Vita Vya Mu’tah
بسم الله الرحمن الرحيم
(Jumada Al-Ula 8 AH )
Tokea mwaka wa kwanza wa hijria Mtume (SAAW) alipoasisi serikali ya kwanza ya Kiislamu upinzani mkubwa ulikuwa ni kutoka kwa waarabu hasa maqureishi. Hivyo Mtume (SAAW) akasimama kupambana nao na kufikia mwaka wa 6 AH alifanikiwa kuzima upinzani huu kwa mkataba wa Hudaybia na akapata pia kumakinika kuvizima vitimbi vya mayahudi.
Kufikia hapo njia ya da’awa ilikuwa kwa kiasi kikubwa iko wazi kuelekea nje ya Jazirat-ul arab. Ndani ya mwaka wa 6AH barua zilipigwa muhuri wa Mtume SAAW kuelekezwa kwa watawala mbalimbali kuwalingania Uislamu. Ndipo upande wa Sham, sahaba Al-Harith bin Umair Al-Azdy (R.A) alitumwa na barua ya Mtume (SAAW) ili amfikishie mtawala wa Busra. Njiani gavana wa Al-Balqi anaejuulikana kwa jina la Shurahabil kwa kibri na jeuri walimfunga kamba na kumkata kichwa wakamuuwa balozi huyo wa Mtume SAAW.
Mtume (S.A.W) akaandaa jeshi kukabiliana na warumi waliokuwa watawala wa biladu Sham ndani ya mwezi kama huu wa mfunguo nane (jumadu l-ula) mwaka wa 8AH. Kikosi cha Waislamu kilielekea upande wa Kaskazini (Sham) huku idadi ya wapiganaji wa Kiislamu ilikuwa ni 3000. Wakati Waislamu wakipanga mikakati ya uvamizi wakapata taarifa kutoka Sham kwamba warumi wameshaandaa jeshi la wapiganaji 100,000. Kikosi cha Waislamu kikapiga kambi katika eneo la Ma’an mpakani na Syria kujadili cha kufanya. Amma kitume ujumbe kwa Mtume (SAAW) awaongezee wapiganaji na kusikiliza amri yake itakayokuja au wasonge mbele na idadi yao chache. Hapo akasimama sahaba Abdallah bin Rawah, mmoja wa majemadari akasema: “Sisi hatupigani na makafiri isipokuwa kwa ajili ya Uislamu uliotutukuza, hivyo ni moja kati ya mawili, shahada au ushindi”. Jeshi la Kiislamu likapata motisha kwa maneno ya sahaba huyo, na hapo likasonga mbele kupambana na jeshi wasiloliafikia hata robo ya jeshi lao.
Mtume SAAW alikwishapanga majemadari wa vita hivi, na wa awali ni Zaid bin Harthah ambae alishika bendera ya Waislamu akaongoza jeshi mpaka akapata shahada. Hapo akafuatia Jaafar bin Abu Talib kuongoza jeshi naye akauwawa shahid, na hivyo jemadari wa tatu akawa Abdallah bin Rawah nae pia akapata shahada. Waislamu wakamchaguwa Khalid bin Walid kuwa jemadari wa nne baada ya wale majemadari waliochaguliwa na Mtume SAAW kupata shahada. Khalid akatafakari na akabuni mkakati maalum wa kukiokoa kikosi cha Waislamu. Alibadilisha utaratibu wa jeshi la Waislamu kwa ujanja na warumi wakadanganyika kwa kudhani jeshi jipya la Waislamu limekuja kuwapa nguvu na kuungana na jeshi la awali. Kwa mkakati huu Khalid bin Walid alikiokoa kikosi kilichobaki cha Waislamu na kurejea Madina salama usalimini.
Vita hivi vinatufundisha kwamba Muislamu awe tayari kuutetea Uislamu katika hali yoyote hadi kutoa nafsi yake. Kikosi cha Waislamu bila ya shaka kilitambua kuwa kukabiliana na jeshi kubwa mara 30 ya jeshi lao ni kujiingiza kwenye mauti lakini walifanya muhanga wa hali ya juu katika vita hivi vilivyokuwa vikali sana. Waislamu walifahamu kwamba Mwenyezi Mungu ananunua nafsi na mali za Waislamu kwa ajili ya kuwalipa pepo:
إِنَّ اللَّهَ اشْتَرَى مِنْ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ بِأَنَّ لَهُمْ الْجَنَّةَ ِ
“Hakika M/Mungu amenunua kwa waumini nafsi zao na mali zao kwa (kuwalipa)pepo”
(TMQ Tawba:111)
Maoni hayajaruhusiwa.