Uzawa wa Mtume ni Bishara ya Ushindi Wetu

Amesema Mtume SAAW :
“Mimi ni dua ya baba yangu Ibrahim, ni bishara ya Issa, na mama yangu aliona ndotoni akitoka nuru (tumboni) kuyaangazia maqasri ya Sham”.

(Imam Ahmad)
Kipenzi chetu Mtume SAAW ni dua ya Ibrahim As. kama Quran inavyotukumbusha:

“Ewe Mola wetu! Waletee Mtume anaetokana na wao”

(Baqara : 129)
Na pia ni bishara ya Issa As. alipowaeleza wana wa Israil kama ilivyotajwa ndani Quran.

”Na mimi ni Mwenye kuwabashiria Mtume baada yangu, jina lake ni Ahmad”.

Amma kutoka nuru tumboni ni ndoto aliyoiona mama yake Mtume SAAW alipokuwa mja mzito akiwa na mimba ya Kipenzi chetu Muhammad SAAW. Nayo ni bishara ya ushindi unaoendelea wa Ummah wake mpaka siku ya kiyama. Licha ya Ummah wake kusibiwa na kufikwa na mitihani na kutetereka hapa na pale kama hali tuliyonayo leo tangu kuangushwa Khilafah.

Ikifafanua zaidi bishara hii ya ushindi Tafsiri ya Mukhtaswar Ibn Kathir inanena haya:

‘ Na kuhusishwa Sham katika bishara hii ni kutokana na ukweli kwamba Sham itakuwa ndio Makao makuu ya Uislamu katika zama za mwisho (akheri zaman).
Kama alivyosema Mtume SAAW:

”Halitoacha kundi katika Ummah wangu kusimama juu ya haki, halitodhurika kwa atakaelipinga , wala halitodhoofika kwa kuwachwa mkono mpaka ije amri ya Mungu (ushindi) Nalo litatoka Shaam”

(Bukhar na Muslim) (Mukhtaswar Ibn Kathir vol. 1 aya 129 Surat Baqara).

Maeneo ya Sham yanahusisha Syria, Lebanon, Palestina, Jordan, na baadhi ya maeneo ya Iraq. Bishara hii ni moja katika nyingi juu ya ushindi wa Ummah huu, kama vile pia alivyosema Mtume SAAW:

“Hakika Allah amenisogezea dunia yote nikaona kutoka mashariki mpaka magharibi .Na kwa hakika utawala wa ummah wangu utafika sehemu zote nilizosogezewa. Na nimepewa khazina mbili, nyekundu na manjano. (Muslim)

Aidha, kuna bishara ya kurudi tena Khilfah, baada ya watawala waovu, inayosema:
‘kisha itarudi tena Khilafah kwa manhaj ya Utume… au alipobashiri Mtume SAAW kuifungua/fathi Constatinople/Uturuki iliyofunguliwa na Khalifah Muhammad Fathi, na kufunguliwa kwa Rome ambayo bado haijafunguliwa hadi leo, lakini ufunguzi wake hauna shaka insha-Allah.

Bishara hizi ni ushindi kwa Ummah huu, lakini ni lazima tuweke ufahamu wa kina juu ya dhana na makusudio ya bishara. Kwa kuwa makafiri huleta ufahamu wa kimakosa kiasi cha kuwachanganya hata Waislamu wenye ikhlasi.
Kuamini bishara huingia katika mambo ya kiimani /kiakida, nako ni kuamini mambo ya ghaib ambayo Muislamu huwajibika kuyaamini kama yalivyo, bila ya kutoa vigezo vya kiakili wala kutizama mawafikiano ya bishara hiyo na mazingira yaliyomzunguuka.

Pili, kuamini bishara maana yake sio kujipweteka na kusubiri bishara hiyo ijiri, na kuacha kufanya kazi ya ulinganizi wa kurejesha dola, au kusema kama wanavyosema baadhi ya watu kwamba hakuna haja ya kushughulika kwani ‘Khilafah ni ahadi ya Allah Taala’. Hapana shaka  Khilafah ni ahadi ya Allah Taala hakuna anayelipinga hilo, lakini sheria imetufunga kufanya matendo maalum kuiendea bishara hiyo, na kufanya matendo hayo au kutofanya, hakuzuii bishara husika kujiri. Lakini lau hatukufanya matendo tuliyoamrishwa katika mzunguuko wetu wa kibinaadamu tutakuwa na dhambi, kwa kuwa sheria imetutaka tufanye matendo hayo.

Hakuna mbora wa kufahamu bishara ya ushindi kama kipenzi chetu Mtume SAAW, lakini alihangaika kutafuta nusra kwa makabila mbalimbali ili asimamishe dola, alihajiri Makka kwa siri, alijificha, alikodi mjuzi wa njia, alipigana jihadi nyingi nk. Yote haya si kwa sababu alikuwa na shaka juu ya ushindi alioahidiwa na Mola wake, bali matendo haya huingia katika upande wa amri za Allah Taala ambazo aliwajibika atende na sio kujipweteka kusubiri ushindi. Na masahaba nao walielewa vyema kuhusu bishara na hawakuwa na shaka juu ya bishara mbali mbali, lakini walifanya matendo waliyotakikana na sheria kuyatenda.

Tatu, bishara tulizopewa lazima zitulize nyoyo za Waislamu na sio kutapatapa na kujiingiza katika aibu, fedheha na mitego ya makafiri, kana kwamba hatuna mfumo kamili wa maisha wenye manhaj/njia yake yenye kujitosheleza katika kila kitu. Hivyo, lazima tujiamini na Uislamu wetu ambao bishara ya ushindi iko upande wake.
Mtume SAAW hata katika hali ngumu ya kuteswa watu wake, kutengwa kwa vikwazo, kuuliwa wafuasi wake, kunyanyaswa nk. kamwe hakujiingiza kuunga mkono tawala za kikafiri wala taratibu/nidhamu zao.
Na kwa hakika katika tareekh makureishi walidhamiria kumpa yeye jambo kubwa zaidi, yaani kupewa ufalme kamwe, lakini alikataa kata kata.

Au pia alipoona masharti ya baadhi ya makabila yaliyotaka kumpa nusra ya kusimamisha dola yanapingana na Uislamu kama vile kabila Amr bin S’asah walipotaka kumpa utawala uwe katika mikono ya kabila hilo pia Mtume SAAW alikataa kata kata.
Au pale kabila la Bani Shayban nao walipompa masharti ya kuwa wampe Mtume SAAW hatamu za madaraka lakini kwa sharti asipigane vita na mafursi, kwa kuwa kabila hilo walikuwa na mkataba na Mafursi wa kutukuwepo mapigano baina yao, Mtume SAAW pia alilikataa jambo hilo. Aliyakataa masharti hayo yote na akasimama na msimamo thabiti wa Kiislamu wala hakuleta kisingizio cha maslahi ya Waislamu. Licha ya kujua kwa yakini kwamba watu wake wanateswa, wana tabu, mashaka kiasi cha kuwa hali mbaya ya kuhitaji nusra ili wapate faraja.

Ajabu ! Ambayo baadhi ya Waislamu hawaizingatii ni kwamba makafiri hawaongozwi na wahyi, wala hawana bishara yoyote upande wao, bali wanaongozwa na matamanio yao na mipango ya akili zao finyu. Lakini wao wanajiamini katika kusukuma ajenda zao za kipotofu na huzileta kwa Wislamu moja kwa moja (radically) bila ya kusita sita, kama tunavyoshuhudia suala la ushoga namna nchi za magharibi wanavyolivalia njuga bila ya kujali dini mila wala desturi za watu. Basi iweje sisi Waislamu ambao Allah Taala yuko upande wetu, bishara za kipenzi chetu SAAW ziko upande wetu na tunafuata dini ya haki, kwanini tusiubebe Uislamu wetu katika hali ya kuwa kifua mbele na kujiamini.

Katika kipindi hiki cha Mfungo sita (Rabiul Awwal) tunachokumbuka uzawa wa kipenzi chetu Mtume Muhammad SAAW ambae katumwa kuwa ni nuru ya kuangazia dunia na wanadamu wote, ni jambo muhimu kwa Ummah wetu wa Kiislamu kurejea juu ya mstari wetu kama alivyotuonesha Mtume SAAW kivitendo. Pia kwa wasiokuwa Waislamu wakati umefika wa kuchunguza na kutafiti kwa uadilifu mafunzo na masuluhisho yaliosheheni nuru ya Mtume SAAW ambae ametumwa kwa watu wote.

قُلْ يَاأَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا
Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote …………’

(TMQ 7: 158)

#MuhammadNiNuruKwaUlimwengu

Maoni hayajaruhusiwa.