Usiuze Usichokuwa Nacho!

بسم الله الرحمن الرحيم

Swali:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakaatuh

Mwenyezi Mungu akudumishe kuwa rasilimali kwa ajili ya Uislamu.

Natarajia kuwekewa wazi maudhui ya “usiuze usichokuwa nacho”. Je, inahusu kila bidhaa inayouzwa? Ama ni makhsusi tu vyakula?

Kwa mfano: mfanyibiashara anayeuza vitu vya ujenzi kama simiti na mchanga n.k [anapokuja mtu] na kutaka chuma, na ikawa hana, akawasiliana na muuza vyuma ili amtumie kiasi cha chuma kilichotakiwa. Ni ipi hukmu ya hali hii?

Angalizo:

Kabla ya hapo huwa kuna makubaliano ya bei kati ya mfanyibiashara na yule muuza vyuma.

Mfano mwengine: mtu amenunua bidhaa na kabla ya kukabidhiwa akamuuzia mtu mwengine. Je, hii pia yaingia kwenye kuuza usichokimiliki?

Jibu:

Wa Alaikum Assalam Wa Rahmatullah Wa Barakatuh,

Katazo la kutouza asichokuwa nacho mfanyibaishara linaenea kwa vyakula na visivyokuwa vyakula pia, chochote ambacho kinaweza kupimwa kwa mizani au kwa idadi. Na tumelifafanua hilo kwenye kitabu cha “Nidhamu ya Kiuchumi” chini ya anwani “haifai kuuza usichokuwa nacho”. Na nitakunukulia yafuatayo:

[Hairuhusiwi kuuza usichokuwa nacho: haifai kuuza bidhaa kabla ya kuimiliki kikamilifu, na iwapo ataiuza katika hali hii basi uuzaji unakuwa batwil. Na hili linahakikishika katika hali mbili:

Kwanza: ikiwa mtu atauza bidhaa kabla ya kuimiliki.

Pili: kuiuza baada ya kuinunua lakini kabla ya kuimiliki kikamilifu kwa kukabidhiwa – ikiwa ni bidhaa ambayo ni sharti kukabidhiwa ili kuimiliki kikamilifu – kwa sababu, mkataba wa kuuza huwa juu ya kinachomilikiwa [na muuzaji] ama kitu ambacho bado hakijamilikiwa… au mtu amekinunua lakini hajakimiliki kikamilifu… kama hajakabidhiwa, basi itakuwa haiwezi kufungiwa mkataba wa uuzaji. Kwa kuwa hakijapatikana kitu ambacho kitafungiwa mkataba wa uuzaji kisheria. Kwa hakika amekataza Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) mtu kuuza kitu asichokimiliki. Imepokewa kutoka kwa Hakeem bin Hizaam akisema:

«قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، يَأْتِينِي الرَّجُلُ يَسْأَلُنِي الْبَيْعَ لَيْسَ عِنْدِي مَا أَبِيعُهُ، ثُمَّ أَبِيعُهُ مِنْ السُّوقِ»، فقال: «لَا تَبِعْ مَا لَيْسَ عِنْدَكَ»

Nilisema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, najiwa na mtu akitaka nimuuzie nisichokuwa nacho, kisha mimi hukinunua kutoka sokoni” akajibu: “Usiuze kitu usichokuwa nacho” (Imepokewa na Ahmad)

Na imepokewa kutoka kwa Amr bin Shuaib, kutoka kwa babu yake, akisema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):

«لَا يَحِلُّ سَلَفٌ وَبَيْعٌ، وَلَا شَرْطَانِ فِي بَيْعٍ، وَلَا رِبْحُ مَا لَمْ تَضْمَنْ، وَلَا بَيْعُ مَا لَيْسَ عِنْدَكَ»

“Si halali kuchelewesha na kuuza hapo hapo, wala sharti mbili ndani ya uuzaji mmoja, wala faida ya usichodhamini, wala kuuza usichokua nacho” (Imepokewa na Abu Daud)

Tamko la Mtume aliposema “usichokuwa nacho” ni “jumla” linaenea, hivyo inaingia chini yake kitu chochote kisichokuwa katika umiliki wako, na pia usichoweza kukabidhi, na vilevile kitu ambacho hukijamiliki kikamilifu. Na hayo yanatiliwa nguvu na hadithi zilizokuja kukataza kuuza kitu ambacho hujakabidhiwa – ikiwa ni bidhaa ambayo ni sharti kukabidhiwa ili kuimiliki kikamilifu – kwa sababu, [hizo hadith] zinajulisha kwamba, mtu anayenunua kitu kinachopaswa kukabidhiwa ili ununuzi wake utimie, [kwa hali hii] haifai kwake kukiuza hadi pale atakapokabidhiwa, kwani [bila hivyo] hukmu yake itakuwa ni ya kuuza kitu usichomiliki. Kwa kauli yake Mtume (saw): «مَنْ ابْتَاعَ طَعَاماً فَلَا يَبِعْهُ حَتَّى يَسْتَوْفِيَهُ» “Yeyote atakayenunua chakula basi asikiuze hadi atakapokabidhiwa” (Imepokewa na Bukhari) na kwa hadith ilipokewa na Abu Daud:

«أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ نَهَى عَنْ أَنْ تُبَاعَ السِّلَعُ حَيْثُ تُبْتَاعُ، حَتَّى يَحُوزَهَا التُّجَّارُ إِلَى رِحَالِهِمْ»

“Kwamba Mtume (saw) amekataza bidhaa zisiuzwe hadi pale wafanyibiashara watakapokabidhiwa kwenye makazi yao”. Na kwa hadith ilipokewa na ibn Majah:

«أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ نَهَى عَنْ شِرَاءِ الصَّدَقَاتِ حَتَّى تُقْبَضَ» “Kwamba Mtume (saw) amekataza kununua sadaka hadi zitakapokabidhiwa kwa wenyewe”. Na kwa hadith ilipokewa na Al-Baihaqi kutoka kwa ibn Abbas, alisema, kwamba pindi Mtume (saw) alipomtuma Uttab bin Usayd Makkah alisema:

«إِنِّي قَدْ بَعَثْتُكَ إِلَى أَهْلِ اللَّهِ، وَأَهْلِ مَكَّةَ، فَانْهَهُمْ عَنْ بَيْعِ مَا لَمْ يَقْبِضُوا»

“Mimi nimekutuma kwa watu wa Mungu na watu wa Makka, wakataze wasiuze kitu ambacho hawajakabidhiwa”.

Hadithi hizi ziko wazi katika kukataza kuuza chochote ambacho hujakabidhiwa, kwa sababu muuzaji hajakimilki kikamilifu. Na kwa sababu kinachohitaji kukabidhiwa hakiwezi kumilikiwa mpaka mnunuzi akitie mkononi, na kwa kuwa ni katika dhamana ya muuzaji wake. Kutokana na hayo, yabainika kwamba ili uuzaji uswihi basi ni sharti awe muuzaji ameimiliki bidhaa na tena umiliki uliotimia. Ama akiwa hajaimiliki, au ameimiliki lakini umiliki sio kamili, basi haitofaa kwake kuiuza hiyo bidhaa moja kwa moja. Na hii inaenea kila kitu ambacho umekimiliki ila hujakabidhiwa – ikiwa ni bidhaa ambayo ni sharti kukabidhiwa ili uuzaji utimie- nayo ni chochote cha kupimwa au kuhesabika. Ama bidhaa isiyosharutiwa kukabidhiwa ili umiliki kutimia -nayo ni bidhaa yoyote isiyopimwa au kuhesabika, kama vile wanyama, nyumba, ardhi na mfano wake… hizi yaruhusiwa kwa muuzaji kuuza hata kabla ya kukabidhiwa. Kwa sababu kwa mujarabu wa kufungwa mkataba tu kwa ijaab na qabul basi tayari uuzaji ushatimia, sawa awe amekabidhiwa au la, na atakuwa ameuza kitu alichokimiliki kikamilifu. Kwa hiyo, suala la kutouza halifungamani na kukabidhiwa au kutokabidhiwa, bali linahusiana na umiliki wa kinachouzwa, na ukamilifu wa huo umiliki.

Ama suala la kuruhusiwa kuuza kitu ambacho hujakabidhiwa -kisichopimwa au kuhesabiwa – hilo limethubutu kwa hadith sahihi. Amepokea Bukhari kutoka kwa ibn Umar kwamba Umar alikuwa na ngamia mzito wa mwendo juu ya Abubakar,

«فَقَالَ لَهُ النَّبِيُّ ﷺ بِعْنِيهِ، فَقَالَ عُمَرُ: هُوَ لَكَ فَاشْتَرَاهُ ثُمَّ قَالَ: هُوَ لَكَ يَا عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عُمَرَ، فَاصْنَعْ بِهِ مَا شِئْتَ»

“Mtume (saw) akamwambia: niuzie mimi, Umar akamjibu: sawa ni wako, basi akamnunua, kisha akasema: huyo sasa ni wako Ewe Abdullah bin Umar mfanyie utakavyo” na huku ni kutasaraf katika kitu kilichouzwa kabla ya kukabidhiwa kwa kutoa tunu, na inajulisha ufaaji wa kukiuza pia, kwa sababu muuzaji tayari ashamiliki kikamifu.

Hivyo basi, chochote anachomiliki muuzaji na akawa amekimiliki kikamilifu basi ataruhusiwa kukiuza. Na kitu ambacho hakimiliki au hajakimiliki kikamilifu haitofaa kwake kukiuza. Na kwa hiyo, kitendo kinachofanywa na wafanyibiashara wadogo wadogo kuelewana bei na mnunuzi  juu ya bidhaa kisha kumuuzia, halafu kwenda kwa mfanyibiashara mwengine ili kununua hiyo bidhaa kutoka kwake na kisha kuileta na kumpa mnunuzi… hiki kitendo hakifai, kwa sababu ni kuuza usichokimiliki. Kwa kuwa yule mfanyibiashara alipoulizwa bidhaa hakuwa nayo wala hakuwa ni mwenye kuimiliki, ila yuajua kwamba ipo sokoni kwa mtu mwengine, halafu humdanganya mnunuzi na kumwambia kuwa yuko nayo na kumuuzia, kisha ndipo huenda kuinunua baada ya kuwa tayari ashaiuza! Kitendo hiki ni haramu na haifai. Kwa sababu ameuza bidha ambayo bado hajaimiliki.

Vilevile, kitendo kinachofanywa na baadhi ya wenye maduka ya mboga, mtama, na nafaka zengine, wanauza mboga au nafaka yoyote kabla hawajazimiliki kikamilifu! Kwani baadhi ya wafanyibiashara hununua mboga, mtama, au nafaka kutoka kwa wakulima, halafu wanauza hata kabla hawajakabidhiwa! Hiki kitendo hakifai kwa sababu, hizi [mboga, nafaka] ni katika vyakula, na ni vitu ambavyo umiliki wake hautimii ila kwa kukabidhiwa.

Hivyo hivyo, kitendo kinachofanywa na wanaoingiza bidhaa kutoka miji mengine, kwani baadhi yao hununua bidhaa na huweka sharti ya kufikishiwa mji alioko, kisha anauza hata kabla hazijafika… yaani, hata kabla hajazimiliki kikamilifu. Huu ni uuzaji haramu, kwa sababu ni kuuza kitu ambacho bado hajakimiliki kikamilifu”].

Kiufupi: ni kwamba, kuuza kitu usichokuwa nacho -yaani hukimiliki -au hujakabidhiwa, hilo halifai. Na hiyo [hukmu] inaenea kitu chochote kinachopimwa au kuhesabiwa, haijalishi iwe ni chakula au la. Ama ikiwa uuzaji wake sio kwa kipimo au hesabu -kama vile wanyama, nyumba, ardhi, na mfano wake – basi itaruhusiwa kuuza pale tu mkataba unapokamilika kwa ijaab na qabul. Utakua umiliki wake umetimia kwa huo mkataba. Ama kukabidhiwa sio sharti katika hali hii kama ilivyobainishwa huko juu kwenye kitabu cha Nidhamu ya Kiuchumi.

Kwa hiyo, huyo mfanyibiashara wa vyuma na simiti … haifai kwake kuuza kitu asichokuwa nacho, bali ni anunue kwanza [bidhaa] kisha akabidhiwe – yaani aihamishie dukani kwake – halafu aionyeshe kwa ajili mauzo. Na kama tulivyosema, hii ni kwa kitu chochote kinachopimwa au kuhesabika, na huuzwa hivyo. Ama ikiwa ni kitu kisichopimwa au kuhesabika basi itatosha tu kukimiliki na si lazima kukabidhiwa kama tulivyobainisha.

Nataraji hayo yanatosheleza, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mwenye hekima zaidi.

Ndugu Yenu,

Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

1 Jumadal Al-Awwal 1443 H

5/12/2021 M

Link ya jibu hili kutoka kwa ukurasa wa Amiri wa Facebook

Maoni hayajaruhusiwa.