Uovu wa Ubepari Na Uadilifu wa Uislam

Hakika yanayofanywa na mataifa makubwa leo katika ardhi za Waislamu ni mambo yenye kupasua moyo kwa uovu uliopindukia ambao hata wanyama wakubwa ndani ya mbuga za wanyama hawathubutu kuwafanyia wanyama wengine.

Leo tunashuhudia damu tukufu za Waislamu zikimwagika kuanzia Syria, Palestina, Iraq, Afghanistan, Burma, Yemen nk. Kila kukicha watoto wadogo wanauwawa kutoka Yemen, Syria, Burma nk. Kiasi kufikia leo zaidi ya watoto elfu wamezaliwa mwaka huu ndani ya kambi za wakimbizi wa Rohingya ndani ya Bangladesh kutokana na kubakwa na wanajeshi wa kishirikina wa kibudha huko Burma.

Aidha, tumeshuhudia mara kadhaa matumizi ya silaha za sumu kama vile kijidola cha Israel na serikali ya Syria chini ya rais Bashar wanavyotumia silaha za sumu na mabomu ya phosphorus dhidi ya Waislamu wa Ghaza, tena katika maeneo ya makazi ya watu. Yote haya yanatendeka kwa kukosa ubinadamu yakisukumwa na mfumo wa kinyama na ukatili wa kibepari usiojali utu wala huruma.

Uislamu uko tofauti na ubepari kutokana na vipimo vyake vya matendo. Vipimo vya matendo Kiislamu ni ‘halali’ na ‘haram’ na lengo la kutenda ni kupata radhi za Allah sw. Hilo huwa ndio msingi wa kumsukuma Muislamu katika kutenda, kinyume na ubepari, ambao kwao kipimo ni maslahi kwa mujibu wa akili  huku lengo kuu ni kujistarehesha.

Msukumo huu wa kipekee katika matendo ya mwanadamu ndio ambao umeufanya Uislamu na Waislamu kwa zama zote kuwa uwa la waridi katika karne zote ilioutawala ulimwengu na kuacha athari ya kihistoria ya kipekee.

Amesema Allah Taala :

وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُوا اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى َ

(المائدة: 8….

 “Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutowafanyia uadilifu, fanyeni uadilfu kwani ndio kujikurubisha zaidi katika uchamungu”

(TMQ 5:8)

Msukumo huo ndio uliowafanya Waislamu wakati wote kuwa waadilifu hata pale walipokuwa na nguvu, athari na mamlaka katika ulimwengu. Kamwe hawakuzitumia nguvu na uwezo wao katika kutenda dhulma, ukatili wala kuwadhuru wengine.

Mfano hai ni Jemadari na sahaba mkubwa Khalid bin Walid ra. wakati alipofungua/ fathi ndani ya nchi ya Iraq, alipofikia katika kanisa linalojulikana kama ‘kisima cha tende’ katika vijiji vya Iraq, hapo Khalid bin Walid akakuta vijana arobaini wa kinaswara wakijifundisha kitabu cha biblia wakiandaliwa kwa ajili ya kuueneza na kuhubiri unaswara/ ukiristo maeneo mengine. Jemadari Khalid akaamiliana na vijana hao kwa uadilifu na inswafu, hakuchoma moto kanisa lao, hakuwatesa, wala hakuwalazimisha kuingia katika Uislamu. Bali aliwapa fursa kwa uadilifu kuufahamu Uislamu

Kati ya vijana hao walikuwemo vijana watatu: Syrin, Yasaar na Nasiir, na baada ya kufunguliwa Iraq kikamilifu vijana hao wote watatu waliona nuru, uadilifu na inswafu ya  Uislamu,  ukawaathiri na wakasilimu.

Kijana Syrin akazaa mtoto anaetambulika kwa jina la Muhamad bin Syrin, huyo akawa mwanachuoni mkubwa zama za Tabiin katika fanni ya Hadith, fiqhi na elimu ya wapokezi. Pia, kijana Yasaar nae akapata mtoto anayejuulikana kama  Ishaq Abu Muhammad bin Ishaq bin Yasaar, nae akawa bingwa katika fanni ya Seerah na mwanachuoni mkubwa, ambaye pia ndio mwalimu wa mwanatarekh mkubwa wa Kiislamu (Ibn Hisham). Halkadhalika, kijana Nasiir, ndie akawa ndio baba mzazi  wa Jemadari Musa bin Naswir aliyeongoza Waislamu katika  fathi/ufunguzi wa  Andalus (Spain) na Kaskazini mwa Afrika.

(Al-Bidaya wa Nihaayah ) Huo ndio Uislamu, na hivyo ndivyo ulivyobebwa na Waislamu zama zote, na ndivyo utakavyobebwa na dola ya Kiislamu ya Khilafah Rashidah, ambao umeweka nidhamu thabiti katika kila kipengee ikiwemo katika miamala ya kivita.

Ust. Issa Nasibu

Maoni hayajaruhusiwa.