Nani Hukabidhiwa Zakat Kwa Kutokuwepo Dola Ya Kiislamu?
بسم الله الرحمن الرحيم
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh,
Sheikh wetu, kuna mzozo juu ya nani akabidhiwe zakat? Kwa serikali ambapo inajulikana kwamba haitoitumia kwa matumizi yake maalum au isambazwe kwa masikini na mafakiri? Tunataraji utatupatia ufafanuzi pamoja na kutaja dalili zake.
Allah akulipeni kheri.
Ndugu yenu Muhammad Adil Jamil
Jawabu:
Umesahau kuanza swali lako kwa Salam. Lakini sisi tunakutakia kheri, tunajisalimu wenyewe kwa niaba yako! Na kama uonavyo tunakurejeshea Salam… Waalaykum Salam Warahmatullah Wabarakatuh
Kuhusu zakat katika Uislamu hutekelezwa kama ifuatavyo:
1-Zaka ya dhahabu na fedha (pesa) inafaa kumkabidhi anayehusika na zaka katika Dola nayo (dola) itawafikishia inayowastahikia. Na inajuzu kwa yule mtoaji kuwapa inaowastahikia, nao ni mbea/aina nane zilizotajwa katika Aya Tukufu “Hakika ya zaka ni kwa ajili ya mafakiri, masikini, wanaoitendea kazi, wenyekuzoeshwa nyoyo zao, watumwa wanaohitajika kukombolewa, wenye madeni, katika njia ya Allah (Jihadi), na aliyekatikiwa na safari, hiyo ni faradhi kwenu kutoka kwa Allah. Na Allah ni mjuzi na mwenye hekima”
2-Zaka ya wanyama, mazao (nafaka) na matunda hukabidhiwa muhusika wa zaka katika Dola na yeye ataifikisha kwa inaowastahikia. Na wala haifai kutolewa zaka yake (aina hii) kutoka kwa mwenye ile zaka (yaani mtoaji) isipokuwa kwa njia ya Dola.
3-Lakini yote haya pindi tu ikiwa Dola ya Kiislamu ipo, Allah atakapoupa faraja ummah wa kiislamu kuuondoshea mashaka na kuunusuru kwa kusimamisha Khilafah Rashida, basi wakati huo zaka ya wanyama, mazao na matunda itatekelezwa kwa njia ya Dola kama ni wajibu (wujuuban) na sio kwa njia ya mtu binafsi mmoja mmoja. Ama kutoa zaka ya dhahabu na fedha (pesa) na biashara inafaa kuitoa kwa njia ya Dola au njia ya mwenye nayo moja kwa moja.
4-Ama hivi sasa kwa kuwa hakuna Dola ya Khilafah ambayo inatekeleza ahkam za kisharia, kwahiyo, watu binafsi mmoja mmoja watatoa zaka ya mali zao ikiwa za wanyama au mazao au matunda au biashara au dhahabu na fedha, watazitoa watu binafsi mmoja mmoja moja kwa moja kuwapa zinaowastahikia kwa mujibu wa ahkam za sharia na watahakikisha hilo. Na Allah ndie mwenye kuwafikisha.
Yameelezwa yafuatayo katika kitabu cha Al Am-wal, mlango wa kutoa zaka kwa Khalifah uk:170: (Hutolewa zaka ikiwa ya wanyama, au mazao, au matunda au pesa, na mali ya biashara kwa kupewa Khalifah au aliye kwa niaba yake miongoni mwa mawali na ma-amil au anaowateua katika waandishi na wakusanyaji wa zaka. Amesema Allah Mtukufu:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ
“Chukua katika mali zao zaka uwatoharishe na uwasafishe kwayo na waombee dua, hakika dua yako ni utulivu kwao” (Tauba: 103).
Hakika Allah amemuamrisha Mjumbe wake katika Aya hii achukue zaka kwa wenye mali, na alikua Mjumbe (SAAW) akiteua mawali, ma-amil na waandishi wa zaka ili waichukue kutoka kwa wenye mali, kama alivyokua akiwateua wakadiriaji wakadirie mitende na mizabibu. Watu wakati wa Mtume (SAAW) walikua wakimpa yeye zaka au wale anaowateua katika mawali ma-amil na waandishi wa zaka…
Na zimepokewa riwaya kadhaa kutoka kwa masahaba na matabiina za kujuzisha mtu mwenyewe kugawa zaka na kuziweka katika sehemu zake katika mali zisosema (asswamitah) yaani pesa. Hakika amepokea Abu Ubaid ya kwamba Kaisan alikuja kwa Umar na dirham mia mbili za zaka, na akamwambia: “Ewe Amiir Almu-uminuun hii ndio zaka ya mali yangu” Umar akamwambia: “Nenda nayo wewe ukaigawe”. Kama vilevile alivyopokea Abu Ubaid kutoka kwa Ibn Abass kauli yake: “Ukiiweka wewe katika sehemu zake na hukumhesabia (hukumpa) chochote kati yake ambao unawasimamia (watu wako wa nyumbani), basi hakuna kosa”. Na pia pamepokelewa kutoka kwa Ibrahim na Al-Hassan wamesema: “Iweke sehemu zake na ifiche”. Haya ni katika visosema (asswaamit) yaani pesa. Ama wanyama, mazao na matunda hapana budi kuzitoa kwa Khalifah au kwa anaowateua. Abu Bakr amepigana vita na wazuiaji wa zaka wakati walipojizuia kuitoa kwa mawali na waandishi ambao amewateua. Na akasema: “Naapa kwa Allah lau kama watanizuia kamba ya kufungia mnyama wasinipe na ambayo walikuwa wakiitoa (kama zaka) kwa Mjumbe wa Allah (SAAW) basi nitapigana nao vita kwayo”. Wamekubaliana Bukhar na Muslim kwa njia ya Abu Huraira).
Ndugu yenu Ata Ibn Khalil Abu Rashtah
22, Ramadhan, 1438H
17, June 2017
Maoni hayajaruhusiwa.