudhibiti mji kwa badali ya makubaliano ya pamoja baina ya Ankara na Moscow katika namna ya usimamizi wao. Serikali ya Kituruki inahakikisha kwa kiwango kikubwa uundaji upya sawia na Kuhami Furaat, na kupitia kwa kushinikiza upinzani nchini Syria kuhudhuria kongamano la Sochi, huku Warusi wakisisitiza juu ya kuukabidhi mji baada ya kuudhibiti kwao na pia kuiruhusu serikali kufanya maendeleo zaidi katika mkoa wa Idlib.

Huku haya yakijiri, Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Nurettin Canikli katika mahojiani ya runinga jana alithibitisha, “Tunajua kwamba Urusi inaisaidia serikali pakubwa” … Ama kuhusu matarajio ya Uturuki ya operesheni hii, chanzo cha Kituruki kiliiambia Al-Araby Al-Jadeed “Oparesheni hii inatarajiwa kuendelea kwa kiwango kisicho zidi miezi mitano hadi sita … Chanzo hicho kilitaja “mikondo hii ya kidiplomasia haikuathiri Washington.” (Al-Araby Al-Jadeed, 20/01/2018)

“Mnamo 20 Januari, Uturuki aliamua kupeleka majeshi yake karibu na Afrin kaskazini magharibi mwa Syria … Moscow ina wasiwasi kuhusu habari hii,” Wizara ya Kigeni ya Urusi ilisema katika taarifa, ikitaja kuwa ilikuwa “ikifuatilia kwa karibu maendeleo ya hali hii.” “Urusi ingali imejitolea katika msimamo wake kuhusiana na kutafuta suluhisho ya mzozo nchini Syria, kwa msingi wa kuhifadhi hadhi ya eneo la nchi hii na heshima kwa ubwana wake,” wizara ilisema). (Chanzo: Rudaw, 20/01/2018)

Amerika inataka operesheni ya kijeshi ya Uturuki kubakia kufungika kiwakati na kieneo, na kushauri “kujizuia kibinafsi” na kuhakikisha kuwa operesheni nyenginezo za kijeshi zinafungika kieneo na kiwakati, ili kupunguza uharibifu kwa maisha ya raia.” Msemaji wa Wizara ya Kigeni ya Amerika Heather Nauert alisema, “Tunaisihi Uturuki kujizuia na kuhakikisha kuwa oparesheni zake za kijeshi zinabakia kufungika kieneo na kiwakati na zenye kuaminika kuepuka majeruhi ya raia.” Waziri wa Ulinzi wa Amerika Jim Mattis alisema mnamo Jumapili kwamba Uturuki iliiarifu Amerika kabla ya hatua hiyo, akitaja kuwa Washington inawasiliana na Ankara kuhusu maendeleo ya hali hiyo. Alisema kuwa Waziri wa Kigeni Sergey Lavrov na mwenzake wa Amerika, Rex Tillerson, wamejadiliana juu ya “hatua ili kuhakikisha kuhifadhi uthabiti kaskazini mwa nchi”. Waziri huyo wa Kigeni wa Uturuki alijadili operesheni ya kijeshi pamoja na mwenzake wa Amerika, lakini bado hakufichua yaliyotokea baina pande mbili hizo. (Chanzo: Shirika la BBC Arabic, 22/01/2018)

Waziri wa Kigeni wa Amerika Rex Tillerson alisema nchi yake inatarajia kufanya kazi na Uturuki kuasisi eneo salama kaskazini magharibi mwa Syria ili kufikia matakwa ya kiusalama ya Ankara… Kinara wa kituo kikuu cha utoaji amri za kijeshi cha Amerika, Jenerali Joseph Votel, alithibitisha kuwa Uturuki iliiarifu nchi yake kwa mukhtasari juu ya oparesheni zake za kijeshi mjini Afrin, akitaja kuwa mji huo hauko ndani ya mipaka ya eneo la oparesheni za kijeshi za Amerika.

Wizara ya Ulinzi ya Amerika inatoa wito wa “kutopalilia mzozo”, ikitaja kuwa inafahamu wasiwasi wa kiusalama wa Uturuki eneo hilo. (Chanzo: Russia Today, 23/01/2018)

– Kituo Kikuu cha Utoaji Amri za Kijeshi cha Amerika kilisema Uturuki iliwaarifu kwa mukhtasari juu ya operesheni ya kijeshi katika mji wa Syria, Afrin, kikisisitiza wakati huo huo kuwa mji huo haumo ndani ya mipaka ya eneo la operesheni za kijeshi. Jenerali Joseph Votel, Kamanda wa Kituo Kikuu cha Utoaji Amri za Kijeshi cha Amerika, katika taarifa kwa vyombo vya habari mnamo Jumapili alisema kuwa nchi yake haitilii makini maalumu kwa eneo la oparesheni za Kituruki. (Chanzo: Quds Press, 21/01/2018)

– Waziri wa Kigeni wa Amerika Rex Tillerson alisema nchi yake inatarajia kufanya kazi na Uturuki kuasisi eneo salama kaskazini magharibi mwa Syria ili kufikia matakwa ya kiusalama ya Uturuki; hii ilikuwa siku ya tatu ya oparesheni Olive Branch iliyo anzishwa na majeshi ya Uturuki na Jeshi Huru la Syria. Eneo la mji wa Syria wa Afrin, Waziri wa Kigeni wa Amerika, “Wacha tuone ikiwa twaweza kufanya kazi na nyinyi ili kuunda aina ya eneo la usalama ambalo huenda mukahitaji… kwa hivyo tuko katika majadiliano na Waturuki na baadhi ya majeshi yaliyoko uwanjani pamoja na vipi tunaweza kutuliza hali hii na kutatua wasiwasi wa Uturuki kwa usalama wao.” (Chanzo: Turk Press, 23/01/2018)

– Na taarifa za Waziri wa Kigeni wa Amerika Rex Tillerson juu ya tangazo la nia ya nchi yake ya kuunda jeshi la wapiganaji elfu 30, ambao kazi yao ni “kulinda mpaka,” iliyo ikasirisha Ankara na kumfanya Tillerson kutoa maoni kwa maripota waliokuwamo ndani ya ndege ya serikali ya Amerika, “Nchi hii haina nia ya kubuni jeshi lolote la mipakani nchini Syria”.

Akiongeza kuwa kwa mujibu wa Anatolia, nchi yake inatoa ufafanuzi kwa ripoti za mashirika ya habari ya Uturuki za kuhusu nia ya Amerika kubuni jeshi la usalama mipakani nchini Syria, kwa hili, Nauert alisema, “Wapigeni vita kundi la ISIS, na hiyo ndio sababu halisi ya kuweko kwetu huko, na hiyo ni moja kati ya vitu ambavyo Waziri na wengineo katika Wizara ya Kigeni wameangazia kwa maafisa wa Kituruki.” (Chanzo: Orient, 19/01/2018)

– Jumanne iliyopita, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Amerika Eric Bahon alisema nchi yake imefahamu wasiwasi wa Uturuki kuhusu jeshi la usalama mipakani inayopanga kuliunda nchini Syria, akitaja kadhia hii kwa maafisa wa Kituruki.

Bahon alitaja kuwa nchi yake iko katika mawasiliano ya karibu ya kila mara na Uturuki; mshirika wake katika NATO. Bahon alitumia maneno “jeshi tarajiwa la usalama mipakani” katika jibu lake … leo, Alhamisi, Waziri wa Kigeni wa Amerika Rex Tillerson alikuja kutangaza kwamba Amerika haikuwa na mipango ya kubuni jeshi lolote la mipakani nchini Syria, akitoa maoni juu ya ripoti za habari za kadhia hii. Aliongeza katika taarifa kwa vyombo vya habari: “Kadhia hii inahisiwa na kufafanuliwa kwa njia ya kimakosa, na baadhi ya watu wamezungumza kwa njia ya kimakosa, hatuundi jeshi lolote mipakani”. (Chanzo: Yenisafak Arabic, 17/01/2018)

Ni wazi kutokana na taarifa zilizopita kuwa Olive Branch ni tawi linalo bebwa na Uturuki kwa ushirikiano na Amerika na Urusi … na kwamba taarifa za Amerika mwanzoni mwa kubuniwa wanajeshi wa mipaka elfu 30 zilikuwa ni kuhalalisha tu operesheni ya Afrin, Amerika kisha ikabadilisha taarifa hiyo kwa namna ya kukataa wazi baada ya lengo lake kupatikana!

4- Hivyo basi, hatua za Uturuki nchini Syria ni za kutumikia miradi ya Amerika kwa kupanda nidhamu ya kisekula nchini Syria. Taarifa hizo za kelele kutoka kwa Erdogan ni kwa lengo tu la kuhadaa wajinga miongoni mwa watu kwa maneno makali na taarifa tasa zisokuwa na vitendo, kama wakati aliposema, hatutaruhusu Hama nyengine; lakini serikali hiyo ikatekeleza katika kila jiji na mji zaidi ya yaliyo fanyika Hama … pamoja na harakati bandia zisizo zalisha vitendo vya kiikhlasi. Aliwahadaa watu kwa taarifa za kupotosha zilizo wafanya wapumbavu wajinga miongoni mwa watu kama alivyosema kuhusu uamuzi wa Trump wa kuitambua Al-Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa umbile la Kiyahudi. Erdogan alitishia kukata mahusiano yake na umbile hilo la Kiyahudi endapo Jerusalem itatambuliwa kama mji mkuu wa umbile hili. Lakini hakukata mahusiano yake na Amerika iliyochukua uamuzi huu, bali badala yake inalisaidia umbile hili la Kiyahudi na kulipatia kila kitu kudumisha uhai wake. Pia alitoa wito wa suluhisho la Kiamerika la dola mbili, linalojumuisha kugurisha asilimia 80% ya Palestina kwa Mayahudi, na kutoa wito wa Jerusalem Mashariki kuwa mji mkuu wa Palestina, akiisalimisha Jerusalem Magharibi kwa Mayahudi hao. Hii ni kwa kuongezea yale aliyo yafanya na anayo endelea kuyafanya nchini Syria, na hata khiyana zake, zilizotilia nguvu uwepo wa maadui wa Kirusi na Kiamerika na serikali ya Syria, ima kupitia kuikabidhi Aleppo au kufungua kambi za Kiamerika ili kuingilia kati nchini Syria au kufungua anga ya Uturuki kwa ndege za Urusi au mikutano ya Astana, ambayo aliwashinikiza viongozi wa makundi ya kisilaha kukubali maamuzi yao na kuleta utulivu katika viwanja vya kivita na kupoza na kujiondoa kutoka maeneo na kuyasalimisha kwa serikali na kisha kuizingira Idlib na maeneo mengine zaidi. Hatimaye ikaja sura hii ya “Olive Branch” ili kuirahisishia serikali kuingia Idlib!

Mwisho, tunayahutubia makundi yote kwa kusema musidanganyike na vitendo vya Erdogan, na musiisalimishe Idlib kwa serikali … na wala musisahau yale yaliotendeka kwao mjini Aleppo, lakini kumbukeni hadith iliyo simuliwa na Bukhari kutoka kwa Abu Hurayrah (ra) kutoka kwa Mtume (saw) aliyesema:

»لَا يُلْدَغُ الْمُؤْمِنُ مِنْ جُحْرٍ وَاحِدٍ مَرَّتَيْنِ«

“Muumini hang’atwi mara mbili ndani ya shimo moja”. Sembuse kung’atwa mara nyingi?

(إِنَّ فِي ذَلِكَ لَذِكْرَى لِمَنْ كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ)

“Hakika huo ni ukumbusho kwa yeyote mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.” [Qaf: 37]

7 Jumada I 1439 H

24/1/2018 M

Inatoka Jarida la Uqab: 15.    https://hizb.or.tz/2018/04/01/uqab-15/

Maoni hayajaruhusiwa.