Israi na Miiraj Itusukume Kusimamisha Khilafah Tuikomboe Al-Quds

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَى بِعَبْدِهِ لَيْلاً مِنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ
‘Utukufu ni wake Yeye ambae amempeleka mja wake usiku (mmoja tu) kutoka msikiti mtukufu (wa Makka) mpaka msikiti wa mbali (Baytul-Muqadas) ambao (tumeubariki) na kubariki vilivyoko pembezoni mwake, ili tumuoneshe baadhi ya aya zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na kuona’. (Tmq 17:1)

Allah Ta’ala anatangaza katika aya hii akianzia kujitakasa kwa utukufu wake: Kwamba ni Yeye ndie aliyemchukuwa Mtume SAAW kumpeleka safari tukufu ya Israi na Miiraj. Safari iliyoanzia Masjid Al-Haraam Makka hadi msikiti mtukufu wa Al-quds katika Biladi Shaam. Ni msikiti uliobarikiwa na pia kubarikiwa eneo la pembezoni mwake ambalo ni eneo lote la Biladu Shaam.

Licha ya kuwepo aya hii na nyenginezo pamoja na makumi ya hadithi kuthibitisha wazi wazi utukufu wa msikiti wa Al-quds kuwa ni miongoni mwa misikiti mitukufu, kampeni kali ya makafiri kwa kuwatumia baadhi ya mashekhe na watawala vibaraka katika nchi za kiislamu huudogosha msikiti wa Baytul Muqadas kiasi cha kuuonesha msikiti huu ni msikiti sawa na misikiti miengine. Kitu ambacho si sawa kabisa! Kampeni hii hufanywa kwa kutumia mbinu za namna mbili.
Kwanza, wanaionesha na kuitangaza qadhia ya Palestina kuwa ni tatizo la wapalestina peke yao na sio qadhia ya umma mzima, hivyo mustakbali wa msikiti wa Baitul-Muqadas umo mikononi mwa watu wa Palestina peke yao. Pili, kitendo cha watawala wa Saudia kujipachika cheo bandia cha ‘utumishi wa Haraam mbili’ (Hadimu-ul Haramayn) wanakusudia kuujenga umma na kupandikiza fikra kwa Waislamu kwamba Haraam zipo mbili tu, yaani Masjid ul-Haraam ya Makka na Masjid Nabawi ya Madina, huku watawala hao vibaraka wa Saudia wanashiriki kikamilifu katika kuhakikisha mchakato wa amani baina ya waislamu wa Palestina na kijidola cha mayahudi ili kuimakinisha dhulma ya mayahudi ikiwemo kuendelea kuishikilia ardhi tukufu ya Waislamu pamoja na msikiti wa A-quds ambao ndio Haraam ya tatu.

Eneo lote la Alquds lina historia ndefu tangu zama za Mitume waliotangulia ikiwemo wakati wa Mtume Suleiman AS. na wengineo. Amma Msikiti huu na eneo lake licha ya kuwa Mtume SAAW alianzia safari yake ya Israi, lakini uliingizwa rasmi chini ya usimamizi wa dola kwa kukombolewa katika Khilafah ya Umar ra. ndani ya mwezi kama huu wa Rajab mwaka wa 28 Hijria sawa na mwaka 638 miladi. Kamanda mahiri na jasiri wa dola ya kiislamu Amru ibn al Ass aliongoza mapambano ya kuukomboa mji wa Aelia, na kutokana na uadilifu na utukufu wa Uislamu, wakaazi wake kwa ridhaa za nafsi zao chini ya Askofu wao Mkuu Bwana Sophronius wakajisalimisha bila ya mapigano kuwa chini ya kivuli cha Khilafah na kulikabidhi eneo lao rasmi kwa mkataba. Khalifa Umar ra. akafunga safari ndefu yeye binafsi kuja kulishuhudia tukio hilo kubwa na tukufu kwa macho yake na kuswali katika eneo alipowasalisha Mtume SAAW mitume wote , na kuandika mkataba wa aina yake wa kihistoria unaosomeka:

KWA JINA LA ALLAH, ARRAHMAN, ARRAHIYM
Huu ni waraka wa mkataba kutoka kwa Umar Mtumwa wa Allah, Amiri wa Waislamu, kwa watu wa Aelia. Anadhamini kwao usalama wa maisha yao, mali zao, makanisa yao na misalaba yao…Makanisa yao yasivunjwe wala yasiondoshwe, na kisiondoshwe chochote katika vitu vyao.Wasilazimishwe katika mambo ya dini, na asidhuriwe yoyote. Asiwepo yahudi yoyote pamoja nao ndani Aelia, na watu wa Aelia watalipa jizya kama wanavyolipa watu wa miji mingine”

Katika zama zote baada ya ukombozi huu, Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika manaswara ambao hawakuwa maadui wa wazi kwa Waislamu waliishi katika eneo hili kwa raha mustarehe. Waislamu walikuwa wakiuzuru Batul-Muqadas kama shaair yao kwa kufanya ibada ndani yake bila ya pingamizi wala bughza. Hali iliyoendelea mpaka katika mwaka wa 1099 AD. walipovamia washenzi wa vita vya msalaba kwa kufanya unyama usiomithilika, kupora na kuinajisi Alquds na kuliingiza eneo zima katika mamlaka yao.

Kutokana na shauku ya Waislamu kupigana jihadi na kukomboa miji yao na hususan maeneo matukufu. Katika mwaka wa 1187 AD baada ya Waislamu kupigana kwa karibu karne nzima waliweza kuirejesha tena Alquds katika himaya yao na kuwafukuza makafiri kwa aibu, fedheha na idhilali chini ya Jemadari na miongoni mwa mashujaa wa umma huu Salahudin Ayoub (Allah Amrehemu)

Matukio ya kuanza kudhoofika Khilafah na kupelekea kuangushwa rasmi dola ya mwisho katika mwaka 1924 yalipelekea majanga na misiba mikubwa kwa Uislamu na waislamu kijumla. Moja kati ya misiba hiyo ni kuchukuliwa tena Al-quds na eneo lake lote kuingia katika mikono najis na miovu ya makafiri. Hali hiyo ilianzia katika mwezi wa Disemba mwaka wa 1917 wakati eneo la Palestina lilipochukuliwa kwa mabavu na Uingereza chini ya Allenbye kwa baraka za Jumuiya ya League of Nation. Hali hiyo iliendelea mpaka katika mwaka wa 1948 waingereza walipowakabidhi makafiri wenzao wa kiyahudi kwa baraka kamili za ‘Tamko la Balfaour” na kuhalalilishiwa zaidi na Azimio la Umoja wa mataifa.

Tangu wakati huo mpaka leo Waislamu wanaoishi katika eneo hilo pamoja na msikiti wa Alquds wamesibiwa na kila aina ya vituko na dhulma kutoka kwa mayahudi kwa msaada wa madola ya kibepari ya Magharibi hususan Marekani na Uingereza. Wanauwa, kunyanyasa Waislamu, kuchimba mashimo katika eneo la msikiti ,kuvuruga eneo lake na kueneza najsi katika eneo tukufu kwa kutenda ufisidifu mkubwa usiomithikia.

Miongoni mwa matukufu ya msikiti wa Alquds ni kule kuwa msikiti wa tatu kwa utukufu baada ya Masjidul- Haraam wa Makka na Masjid Nabawi wa Madina. Msikiti huu pia ndio kibla cha mwanzo cha Waislamu. Kadhalika ni msikiti wa pili kujengwa baada ya Masjid ul- Haraam. Msikiti uliojengwa miaka 40 tu baada ya kujengwa Masjid-ul Haraam. Kadhalika Masjid Al-aqswa una kheri ziada kama ilivyotaja quran tukufu kwamba ni msikiti uliobarikiwa na kubarikiwa vilivyo pembezoni mwake. Kwani msikiti huu ndio kituo cha safari ya Mtume SAAW kwenda safari tukufu ya miiraj, ndipo mahala aliposwalisha Mtume SAAW Mitume As. wote. Ardhi yake ndiyo ardhi atakayotokea tena Issa As, ni eneo ambalo Mtume SAAW amebashiri kuibuka kundi litakalosimama kidete kuupigania Uislamu mpaka kupata nusra ya Allah Ta’ala, ndio makao makuu ya Khilafah ya mwisho, ardhi yake ndiyo itakayofufuliwa watu, na mwisho hili ni eneo lililotumwa mitume wengi.

Baada ya kuyataja baadhi ya matukufu ya Al-aqswa tuikumbukeni kauli tukufu ya Allah Taala aliposema:

ذَلِكَ وَمَنْ يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّهِ فَإِنَّهَا مِنْ تَقْوَى الْقُلُوبِ
Namna hii anayeziheshimu alama za (dini ) Mwenyezi Mungu, basi hilo ni jambo la uchaji Mungu wa moyo” (TMQ 22:32)

Kwa aya hii, dini yetu inatulazimu tuyatukuze matukufu ya dini yetu na kuyapa hadhi inayostahili, kuanzia misikiti hususan misikiti mitukufu, Kaaba na meneo yake kama swafah na marwa, siku na miezi mitukufu, kitabu chetu cha quran pamoja na Mitume wetu As.
Moja katika Shaair za dini yetu ni huu msikiti wa Masjid al-Aqswa. Tunalazimika tuutukuze kwa kuswali ndani yake, kuuzuru na kulizuru eneo lake. Lakini hayo yatawezekana vipi ilhali leo msikiti huu mtukufu na eneo la kando yake lililobarikiwa liko chini ya makucha ya kidola dhaifu cha mayahudi?

Ili kuweza kuipa Al-aqswa haki inayostahiki kama shaair nyengine, kitu kisichowezekana chini ya utawala usiokuwa wa Kiislamu hususan utawala wa kiyahudi ulipo sasa. Hivyo ni wajibu na inatubidi tukiwa umma bora tuukomboe msikiti huo.

Katika mwezi kama huu mtukufu wa Rajab tunaposoma kisa kitukufu cha ‘Israi’ na ‘Miiraj’ itulazimu kuona moja kwa moja ufaradhi wa kuikomboa Al-aqswa na kuirejesha katika mikono ya Waislamu, na hilo litawezekana tu kwa kuirejesha tena Khilafah itakayoyaunganisha majeshi ya nchi za Kiislamu kuwatia adabu maadui wa Allah na Mtume wake na kuwarejeshea Waislamu amani na furaha ya kweli na Shaair zao zote.
#RajabFarajaKwaWalimwengu

Na Ishaq Makame

Maoni hayajaruhusiwa.