Furaha na Mafanikio Halisi
Jumla ya wanadamu kila umuonaye anakwenda mbio huku na kule. Si tajiri wala masikini iwe ni mchana au usiku wote wanajituma kupita maelezo wakitafuta furaha na mafanikio. Ili tupate kuelewa mbio zao ni lazima tupate maana halisi ya furaha na mafanikio. Na ili tupate maana ya sawa ya maneno haya hatuna budi kurudia itikadi ambayo ndiyo msingi wa kupima usahihi na ubatili wa maana ya neno lolote lile. Kwa kuwa sasa tunatawaliwa na mfumo wa kirasilimali unaotokamana na itikadi ya Usekula (kutenganisha dini na maisha) iliyo mchanganya mwanadamu kwa kutomjibia kikweli maswali yake msingi nayo ni nini ulimwengu, binadamu na uhai? Badala yake ikamuachia kila mmoja kujijibia mwenyewe anavyotaka kwa kipimo cha manufaa/maslahi. Itikadi hii ikampa mwanadamu nguvu na mamlaka ambayo asili ni ya Allah (swt). Nguvu hizi ni pamoja na kutunga sheria kwa mujibu wa akili yake finyu ili kusimamia mambo ya wanadamu jumla. Itikadi hii haikutosheka na kumpa mwanadamu mamlaka bali ili mfafanulia kuwa lengo la kuishi hapa duniani ni kushibisha matamanio ya kiwiliwili chako kwa kiwango cha juu uwezavyo.
Na kwamba furaha inatokamana na uhuru mwanadamu aliokuwa nao katika kufanya atakavyo wakati wowote. Na kwamba aliye fanikiwa ni yule aliyefikia upeo wa juu katika kushibisha matamanio yake!
Kwa maana hiyo, utawakuta wanadamu waliobeba itikadi ya kisekula wakienda mbio zisizo na kikomo wakiamini kuwa kufanya hivyo kutawawezesha kumiliki mali nyingi zitakazo wawezesha kukimu matamanio ya viwiliwili vyao na hatimaye kuwa na furaha na mafaniko. Lakini hali ni kinyume kutokana na kuwa itikadi hiyo inakwenda kinyume na maumbile ya mwanadamu. Hali ni mbaya na yenye kukatisha tamaa kwani wafuasi wa itikadi hii wamekuwa duni kuliko hata wanyama. Kwani kumeshuhudiwa watu wanaomiliki chungu ya mali/pesa lakini bado wanataka kuwaibia walala hoi, kuna ambao wamekuwa na mali/pesa lakini bado wana wasiwasi kwamba zitawaondokea na hivyo kila kukicha wanalaghai kuhakikisha wanaziongeza mali/pesa zao na wengine kufikia viwango hata vya kuwafanya wazazi wao (mama zao) kama wake zao, wengine watoto wao kama waume au wake zao! Nao wanaume wakiolewa na wanaume wenzao na ilhali wanawake wakiolewa na wanawake wenzao! Kwa muonekano wa nje wafuasi wa usekula wanaonekana kama watu waliostawi na wanaostahili kuigwa lakini kwa sura ya ndani ni watu waliokata tamaa na maisha na waliojawa na msongo wa mawazo kupindukia kiasi kwamba wengine hufikia hata kujiua kwa mikono yao!
Kwa upande wa pili; tunayo Itikadi ya Uislamu (hapana Mola apasaye kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wake). Itikadi hii Imemtatulia mwanadamu maswali msingi yanayohusiana na ulimwengu, mwanadamu na uhai pale ilipoeleza kwamba nyuma ya vitu hivi kuna Muumba naye ni Allah (swt). Na kwamba vyote viko ndani ya nidhamu maalumu ambayo kila kimoja chake kamwe hakiwezi kujiondosha bali vyote vinamuhitajia Yeye Allah (swt). Na Mwenyezi Mungu kampa mwanadamu jukumu la kufanya ibada ndani ya umri wa maisha yake.
Ibada kwa maana ya kujifunga na maamrisho na kujiepusha na makatazo ya Mwenyezi Mungu mahali popote wakati wowote. Na lengo la kuishi duniani ni kwa ajili ya Uislamu na kazi ya kila siku ni kuulingania Uislamu. Ama furaha ya mwanadamu inatokana na kujifunga na twaa ya Mola wake na wasiwasi (kutokuwa na furaha) wake unatokana na kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Na aliye fanikiwa ni yule aliyepata radhi za Mola wake na afe akiwa ni Muislamu kivitendo na kauli huku akiwa na matarajio ya kuingizwa peponi adumu humo milele kwa Rehema za Mola wake Mlezi.
Ama kipimo ni halali na haramu na kwamba natija ya kudumu katika kutenda halali kunapelekea mwanadamu kuwa na sifa ya uchajiMungu.
Kwa masikitiko makubwa, hivi sasa Waislamu licha ya kuwa na itikadi safi itokayo kwa Mola wao aliyewaridhia katika Uislamu wao, Bado wengi wao ni mateka wa itikadi hii mbovu ima kwa kujuwa au kutojuwa. Kwa sababu wamezaliwa, wamelelewa na wamekulia ndani ya dola hizi za kikoloni zinazoendeshwa na mfumo wa kirasilimali wa kisekula ambao umewafanya wao kuufahamu Uislamu kimakosa na hivyo kuzidi kutumbukia na kubakia katika kiza cha usekula ambacho daima kinawatawala hadi sasa. Wamefahamu ibada kama suala la mtu binafsi na lililofungwa msikitini au nyumbani kwa mtu binafsi. Hivyo basi Muislamu huyu anakuwa mkali kafiri akitaka kumswalisha lakini Muislamu huyu anapotoka nje ya msikiti anampa uongozi na kujisalimisha kwa kafiri yule yule aliyempinga msikitini asimswalishe! Hatima yake ni Waislamu kuwa na maisha ya mbio usiku na mchana na huwezi jua tofauti ya Muislamu na Kafiri kwani wote wanakwenda mbio kutafuta furaha na mafanikio kwa mujibu wa mtizamo wa itikadi ya Usekula.
La msingi na linalotakiwa kwa Muislamu hivi sasa ni kuliendea mbio usiku na mchana suala la namna gani atakavyoirejesha tena serikali ya Kiislamu ya Khilafah. Serikali ambayo iliangushwa 28 Rajab 1342H sawia na 3 Machi 1924 na maadui wa Uislamu kwa ushirikiano na wanafiki ndani ya serikali hiyo wakiongozwa na Mustafa Kamal. Kupitia kusimama serikali hii ndiyo Waislamu watafahamu maana halisi na kuipata ladha ya furaha na mafanikio kwa mtizamo safi wa Uislamu utakaokuwa unasimamiwa na kiongozi MchaMungu asiyejali mipaka ya kikoloni wala mafungamano ya kirasilimali ya kisekula. Waislamu watamiliki hadhi na cheo juu ya mgongo wa ardhi kinyume na hali ilivyo sasa ambapo licha ya kuwa na itikadi safi, wengi kiidadi na mali nyingi bado damu zao ni kama za kunguni zinamwagwa kiholela ulimwenguni kote kila sekunde.
Chanzo kikubwa ni kukosekana kwa Serikali ya Kiislamu ya Khilafah itakayo washajiisha Waislamu kuwa wachaMungu kupitia sera ya elimu iliyo na lengo la kuwafinyanga Waislamu ili kuwa na Utambulisho wa Kiislamu.
Hadi pale ambapo Serikali ya Khilafah itakaposimama furaha na mafanikio itabakia kama kuutafuta unyoya wa mbu kwenye giza totoro. Isipokuwa wale ambao wamejifunga usiku na mchana katika Njia ya Mtume (saw) kuleta mageuzi juu ya mgongo huu wa ardhi wao pekee ndio wanaoifahamu furaha na mafanikio ya dunia hii kupitia kutumia mali/amana walizotunukiwa na Mwenyezi Mungu. Katika kufaulisha jambo hilo licha ya kuwa baadhi yao wamefungwa magerezani, wengine wakiwa katika hali ngumu zisizoelezeka na wengine wakipoteza maisha kamwe hawarudi nyuma katika ahadi walio muwekea Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume wake (saw) bali daima wanasonga mbele wakiwa na yakini iko siku wataipata furaha ya kweli nayo ni kufa wakiwa ni Waislamu na ilhali wamedumu katika msimamo wao.
Namuomba Mwenyezi Mungu awazindue Waislamu wote ili wafahamu jukumu lililoko shingoni mwao kuhusiana na kazi ya kusimamisha Serikali ya Kiislamu ya Khilafah. Na hatimaye wajiunge na ndugu zao wanaharakati wa Hizb ut Tahrir katika kufanya kazi hii yenye malipo makubwa hapa duniani na akhera. Na ambao tayari wameshajiunga basi awadumishe katika khair hiyo hadi mwisho wa pumzi zao. Ama wasiokuwa Waislamu Mwenyezi Mungu awazindue wausome Uislamu kwa moyo mkunjufu na wauone kama ndio suluhisho badala ya mfumo wao wa kisekula wa kirasilimali. Allahuma Amiin!
Ali Nassoro Ali
Mwanachama wa Afisi ya Habari Hizb ut Tahrir Kenya
Imetoka jarida la uqab: 20
https://hizb.or.tz/2018/09/03/uqab-20/
Maoni hayajaruhusiwa.