Kumpa Zawadi Mnunuzi Anaponunua Bidhaa kwa Bei Maalum

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakaatuh

Mwenyezi Mungu akufungulie sheikh wetu Ata Bin Khalil Abu Rashtah na twambuomba Mwenyezi Mungu Azza wa Jallah awarahisishie kwenu wenye nguvu na ulinzi wamchao Mwenyezi Mungu, na wasafi. Swali langu sheikh wangu mheshimiwa ni:

Baadhi ya wenye biashara hufanya aina fulani ya matangazo, ambayo kiufupi huwa hivi:

Kwamba mtu akinunua hapo bidhaa yenye kulingana na kiasi cha riyal ishirini, basi katika hali hiyo mnunuzi ataingia katika droo isiyojulikana ili ajishindie zawadi.

Sasa swali: Je, hayo matangazo yanaingiliwa na uharamu? Ama yafaa?

Na mteja akishasajiliwa na mwenye biashara (katika droo hiyo) bila yay eye mwenyewe kujua, je mteja ataingia katika haramu? Ama uharamu utakuwa tu kwa mwenye matangazo? Mwenyezi Mungu awabariki na atukusanye katika kuwapa bay-ah ndani ya Bait al-Maqdis hivi karibuni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh

Tuliwahi kutoa jibu kwa mfano wa hili swali mnamo 14/5/2007 na nitakunukulia:

[Kwa hakika, bei ya gharar (udanganyifu) ni batili; kwani, bidhaa inayonunuliwa ni lazima ijulikane. Kwa hiyo, pindi itakapokuwa bidhaa yajulikana basi mauzo yataswihi; na la si hivyo basi kutojulikana kwa bidhaa kunabatilisha mauzo.

Ama hali ambazo umezitaja, zinatafautiana katika uhalisia wake, na hivyo kutafautiana pia katika hukmu zake:

1- kumpatia ziada ama zawadi n.k anayenunua kiasi maalumu:  hili laruhusiwa. Mauzo ni sahihi, na ziada inaingia chini ya (mlango wa) zawadi, nayo ni sahihi.

2- Na kuweka zawadi maalumu kwenye bidhaa maalumu iliyotundikwa, kama vile: saa za watoto… ama kuweka ndani yake karatasi iliyoandikwa jina la zawadi ili mnunuaji atakayeipata kwenye bidhaa basi aende kwa mfanyibiashara akachukue tunu ama zawadi yake maalumu iliyokuwa imeandikwa kwenye ile karatasi: hili pia laruhusiwa. Mauzo ni sahihi maadamu bidhaa iliyonunuliwa yajulikana, mfano (sanduku la Kleenex ndani yake kuwe na box la zawadi) kwa hiyo, mauzo yatakuwa sahihi, kwa sababu mnunuzi ametoa thamani ya mfuko wa Kleenix na akapata ndani yake saa, na itakuwa ni zawadi yake, na kama hakupata pia ni sawa, kwa sababu yeye alinunua mfuko wa Kleenix na akatoa thamani yake, na muuzaji halazimishwi kutoa zawadi kwa huo ununuzi. Hivyo mnunuzi akipata zawadi ni sawa na asipopata pia ni sawa.

3- Ama kuuza sanduku iliyofungwa ambayo haijulikani kilichomo ndani, ambapo huenda likawa tupu, ama mkawa na kitu chenye thamani zaidi ya thamani anayolipa, au mna kitu chenye thamani sawa na aliyolipa, au chini zaidi ya aliyolipa… uuzaji huu ni wa udanganyifu, nao hauruhusiwi.

4- Na kuweka namba kwenye bidhaa maalumu na akaelekezwa atakayenunua kuingia kwenye kushiriki kujishindia zawadi, kwa hali hii lenye nguvu ni kwamba itaingia katika mlango wa kamari na hiyo ni kwa sababu, kamari huwa ni “mshindi kuchukua kutoka kwa aliyeshindwa” na jambo lolote ambalo watashiriki ndani yake pande tofauti kwa namna ambayo mshindi atachukua kitu kutoka kwa aliyeshindwa basi itaingia kwenye kamari.

Lau watu watacheza karata na mshindi akachukua kitu kutoka kwa walioshindwa, basi hiyo itakuwa ni kamari na ni haramu. Na kwa mfano, wakishindana watu wawili juu ya farasi, au baiskeli, au magari… na mshindi katika mashindano akachkua kitu kutoka kwa walioshindwa basi itakuwa ni kamari. Na (mfano) watu kumi wakiweka majina yao kwenye makaratasi au namba, kisha wakayatia ndani ya sanduku, halafu wakatoa karatasi moja na mshindi akachukua kitu kutoka kwa wale ambao majina yao hayakutoka, basi hiyo itakuwa ni kamari, nayo ni haramu… n.k

Na sasa hebu tuje kwa namba zinazowekwa katika bidhaa zinazonunuliwa na kisha kushindaniwa. Lenye nguvu ni kuwa, muuzaji huwa ameweka hisabuni thamani ya zawadi. Kwa mfano: zawadi inayoshindaniwa thamani yake ni dinar elfu moja, na nambari yake ni (50) hivyo ataweka namba yake katika kila furushi elfu kumi yaani… ataweka kwenye hili 1 na lile 2… hadi 10,000 ndani yake mutakuwa na nambari (50) naye ataingiza thamani ya zawadi (dinari elfu) kwenye bei ya vile vifurushi. Kwa hiyo badala ya kuuza bei ya kifurushi kwa dinar moja, yeye atakiuza kwa ziada ya qirsh kumi, na wakati wa shindano baada ya kuuza vifurushi elfu kumi atakuwa amezidisha 10,000 × qirsh kumi… yaani, dinar elfu moja= thamani ya zawadi atakayompa mshindi. Kwa hiyo, mshindi atakuwa amechukua zawadi kutoka katika mali za waliopata hasara ya namba, ingawa hilo halitangazwi.

Na hapa huenda mtu akasema: “Kwa hakika muuzaji anauza bidhaa uuzaji wa kawaida tu, kama vile lau hakuweka namba ya kushindaniwa kwa zawadi, ili kuwashajiisha wanunuzi na kuwavutia kununua bidhaa yake, na wala yeye hatii hisabuni kupata thamani ya zawadi kutokana na bei iliyogawanywa”. hilo pamoja na kuwa lawezekana… yaani, kwamba zawadi inawekwa bila kuzidishwa bei kwa ajili tu ya kuwavutia wateja. Lakini huo ni uwezekano dhaifu, hasa pale inapokuwa zawadi inayoshindaniwa ni kubwa, kama vile gari au mfano wake…

Na vyovyote itakavyokuwa, zawadi kama haitokuwa kutokana na namba zinazopata hasara, basi itakuwa katika mambo yenye shubha (utata).

Kwa hiyo, mimi nawashauri ndugu wanaonunua bidhaa zenye namba wasishiriki kwenye mashindano, na wararue namba zinazopatikana kwenye bidhaa, ili shetani asije akawadanganya wakajishughulisha na shidano.

27/rabiul akhir/1428 sawia na 14/5/2007] Mwisho.

Na kama unavyoona, kwa hakika linalotilia nguvu ni kwamba, muuzaji huwa anazidisha kwenye thamani ya bidhaa kitu kitakachofidia thamani ya zawadi kwa uchache. Hivyo, mshindi wa gari (zawadi) atakuwa ameipata kutokana na ziada ambazo wamezibeba wale wenye namba zilizopata hasara. Kwa hiyo, ninalotilia nguvu ni kwamba huu muamala haufai… na kwa uchache – kama nilivyotaja huko juu- huo muamala utaingia kwenye mambo yenye shubha (utata) na muumini hujiweka mbali na mambo yenye shaka ndani yake. Amepokea At-Tirmidhi na akasema: hii ni Hadith Hasan Sahih, kutoka kwa Abu Al-Hawra Al-saa`di akisema: Nilimuuliza Al-Hasan bin Ali: Umehifadhi nini kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw)? akajibu: Nilihifadhi kutoka kwa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema:

«دَعْ مَا يَرِيبُكَ إِلَى مَا لَا يَرِيبُكَ فَإِنَّ الصِّدْقَ طُمَأْنِينَةٌ وَإِنَّ الْكَذِبَ رِيبَةٌ»

“Acha jambo linalokutia shaka, na ufanye lisilokutia shaka. Kwani hakika ukweli ni utulivu, na uongo ni shaka”.

Lakini, ikiwa wewe umekinai kwamba, muuzaji hakuzidisha katika bei ya bidhaa kwa kiasi cha thamani ya zawadi, bali ametoa zawadi hivi tu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu iwe tunu kwa watu ili tu atangaze bidhaa! Basi hapo patahitajika utafiti mwengine…!

Natumai hayo yanatosheleza na Mwenyezi Mungu Ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye hekima zaidi.

Ndugu Yenu

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

29 Muharram Al-Haram 1443 H

6/9/2021 M

Maoni hayajaruhusiwa.