Waislamu na Matayarisho ya Ramadhani

Bila ya shaka si muda mrefu tukijaaliwa Waislamu tutafikiwa na mgeni mtukufu, mwezi wa Ramadhani. Huu ndio mwezi ulioteremshwa Qur-ani yote kuja katika wingu wa kwanza wa dunia. Ndani yake kuna usiku mtukufu kuliko miezi alfu, hufunguliwa milango ya Pepo, na kufungwa milango ya moto. Aidha, ni mwezi wa toba na maghfira kwa Waislamu. Pia AllahTaala humtia kifungoni Iblis aliyelaaniwa. Ni Ramadani tu ndio amali za Waislamu hulipwa maradufu, na nyoyo za Waumini hulainika kwa kupanda juu ucha-Mungu, ukarimu na mapenzi baina yao.

Kwa yote hayo, jee Waumini wana maandalizi yoyote kwa ajili ya mwezi huu mtukufu?
Bila shaka Waislamu hawako nyuma katika kujiandaa na Ramadhani katika mambo mbalimbali kama futari, kutafuta nguo za sikukuu, kushiriki mijadala (japo haina tija) juu ya muandamo wa mwezi nk.

Ramadhani inahitaji matayarisho mapana zaidi kwa kila Muislamu mbali na hayo yaliyozoeleka.
Jambo la kwanza kabisa, ni kumuomba Allah SW atufikishe kuidiriki Ramadhani, kwani wema waliotangulia (maswahaba) walikuwa ikimaliza tu Ramadhani wakimuomba Allah SW awakubalie funga na ibada zao. Na ukianza tu mfunguo saba walikuwa wakimuomba Allah Taala awafikishe waudiriki mwezi wa Ramadhani wakiwa na afya njema ili wanufaike na manufaa makubwa ambayo hayapatikani katika miezi iliyobakia.

Maandalizi mengine ni kuhakikisha Waislamu wanatafuta elimu kuhusu funga. Yaani wajue mambo yanayobatilisha swaumu, kusihi kwake, dalili zake nk. Ili mfungaji awe na uhakika kielimu na anachokitenda. Na kama Muislamu hujui basi ni lazima ajiegemeze kwa mwanazuoni Mujtahid ili iwe hujjah kwake kuwa katekeleza ibada hiyo kwa ujuzi. Allah SW anatukataza kutekeleza jambo tusilo na elimu nalo.

Aidha, Waislamu katika kipindi hiki wanapaswa kujiandaa kwa kuhakikisha hawazidhulumu nafsi zao kwa kufanya maovu, na badala yake wanaziokoa nafsi zao kwa kuhakikisha kumridhisha Allah Taala pekee kwa kuheshimu matukufu yake. Allah SW anasema :

إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِنْدَ اللَّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنْفُسَكُمْ (التوبة: 36

”Hakika idadi ya miezi mbele ya Allah SW ni kumi na mbili katika hukmu ya Allah tokea kuumbwa kwa mbingu na ardhi, katika hiyo imo miezi minne mitukufu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu ndani ya miezi hiyo….. (TMQ 9:36)

Na kwa upande wa Ramadhan ni bora zaidi kujiepusha (min baabu awla), kwa kuwa ni mwezi uliopata utukufu mkubwa zaidi kuliko miezi hii. Una usiku mmoja mtukufu kupindukia maelfu ya siku ya miezi hiyo.

Waislamu pia tunapaswa kujiandaa kifikra kabla ya kuingia Ramadhani, kwa kuweka azma ya kweli ya kuifunga Ramadhani yote kwa ikhlasi na unyenyekevu. Huku tukijiweka mbali na shubha zote. Tujiepushe kuibeba Ramadhani kama kero fulani au kufunga tu ilimuradi watu watuone, au kuogopa kusemwa vibaya ndani ya jamii. Mtume SAAW anatufundisha kuwa vitendo vitalipwa kwa kuzingatia nia ya mtendaji.

Kujitayarisha Waislamu pia kunahusisha kuanza kujizoesha kufanya ibada mbalimbali ili isije kuwawia Waislamu ugumu kuzitenda itakapoanza Ramadhani. Ni vyema kuanza kufanya baadhi ya ibada kama qiyamul-layli, kusoma Qura-ni kwa kuuzoesha ulimi, kufanya dhikri mbalimbali, kutoa sadaka nk.

Bibi Aisha Ra. anasimulia kuwa Mtume SAAW alikuwa akifunga zaidi mwezi wa Sha’abani mpaka unadhania hafungui ataunganisha na Ramadhani…” . Sasa kwetu ni vizuri kuiga mwendo huo mzuri, kama ni matayarisho kwa ibada hii hasa, na nyenginezo.

Kwa kumalizia, kwa kuwa Ramadhani ndio mwezi ulioshuka Qur-ani, ni wajibu kwa Waislamu kujitayarisha kuutekeleza Uislamu wote kijumla. Na hasa yaliyo ya faradhi, kwani Allah SW amewajibisha hilo kwa kutuwajibisha tuufuate Uislamu wote. Na kwa kuwa hili kwa leo haliwezekani kwa kuwa hatutawaliwi na Uislamu, basi ni wajibu Waislamu waweke maandalizi ya kubeba daawa ili kuutawalisha Uislamu katika kila kipengee cha maisha. Na kwa kuwa kipindi cha Ramadhani uchaji wa Waislamu unaongezeka na nyoyo zao hulainika na kuwa wasikivu, basi ni fursa adhimu kuwafikishia ulinganizi ili tushirikiane nao bega kwa bega kufanya kazi ya kutufikisha kuutawalisha Uislamu kupitia dola ya Kiislamu ya Khilafah na kuung’oa ukafiri na matawi yake yote.

Risala ya Wiki No. 36
02 Sha’aban 1440 Hijri /08 Aprili 2019 Miladi

Afisi ya Habari – Hizb ut- Tahrir Tanzania
https://hizb.or.tz/
https://www.facebook.com/Hizb-ut-Tahrir-Tanzania

Maoni hayajaruhusiwa.